Jumanne, 3 Desemba 2013


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Engineer Felchesmi Mramba kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar Es Salaam jana, Jumatatu, Desemba 2, 2013, na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Florens Turuka inasema kuwa uteuzi huo umeanza  jana.

Kabla ya uteuzi wake, Eng. Mramba alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la TANESCO.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
2 Desemba, 2013
SIMULIZI za maajabu zipo nyingi na nyingine zinaendelea kuchukua nafasi, ila hii inaweza kuwa funga mwaka 2013.
Mtanzania Yahya Msemakweli, 34, (pichani) alifariki dunia, akawekwa chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari), ndani ya jokofu kwa siku tano na ndugu zake akiwemo mkewe, waliushuhudia mwili wake na kujiridhisha kuwa ni yeye.



Yahya akiwa ICU MOI.

Hata hivyo, siku ya sita ambayo ndiyo ilikuwa tarehe ya mazishi, walipoufuata mwili wa Yahya hawakuukuta mochwari, droo aliