Alhamisi, 19 Juni 2014


Umati mkubwa wa watu wakishuhudia basi la New Force muda mchache baada ya kupata Ajali
Taarifa kutoka Igurusi zinasema jana mida ya jioni Basi la New Force lililokuwa likitoka Dar es salaam kuja wilayani Kyela limepata Ajali Mbaya eneo la Igurusi na kusababisha Vifo vya watu wawili waliokuwa wakipita njia kwa miguu papo hapo na kujeruhi abiria wengine Arobaini ambao wamekimbizwa Hospitali sasa na kusaidiwa.
Akizungumza na KYELA Nyumbani mmoja wa abiria aliyekuwepo kwenye gari hiyo bwana Ibra Mwangimba alisema "Hakika watu hawana ubinadamu kabisa badala ya kuokoa majeruhi wao wanakimbilia kuiba mizigo na vitu."Bwana Mwangimba aliendelea kwa kumshukuru Mungu kwa kuokoa uhai wake kwa dakika zile ngumu.
Endelea kufuatilia tunakuletea habari kamili
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya Viwanja vya Bunge, Lowassa alisema Serikali ni lazima ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini. Wasomi hao wa fani mbalimbali walijitokeza katika uwanja huo Ijumaa iliyopita, kuanzia saa 12 asubuhi wakisubiri kufanyiwa usaili huo. Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la ajira na akisema ni bomu linalosubiri kulipuka. lowassa Mbunge huyo wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia kwenye malumbano makali na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka kuhusiana na suala la ajira kwa vijana. Kabaka akiwa bungeni, Machi 21, 2012 alitoa takwimu za namna Serikali ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye alikuwa ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana. Jana, Lowassa kuongezeka kwa makundi ya vijana wanaopora watu katika maeneo mbalimbali nchini ni ishara ya ukosefu wa ajira. “Watanzania sasa tupo milioni 48 na kila mwaka vijana zaidi ya 30,000 wanahitimu vyuo vikuu na kazi hakuna, pamoja na hilo hatuambiwi ni vijana wangapi ambao hawana kazi,” alisema Lowassa.
Alisema lazima Serikali itengeneze ajira kwa wananchi wake, huku akimtolea mfano Rais wa Marekani, Barack Obama kwamba alishinda awamu ya pili kwa sababu ya kutengeneza ajira.
“Mfano mzuri ni katika uanzishwaji wa viwanda. Tunapofikiria kuanzisha kiwanda cha pamba kwanza lazima tuangalie tutatengeneza ajira ngapi,” alisema.

Katika kuonyesha kuwa ajira sasa ni tatizo nchini, juzi jioni wakati wa mjadala wa Bajeti Kuu, Naibu Spika Job Ndugai alisema Mtanzania mwenye nia ya kugombea urais mwaka 2015 ili aweze kuelekewa kwa wananchi ni lazima aeleze mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na vyuo vikuu.
Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za mwisho za Serikali ya awamu ya nne, wale wanaojipanga kwa awamu ya tano kama hawataongelea ajira basi waandike wameumia.”
Ndugai alisema vijana wasio na kazi ndiyo wapigakura wakubwa na kusisitiza kuwa mgombea yeyote makini ni lazima afikirie suala la ajira kwa vijana.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema: “Vijana 10,500 kufanya usaili wa nafasi 70 ni janga la taifa. Yupo kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliwahi kulizungumza hili lakini akapondwa kwamba anazungumza mambo kwa kuzua. Sasa huu ndiyo ukweli wenyewe.”

Jumatatu, 16 Juni 2014


Waziri Mwakyembe akipiga mpira kama ishara ya kuzindua ligi hiyo

div class="separator" style="clear: both; text-align: center;">




WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe,amezindua rasmi ligi ya mpira wa miguu itakayowashirikisha madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda inayojulikana na Cocacola bodaboda cup 2014. Uzinduzi huo ulifanyika jana jumamosi katika viwanja vya Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe iliyopo Ilomba jijini Mbeya ambapo zvikundi kumi vya madereva wa bodaboda vitashiriki ligi hiyo. Akizindua ligi hiyo Mwakyembe amewataka madereva wa bodaboda kuendesha pikipiki zao kwa uangalifu na kuacha ulevi ili kupunguza ajali zisizokuwa za lazima. Alisema waendesha boda boda wanapaswa kutumia mashindano kama njia ya kujikumbusha juu ya masuala muhimu ya usalama barabarani kwa kuepuka ulevu watumiapo vyombo hivyo huku akipongeza wadau wa michezo mkoani hapa kwa kuleta mapinduzi katika michezo nchini. Alisema uwepo wa mikakati madhubuti baina ya wadau wa michezo mkoani Mbeya umewezesha kuibuka upya kwa amani,mshikamano na upendo baina ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya na kusababisha mshikamano wa hali ya juu tofauti na miaka kadhaa iliyopita. Dk Mwakyembe pia aliwataka waratibu wa mashindano hayo kampuni ya City Sign Promotion and Marketing Agency kuwaalika wabunge wote wa Mkoa wa Mbeya siku ya mchezo wa fainali ili kwa pamoja waweze kujionea namna michezo ilivyowezesha watu wa makundi yote kukutana na kuzungumza mambo ya msingi wakiweka tofauti zao pembeni.
Awali mmoja wa Wakurugenzi wa City sign Promotion, Geofrey Mwangunguru alisema timu zinazoshiriki michuano hiyo zimegawanywa katika makundi mawili ya A na B ambapo kila kundi lina jumla ya timu tano na kila kundi litatoa timu mbili zitakazoingia hatua ya nusu fainali na baadaye kupatikana bingwa wa michuano.
Aidha Mwangunguru alisema dhamira ya kuanzisha ligi hiyo ni kutambua mchango wa sekta hiyo katika usafirishaji pamoja na kuwaunganisha na jamii ambayo imekuwa ikiamini kuwa kundi hilo halipaswi kuweko katika jamii.
Aliongeza kuwa kabla ya kuanzisha kwa ligi hiyo kampuni yake ilijiwekea vipaumbele vitatu ambavyo ni kuhakikisha umoja wa bodaboda unaanzisha saccoss, kujiunga na taasisi za Pensheni pamoja na kutafuta bima za afya kwa ajili ya maisha yao kutokana na ajali za mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Mwangunguru katika kundi A zipo timu za waendesha bodaboba za Mbalizi standi Umalila,Iyunga,Shewe Sae,Kadege na Uyole wakati kundi B zipo timu za Mbalizi standi Chunya,Ilomba,Soweto,Kabwe na Mafiati.
Mwangungulu alisema bingwa wa mashindano hayo yatakayoendeshwa kwa muda wa siku 31 anatarajiwa kuzawadiwa pikipiki aina ya Boxer yenye thamani ya shilingi milioni 2.5,mshindi wa pili shilingi laki saba,mshindi wa tatu shilingi laki tatu na mfungaji bora shilingi laki moja.
Naye Katibu wa Umoja wa waendesha boda boda Mbeya, Msenda Mdesa, akisoma Risala mbele ya Mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Waziri wa Uchukuzi Dk. Harison Mwakyembe, alisema umoja huo umefanikiwa kuwaunganisha madereva wa bodaboda Mkoa mzima.
Aliongeza kuwa kutokana na umoja huo wamefanikiwa kuanzisha benki yenye wanachama 312 iliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria za uanzishwaji wa benki na kupewa Baraka zote na Benki kuu ya Tanzania.

Alhamisi, 12 Juni 2014

Zifuatazo ni dondoo za timu mbalimbali kuelekea kombe la dunia Brazil kabla hatujaangalia kundi A linafungua dimba leo Leo ndio siku ya siku! Mashindano ya kombe la dunia yatang'oa nanga leo huko Brazil. Mji wa Sao Paolo kutakako fanyika sherehe za ufunguzi rasmi wa mashindano hayo na pia mechi ya ufunguzi kati ya Brazil na Croatia, umekabiliwa na matatizo si haba ikiwemo migomo ya usafiri, usalama, na ghasia za hapa na pale. Fauka ya hayo, msisimko ni mkubwa kote duni POLISI WAPAMBANA NA WAANDAMANAJI BRAZIL Polisi katika mjini wa São Paulo nchini Brazil wametumia mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji wanaopinga Kombe la Dunia, ikiwa ni saa chache tu kabla ya michuano hiyo kuanza. Taarifa zinasema mtu mmoja amekamatwa na mwandishi mmoja wa CNN kujeruhiwa. Waandamanaji wanasema wamepanga kuandamana karibu na uwanja ambao shughuli ya ufunguzi itafanyika. Maandamano zaidi yamepangwa katika miji mingine ya Brazil kupinga michuano hiyo kuandaliwa nchini humo. Picha za TV kutoka São Paulo zinaonesha polisi wa kutuliza ghasia wakitumia mabomu ya machozi na risasi za mpira karibu na uwanja wa Corinthians. Waandamanaji hao wamekuwa wakiimba- wakisema "hakutakuwa na kombe hapa". Lakini pamoja na hayo kipyenga cha referree lazima kipulizwe kabla ya kuruhusu nyasi kuumia wakati miamba miwili ikionyeshana kazi mwamba mmoja toka kusini mwa Amerika na mwingine toka mashariki mwa Ulaya Mwamuzi wa mwaka wa Zamani wa Afrika Kusini, Daniel Bennett,ndoto zake za kushiriki fainali za Fifa za kombe la dunia 2014 zimevurugwa baada ya kutolewa nje kushiriki mashindano hayo kwa sababu ya kuumia kifundo cha mguu. Bennett alipendekezwa kuondolewa kama mwamuzi msaidizi baada ya Jopo la waamuzi soka ulimwengu kukubaliana kumuondoa katika mashindano hayo yatakayoanza nchini Brazil Leo tarehe 12/06/2012 saa tano kamili usiku kwa muda wa Afrika Mashariki Kocha wa Uruguay Oscar Tabarez hajui ni wakani gani mshambuliaji Luis Suarez, atakuwa vizuri na kuwa tayari kurudi kufanya kazi baada ya goti lake kufanyiwa upasuaji, aliyasema siku ya Jumanne. Tabarez alisema " Amerudi vizuri sana na anaweza kuwa bora,anafanya kazi ya ziada nje mazoezi yake kimwili.," "hatuwezi kutajaa tarehe kamili, mimi sijui kama tutaweza kuwa naye kwa ajili ya mechi ya kwanza, ya pili, na ya tatu,Kama ingekuwa ni juu yangu, Suarez angecheza kesho." Tabarez aliwaambia waandishi wa habari baada ya mazoezi ya Uruguay Uruguay katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia katika kundi D watakipiga dhidi ya Costa Rica na kufuatiwa na mechi dhidi ya England na Italia. Suarez aliwaambia mashabiki wake katika Twitter kuwa amewasili katika kikosi nchini Brazil na anajisikia nafuu katika goti lake la kushoto yuko tayari kurudi kwa ajili ya kombe la dunia Kuelekea mechi ya Leo kati ya wenyeji Brazil vs Croatia. Wachezaji nyota wanaotegewa Brazil-Neymar jnr,willian, Oscar,paulinho,T.Silva Croatia Rakitic,Modric,Olivia Folic na Jelavic. Mario Mandizukic hatocheza Leo kutokana na kadi nyekundu anayotumikia Source;Grant Mwaijengo

Mamlaka ya Chakula na Dawa kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya za kyela na Rungwe wamefanikiwa kukamata na kuteketeza shehena kubwa ya pombe haramu aina ya viroba, vipodozi, dawa na vyakula ambavyo muda wake wa matumizi umepita, bidhaa ambazo zimekamatwa wakati wa operesheni ya kutokomeza uingizwaji wa pombe haramu za viroba mkoani mbeya.
Shehena ya pombe haramu za viroba, vipodozi, vyakula na dawa ambazo muda wake wa matumizi umekwisha vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 vimeteketezwa kwa nyakati tofauti katika wilaya za Kyela na Rungwe , zoezi ambalo limesimamiwa na kamati za ulinzi na usalama za wilaya hizo.
Mkuu wa idara ya usafi na mazingira wilayani rungwe Dk. Nimroud kipoza na afisa wa mamlaka ya mapato TRA wilayani kyela Paul Walalaze wanaelezea madhara ya bishaa hizo kiafya na kiuchumi kwa watanzania.
Baadhi ya vijana ambao wameunda kikundi cha kupambana na pombe haramu za viroba pamoja na dawa za kulevya katika mpaka wa kasumulu wilayani kyela wamesema mafanikio yao katika kudhibiti bidhaa hizo yanatokana na kupata ushirikiano mzuri kutoka serikalini.
Meneja wa mamlaka ya udhibiti wa chakula na dawa (TFDA) kanda ya nyanda za juu kusini, Rodney Alananga amesema zoezi la kupambana na bidhaa hizo ni endelevu, hivyo akawataka wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha ili kuepuka kupata hasara

Jumatano, 11 Juni 2014


Binti aliyepata mateso kwa kung’atwa na kuchomwa kwa pasi na mwajili wake, Yusta Lucas (Kushoto) akiwa na mama yake, Modesta Simoni katika hospitali ya Mwananyamala juzi Dar es Salaam.
Hatimaye Yusta Lucas (20), binti anayedaiwa kuteswa kwa kung’atwa na mwajiri wake, Amina Maige ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Mwananyamala alikokuwa amelazwa na kukabidhiwa kwa wanaharakati wa Taasisi ya Jipange. Hatua hiyo ilifikiwa baada ya maridhiano kati ya Ustawi wa Jamii, mama mzazi wa Yusta, Modesta Simon, Kamati ya Ulinzi na Usalama Kata ya Makumbusho na Jipange ambao ndiyo iliyofanikisha kumwokoa binti huyo. Akizungumza jana, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makumbusho, Husna Nondo alisema baada ya kutafakari kwa kina juu ya usalama na urahisi wa kupatikana pale atakapohitajika, wamekubaliana binti huyo akae kwa muda kwa mmoja wa wanakikundi kutoka taasisi hiyo. “Tumeafikiana Yusta aendelee kubaki mikononi mwa wanaharakati ili iwe rahisi kupatikana atakapohitajika mahakamani, maana yeye ndiye shahidi wa kwanza. Mama na mjomba wake waliotoka Tabora wataendelea kukaa Upanga walikofikia,” alisema Nondo. Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Mwananyamala, Rose Temu alisema wamemkabidhi Yusta kwa Jipange kwa maandishi na wanaamini yuko katika mikono salama kwa sababu taasisi hiyo ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele kumuokoa. “Wakati akisubiri kesi yake, tumekubaliana awe chini ya Jipange tumeona asiendelee kukaa wodini kwan anaweza kupata ugonjwa mwingine, uamuzi ambao hata mama yake ameuridhia.”
Mwenyekiti wa Jipange, Janet Mawinza alisema wamekubali kumpokea Yusta kwa ajili ya usalama wake lakini akasema hataeleza ni wapi atakuwa anaishi kwa kipindi atakachokuwa akisubiri kesi. “Sisi tumempokea kama kikundi na tunachoomba ni vyombo vinavyohusika na suala hili kuhakikisha vinashughulikia suala lake kwa wakati ili huyu binti aungane na familia yake Tabora,” alisema. Mama wa binti huyo alisema anaamini binti yake yuko katika mikono salama. “Hawa Jipange ndiyo walikuwa naye tangu siku ya kwanza na sioni kama kuna tatizo wao kuendelea kuwa naye.” TUJIKUMBUSHE
Kwa siku tano, Yusta alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala kuuguza majeraha yanayodaiwa kusababishwa na kung’atwa na kuchomwa na pasi na Maige ambaye alikuwa mwajiri wake huko Mwananyamala Kwa Manjunju kwa muda wa miaka mitatu. Mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi katika Kituo cha Oysterbay na wakati wowote atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
Yusta alikumbwa na masaibu hayo kwa muda mrefu hadi hivi karibuni majirani wakiwa na polisi walipovamia nyumba hiyo na kumkamata bosi wake kisha kumpeleka Kituo cha Polisi cha Oysteraby, Dar ambako anashikiliwa na yeye kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibu baada ya kukutwa na majeraha. Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Camillius Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa ametiwa mbaroni.
Yusta alielezea mwenendo wa mwajiri wake ambao sio wa kawaida KUHUSU MAISHA YA TAJIRI WAKE Aidha, Yusta alianika mienendo mitano ya bosi wake huyo na kusema imekuwa ikimshangaza sana.
MWENENDO WA KWANZA “Mimi katika kuishi kwangu pale sijawahi kumwona jirani yeyote amekuja ndani kusalimia wala yeye kwenda kwa jirani kufanya hivyo jambo ambalo si la kawaida.”
MWENENDO WA PILI “Yeye (bosi wake) hana mume. Lakini tangu nimeishi pale kwa miaka mitatu sijawahi kumwona mwanaume ameingia ndani ya nyumba achilia mbali wanawake wenzake, hata mgeni. Kifupi yeye ni yeye kwa pale nyumbani kama ana marafiki labda wanakutana mbali.”
MWENENDO WA TATU
“Muda wake wa kurudi nyumbani siku zote ni usiku mnene, amewahi sana ni saa mbili usiku. Kwa hiyo, muda mwingi mimi ndiyo huwa nyumbani.”
MWENENDO WA NNE
“Anajiweza, sijui kwa nini aliamua kunifanyia hivi. Maana mtu ana gari, anaendesha mwenyewe na anasema ana hela, ndiyo maana namshangaa kuniadhibu kwa kuning’ata kwa meno.”
MWENENDO WA TANO
“Sikumbuki lini nimewahi kumwona akicheka. Muda mwingi anaonekana amekasirika tu kiasi kwamba nimekuwa nikimwogopa siku zote.”
OMBI KWA SERIKALI
Yusta alisema kufuatia matatizo makubwa yaliyompata ameiomba serikali imsaidie aweze kurudi nyumbani kwao Tabora.
SHUKURANI KWA MAJIRANI
Yusta alitoa shukurani kwa majirani waliojitokeza kuokoa maisha yake ambapo alisema kama wasingekuwa wao hajui ingekuwaje.
MANENO YA MUUGUZI
Kwa upande wa hospitali hiyo, muuguzi kiongozi wa zamu siku hiyo, Mahija Swalehe alikemea tabia za waajiri wa wafanyakazi wa ndani kuwatesa na kuiomba serikali kuliangalia suala hilo kwa jicho la tatu ili kukomesha vitendo hivyo

Alhamisi, 5 Juni 2014

Mbeya CIty FC yaingia Mkataba wa Udhamini na Kampuni ya Binslum Tyres CO. Ltd.. Mkataba huo ni wa Miaka Miwili wenye Thamani ya Tsh. Milioni 360.!! Mkataba umeanza Rasmi sasa., Kiasi hicho kitatolewa kila Mwezi kulingana na Makubaliano waliojiwekea Chukua muda wako Tazama Picha zifuatazo kuhusu kile kilichojiri kwenye Kutia saini Mkataba wa Miaka Miwili kati ya Mbeya City FC na Kampuni ya Binslum Tyres CO. LTD Muda Mfupi uliopita kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya... Mkataba huo umesainiwa na Mwanasheria wa Jiji la Mbeya Adv. James Bernod Kyando na Mkurugenzi wa Binslum Ndg Mohamed Ahmed Binslum.!!

Wakionesha mkataba kwa Waandishi wa Habari

Pichambili hapo juu ni Muonekano mpya wa jezio za Mbeya City Fc

Picha mbili hapo juu ni Mkurugenzi wa Binslum pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri ya jiji la mbeya wakisaini mkataba huo.
WIMBI la wanawake mkoani Mbeya kujifungua watoto na kisha kuwatupa na wengine kutoa mimba limezidi kushika kasi na kukithiri baada ya vitendo hivyo kuripotiwa na vichanga kuokotwa kwenye mashimo na mitoni. Kukithiri kwa vitendo ni baada ya leo Wananchi wa Mtaa wa Mwambenja kata ya Iganzo jijini Mbeya kugundua kutupwa kwa mtoto anayesemekana kuwa na umri usiozidi siku moja jinsia ya kike katika shimo la choo kisichotumika.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Mtaa huo, aliyefahamika kwa jina la Lukasi Mwakalonge, alisema alipewa taarifa na wananchi wake mchana na kuambiwa kuna katoto kametupwa shimoni na bado ni kazima hali iliyomlazimu kutoa taarifa katika Jeshi la Polisi. Alisema baada ya kufika eneo la tukio na kugundua kuwa mtoto bado yuko hai wakaamua kumtoa ndani ya shimo huku wakisubiri jeshi la polisi kwa ajili ya hatua zaidi lakini akawa amepoteza maisha muda mfupi baada ya kutolewa ndani ya shimo. Hata hivyo jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu, vitendo hivyo vya wanawake kutupa watoto kabla na baada ya kujifungia bado vinazidi kutokea hapa nchini ingawa hakuna takwimu sahihi za wanawake waliopatikana na hatia kwa makosa kama hayo.

Jumatano, 4 Juni 2014

MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi aliye vaa koti Jeupe
Mtoto wa MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi Elizabeth Mwasumbi akilia kwa furaha mara baada ya baba yake kuachiwa huru Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, imebatilisha hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela na viboko 12 aliyokuwa akiitumikia Mchungaji wa Kanisa la EAGT la Iwambi Jijini Mbeya, Daniel Mwasumbi(57) aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya ubakaji na kumpa mimba mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Itende Neema Beni(19) jijini hapa. Mchungaji Mwasumbi alihukumiwa kifungo hicho, Januari 2 mwaka huu na mahakama ya Wilaya ya Mbeya na Hakimu Gilbert Ndeuruo na Serikali kuwakilishwa na wakili Achiles Mulisa, ambapo Mahakama ilimtia hatiani Mchungaji katika makosa kinyume cha sheria kifungu cha 130(2)e na 131(1) sura ya 16 ya sheria iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Awali Mchungaji Mwasumbi alikuwa akitetewa na Wakili wa kujitegemea Victor Mkumbe ambapo ilidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari 2008 hadi 2011 ambapo alimpa ujauzito na kumzalisha mwanafunzi huyo watoto wawili wa kiume kwa nyakati tofauti hivyo kumkatisha masomo kinyume cha sheria. Katika Rufaa hiyo Mchungaji Mwasumbi alikuwa akitetewa na Wakili wakujitegemea Benjamin Mwakagamba kutoka Dar es Salaam wakati Serikali iliwakilishwa na Wakili Prosister Paul. Akisoma hukumu ya rufaa hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Atuganile Ngwala, alisema kuwa sababu zilizowasilishwa kwenye mahakama hiyo na Wakili wa upande wa utetezi zilidhihirisha kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa kisheria kwenye hukumu hiyo. Jaji Ngwala ambaye alitumia takribani saa 1:15 kusoma huku hiyo alisema katika utoaji wa hukumu hiyo haukuzingatia vipengele muhimu vya kisheria viilivyotumika na mahakama ya wilaya kumtia hatiani Mchungaji Mwasumbi. “katika rufaa hii ni kweli kuna mambo mengi ambayo yanaonekana kukiukwa katika utoaji wa hukumu, kama zilizovyoweza kuanishwa na wakili wa utetezi hivyo na mimi nakubaliana na wakili Mwakagamba (wakili wa utetezi) kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa kisheria kwenye hukumu hiyo” alisema Aliongeza kwamba kama ilivyoelezwa na wakili Mwakagamba, muda wa lilitopotekea tukio hilo na liliporitiwa kwenye vyombo vya usalama unaonekana kuchelewa na kukinzana, lakini pia ushahidi ulitolewa mahakamani hapo na Mhanga ulionekana kujichanganya hivyo haujaonesha mrufani kutenda kosa hilo’. Awali Jaji Ngwala alimwita mchungaji Mwasumbi kuwa ni mende, na ni mtu hatari sana katika jamii kwa kosa kama hilo na hafai kuwa katika jamii jambo lililowafanya watu waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa hukumu hiyo kuanza kuinamisha vichwa chini akiwemo Katibu wa Kanisa la Uinjisti Bwana Mwakasole. Lakini baadaye, Jaji Ngwala alionesha hisia zake kwamba kutokana na kujichanganya kwa ushihidi hususani wa shahidi namba moja ambaye ni binti aliyefanyiwa kitendo hicho hivyo kumtoa hivyo na haonekani kama ana kosa. Alisema ‘Nasema hivi mtu huyu alikuwa ni mende na ni hatari sana katika jamii asiyefaa kwa namna yoyote ile na anastahili adhabu kali laiti kama ingethibitika hivyo, lakini hapa ushahidi umeshindwa kuthibitisha hili hivyo ana haki ya kuachiwa huru’. Hata hivyo, Jaji Ngwala alisema kuwa kwa upande wa Jamhuri ambao ulikuwa ukiongozwa na wakili wa Serikali, Prosister Paul una haki zote za kukata rufaa na kesi kuanza upya endapo utaona haujaridhika na hukumu hiyo. Wakili aliyekuwa akimtetea Mchungaji Mwasumbi alisema kuwa katika rufaa ya mteja wake aliwasilisha sababu saba za kupinga hukumu hiyo ambapo alidai kuwa hakimu wakati wa kutoa hukumu hiyo alikosea kisheria na haki muda wa kuripotiwa kwa shauri hilo kwa vyombo vya usalama na lilipotokea ulikinzana na kwamba aliegemea kwa ushahidi wa Mhanga tu. Sababu zingine alidai kuwa hakimu aliegemea katika ushahidi au vidhibiti ambavyo awali alivikata mwenyewe, pia alidai kuwa hakimu hakuangalia uhalisia kosa lenyewe na badala yake alionekana kutoa maoni yake binafsi. Lakini sababu nyingine wakili Mwakagamba alisema kuwa hakimu huyo, aliegemea ushahidi ambao ulijichanganya, wendesha mashtaka walishindwa kuwapeleka mahakamani hapo mashahidi wa msingi katika kesi hiyo, hakimu aliegemea upande wa vyeti vya watoto wawil waliodaiwa ni wa Mchungaji Mwasumbi ambapo vyeti vilidurufiwa (photocopy) na si vyeti halisi na mwisho hakimu huyo alitoa hukumu ambayo haikufuata mtiririko uliosahihi wa mashahidi husika. Akizungumza na Mbeyayetu blog, mtoto wa Mchungaji Mwasumbi, Elizabeth Mwasumbi alisema anamshukuru Mola kwa kumwezesha Jaji Ngwala kwa kutenda haki katika rufaa ya baba yake. Alisema; ’Mimi na wenzangu tulikuwa na wakati mgumu sana pindi baba yetu akiwa ndani, kwani mimi niliathirika sana kiafya na kiuchumi nilishindwa kufanya shughuli yoyote kutokana na mawazo lakini namshukumuru Mola kwa kutenda haki’. Hata hivyo nje ya Mahakama ndugu na jamaa waliofurika kusikiliza hatma ya Rufaa hiyo waliokuwa na hamu ya kumlaki kwa furaha Mchungaji Mwasimbi ambaye pia ni mwimbaji wa nyimbo za Injili kushindwa kutokana na Maafisa wa Magereza kumpeleka Gerza la Ruanda kukamilisha taratibu za Magereza
Mama wa watoto mapacha Eliud na Elikana, Grace Joel akiwa amempakata mtoto Eliud ambaye kwa sasa anasumbulia na tatizo la kutokwa na utumbo.
Picha na Godfrey Kahango: Mwananchi
Mmoja wa watoto pacha waliozaliwa wakiwa wameungana na kutenganishwa kwa upasuaji nchini India, hali yake ni mbaya na utumbo wake mkubwa sasa umetoka nje. Mtoto huyo Eliud Mwakyusa na mwenzake Elikana walizaliwa Februari 20, 2013, Kyela, Mbeya wakiwa wameungana kiunoni na Serikali iliwapeleka India ambako walitenganishwa. Walirejea Februari, mwaka huu na kusherehekea siku yao ya kuzaliwa wakiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili walikofikia baada ya kutoka India katika hafla iliyoandaliwa na gazeti hili. Hata hivyo, siku chache baada ya watoto hao kurejea kijijini kwao Kasumulu maarufu kwa jina la Juakali, Kyela, afya ya Eliud ilianza kubadilika baada ya sehemu kubwa ya utumbo wake mpana kuanza kutokeza nje. Utumbo wa mtoto huyo umetoka nje kupitia tundu lililoachwa na madaktari jirani na kitovu chake kwa ajili ya kutolea haja kubwa. Wakizungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki nyumbani kwao, wazazi wa watoto hao, Grace Joel na Eric Mwakyusa walisema tatizo la Eliud lilianza mwezi mmoja uliopita. Grace alisema hali hiyo imesababisha mwanaye aanze kudhoofika naye akiwa hajui cha kufanya kutokana na hospitali iliyowafanyia upasuaji kuwa mbali. Alisema baada ya kutenganishwa walitengenezewa mirija maalumu ya kutolea haja. “...Waliingiza kwa ndani na kubakiza kidogo nje ya tumbo kwa ajili ya kutolea haja kubwa. Hivyo baada ya kuanza kuugua akawa anatapika na anapotapika utumbo huu ukawa unatoka nje kidogokidogo kama unavyoona,” alisema huku akionyesha utumbo huo. Alisema kuwa hali hiyo ya utumbo kutoka nje iliwahi kumtokea mtoto huyo hata wakiwa bado hospitalini nchini India, lakini haikuleta madhara yoyote. Mama huyo alisema afya ya Eliud imekuwa ikidhoofu kila kukicha na sasa imefikia hatua anashindwa kukaa peke yake tofauti na aliporejea kutoka India. Mwenzake aendelea vizuri Afya ya pacha mwenzake, Elikana ni nzuri na muda mwingi amekuwa akikaa na bibi yake mzaa baba, Subira Kasekele. Akizungumzia afya za wajukuu zake Kasekele alisema: “Watoto walinenepa kweli kipindi fulani na wakawa na afya njema, tatizo lipo tu kwa huyu mwingine (Eliud) kwani lilipoanza kujitokeza tatizo hili na afya yake ikaanza kutetereka.” Alisema huwa anashinda na mtoto huyo na kumrudisha kwa mama yake wakati wa kunyonya. Chakula wanachokula watoto Grace alisema licha ya kupewa masharti ya chakula kwa ajili ya watoto hao, hali ya maisha imewafanya wakiuke masharti kwani sasa wanakula chochote kinachopatikana. Baba wa watoto hao, Eric Mwakyusa anasema watoto wake wanaishi kwa kudura za Mwenyezi Mungu kwani wanakula chakula cha kawaida kutokana kipato chake duni. “Tulishauriwa watoto wale vyakula mchanganyiko ili kuwajengea afya njema, lakini uchumi wangu mbaya sina kitu hivyo wanalazimika kula kile tunachokipata kwa siku hiyo,” alisema. Alisema hivi sasa anaendesha pikipiki ya mtu ambayo anaitumia kwa kusafirisha abiria kwa sharti la kupeleka hesabu ya Sh8,000 kwa siku. “Unaweza kuona wakati mwingine ninapata Sh10,000 wakati mwingine 15,000 na siku nyingine biashara hakuna na hapohapo natakiwa kupeleka kwa bosi Sh8,000 ambayo natakiwa kuigawa nyumbani kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine. “Wakati mwingine siwezi kufanya kazi, nahitajika kumpeleka mtoto hospitali au kumwangalia wakati mama yao anafanya kazi nyingine... Bibi yao ana mtoto mwingine, basi yote tumeyapokea kwa kuwa Mungu ndiye mpaji,” anasema Mwakyusa. Wazazi washukuru Wakizungumza kwa hisia, Grace na Eric waliishukuru Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ambayo kupitia magazeti yake, Mwananchi na The Citizen yaliandikwa hali ya watoto hao na kuwafanya watu mbalimbali kuwasaidia. “Kwa mfano, mwenye pikipiki ninayoendesha alisoma kwenye Gazeti la Mwananchi ndipo aliponiita na kunikabidhi niendeshe walau nipate fedha kidogo,’’ alisema Eric na kuongeza kuwa kuna msamaria mwema ambaye ameahidi kumpatia pikipiki ili fedha zote atakazokuwa akipata zisaidie kuendesha maisha ya familia hususan watoto wake, lakini bado hajatimiza na anaamini akiwa tayari atamwambia. Grace licha ya kuwashukuru watu mbalimbali wanaoendelea kuwajulia hali watoto wao lakini akadokeza kwamba familia yake inahofia kwamba huenda isipate nauli ya kwenda Dar es Salaam na hatimaye India kwa ajili ya matibabu ya pili. Safari hiyo imepangwa kufanyika Julai, mwaka huu.
Credit :MWANANCHI
br>

Jumatatu, 2 Juni 2014

Flora Mbasha akiwa na mumewe Emmanuel Mbasha. Flora Mbasha akiwa na mumewe Emmanuel Mbasha. Emmanuel Mbasha, ambaye ni mume wa mwimbaji nguli wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha amejitokeza hadharani na kusema kwamba atakwenda polisi mwenyewe kujibu tuhuma dhidi yake za kumbaka shemeji yake mwenye umri wa miaka 17. Faili la tuhuma dhidi ya Mbasha lilifunguliwa Jumatatu iliyopita katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule) wakati shemejiye huyo (jina tunalihifadhi), alipotaarifu kuwa Mbasha alimbaka mara tatu kwa siku mbili tofauti. Kesi hiyo ilipewa namba TBT/RB/3191/2014 na TBT/IR/1865/2014. Tangu siku hiyo, polisi imekuwa ikieleza kuwa inamsaka Mbasha bila ya mafanikio lakini mwishoni mwa wiki mtuhumiwa huyo aliongea na gazeti hili na kuelezea upande wake wa tukio hilo na kwamba yuko tayari kujisalimisha ili ukweli ubainike. “Tuhuma dhidi yangu ni za kutengeneza,” alisema Mbasha na kufafanua kuwa yote hayo yanatokana na mgogoro wa kifamilia baina yake na Flora na familia yake ambao alisema umedumu kwa siku kadhaa. “Mimi sijabaka na sijawahi kubaka; sijatenda dhambi yoyote; sijafanya kitu chochote na kibaya haya mambo yote ni ya kusingiziwa tu. Mungu wangu ni shahidi. Na kwa kuwa sijafanya hiyo dhambi kama wanavyodai, basi Mungu wangu atanitetea,” alisema Mbasha ambaye anaonekana zaidi kwenye video ya wimbo wa Maisha ya Ndoa alioshirikiana na mkewe Flora. “Si wamesema wananitafuta, nitakwenda mwenyewe polisi. Nitawasikiliza na nitatoa maelezo yangu. Kama wakinipeleka mahakamani basi ukweli utajulikana… ipo siku kila kitu kitakuwa wazi.” Kabla ya kufunguliwa kwa faili la tuhuma hizo, msichana huyo alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Ilala (Amana) ambako alifunguliwa faili la matibabu namba 667. Matokeo ya vipimo ambavyo vilifanywa na daktari kung’amua kama binti huyo aliingiliwa vinaonyesha kuwa kulikuwa na mbegu utokaji wa mbegu usio wa kawaida (HVD). Kadhalika binti huyo alifanyiwa vipimo kuona kama ameambukizwa virusi vya Ukimwi (VVU), pia kupata ujauzito, lakini matokeo ya awali yalionyesha kuwa yupo salama. Akiwa nje ya kituo cha polisi Jumatatu usiku, binti huyo aliliambia gazeti hili kwamba mara ya kwanza alibakwa mchana Mei 23 na kwamba mtuhumiwa alirudia kitendo hicho Jumapili Mei 25 usiku ndani ya gari katika eneo la Tabata, ambako anadai alifanyiwa kitendo hicho mara mbili. Hata hivyo, Mbasha alihoji: “Hivi kweli hata kama mimi ni mbakaji, kweli nimbake mtoto wa kumlea mwenyewe mara tatu, yaani Ijumaa halafu nirudie tena Jumapili? Hata kama ni kusingiziwa basi tuhuma hizi zimezidi.” “Huyu binti nimekaa naye miaka mingi na sijawahi kumfanyia hivyo. Hapo nyumbani kwangu wamekaa mabinti wengi, wakiwamo shemeji zangu wadogo zake na Flora na sikuwahi hata kuwagusa, leo hii kwa nini wananifanyia hivi?” Mgogoro wa familia Mbasha alidai kwamba chanzo cha kusingiziwa kwake ni mgogoro baina yake na mkewe Flora, ambao umesababisha mgawanyiko mkubwa ambao umefanya achukiwe na familia nzima ya mkewe. “Yako mambo mengi tu ambayo yanahusu familia, kwa hiyo ilifika mahali mimi na Flora tukawa hatuishi kwa amani na hata hili jambo limetokea wakati tukiwa na mgogoro huo. Hivyo Flora na ndugu zake waliamua kumlisha binti huyo maneno ili mimi nifungwe,” alisema Mbasha. Hata hivyo, Flora hakutaka kuingia kwa undani katika suala hilo, akisisitiza kuwa Mbasha bado ni mumewe na kwamba yaliyotokea awali alishamsamehe, lakini akamtaka ajitokeze kutoa maelezo polisi. “Mimi nilishamwambia kwamba hata kama alifanya au hakufanya, nilishamsamehe kutoka ndani ya moyo wangu maana yeye ni mume wangu wa ndoa na Mungu wangu ni shahidi, lakini kuna suala la kisheria polisi ambalo mimi siwezi kuliingilia,” alisema Flora ambaye alitamba na wimbo wa injili wa “Tanzania” ambao ulimfanya aalikwe katika shughuli mbalimba za kitaifa. “Tatizo linakuwa kubwa kwa sababu yeye mwenyewe haonekani na taarifa ni kwamba amekimbia,” alidai Flora. “Sasa kama kweli hajafanya kitendo hicho, kwa nini anajificha? Ajitokeze… aende polisi na huko ndiko akatoe maelezo yake. Kuzungumza na vyombo vya habari haisaidii kabisa.” Mwimbaji huyo, ambaye ni mjukuuu wa muhibiri maarufu wa Injili, Askofu Moses Kulola alisema yeye hana uwezo wa kuingilia kesi hiyo kwani hakuhusika kwa namna yoyote ile kupeleka suala hilo polisi kwa sababu hakuwapo wakati likitokea na kwamba linasimamiwa na familia. “Inawezekana anatamani nikafute kesi polisi, mimi sina uwezo huo kwa sababu ni suala la kisheria na tuhuma zenyewe ni za kijinai. Pili familia yenye mtoto ndiyo inafuatilia kesi hiyo, lakini hilo halifuti msamaha wangu kwake,” alisisitiza. Kauli ya Flora kwamba ameshamsamehe mumewe inafanana na ya Mbasha ambaye pia alisema kwamba kama kuna jambo ambalo mkewe alimkosea, hana tatizo na kwamba alishamsamehe. “Flora ni mke wangu, mke wa ujana wangu, ninampenda asilimia 100 na yeye analifahamu hilo, lakini sijui ni kitu gani kimemkuta? Sijui ni nini kimeingilia ndoa yetu?” alisema Mbasha. Alisema ameshampigia simu mkewe mara nne akitaka waonane ili wazungumze, lakini hakuonyesha utayari, kauli ambayo Flora aliikanusha akisema: “Hajanitafuta maana tangu Jumatatu hapatikani kwenye simu.” Mwenendo wa upelelezi Wakati hayo yakiendelea, maendeleon ya kesi hiyo yanasuasua baada ya faili kutokupelekwa Kituo cha Polisi Buguruni kutoka Tabata kwa ajili ya hatua zaidi. Baadhi ya wanafamilia wa mtoto anayedaiwa kubakwa walisema jalada hilo lingefikishwa Buguruni Jumatano jioni, lakini kutokana na ofisa anayeshughulikia kesi hiyo kuwa na udhuru, ilishindikana. Mjomba wa Flora ambaye amepewa jukumu la kusimamia kesi hiyo, alisema wamekuwa wakifuatilia Kituo cha Polisi cha Tabata tangu tukio hilo liliporipotiwa, lakini wakaelezwa kuwa kesi hiyo itahamishiwa Buguruni. “Tuliambiwa lile faili lazima lihamie kituo cha Buguruni. Nilifika hapa nikaonana na kamanda wa polisi wa wilaya ambaye ametupokea vizuri na kuonyesha moyo wa kutusaidia,” alisema. Kamanda wa polisi wa Ilala, Marietha Minangi alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa kesi hiyo na kwamba hafahamu taarifa kuwa faili hilo linacheleweshwa kuhamishiwa Buguruni. “Tunaendelea kuchunguza, ila siyajui hayo masuala ya faili yanayotoka kinywani mwako. Lakini nimepata taarifa kuwa bado wanachunguza,” alisema Minangi. Mwanzoni mwa wiki jana, Kamanda Minangi alisema kuwa maofisa wake walikuwa wanaendelea kumsaka mtuhumiwa na kwamba walienda mpaka nyumbani kwake, lakini hawakumkuta. “Nimefuatilia ni kweli hiyo kesi imefunguliwa na maofisa wangu wameniambia walienda nyumbani kwake na hawakumkuta mtu. Waliniambia walikaa pale kwa takribani dakika 20 na ile nyumba ina fence (uzio) na geti waligonga kengele, lakini hakuna mtu aliyekuja kufungua. “Na baadaye waliwauliza majirani, nao wakasema hawafahamu mtu huyo alipo. Inaonekana ametoweka, lakini sisi kama wasimamizi wa sheria tunaendelea kumtafuta mpaka tutakapomkamata,” alisema Minangi. Ustawi wa Jamii Kesi hiyo pia inafuatiliwa kwa karibu na Idara ya Ustawi wa Jamii ya Manispaa ya Ilala kujua usalama na matibabu ya binti huyo. Ofisa ustawi wa jamii anayeshughulikia ulinzi na usalama kwa mtoto wa manispaa hiyo, Fransica Makoye alisema kuwa wanalishughulikia suala hilo kama mengine katika kutafuta haki na usalama wa mtoto na wala hawahusishi na umaarufu wa wahusika. “Sisi tunafuatilia kama alipata tiba sahihi mara baada ya tukio la kubakwa na kufahamu mahali ambako anakaa kwa ajili ya usalama wa huyo mtoto. Tumeiona PF3 haionyeshi kama alipata matibabu, lakini tutawajulisha zaidi kinachojiri kwa kuwa tutaenda Hospitali ya Amana kwa maelezo zaidi,” alisema Makoye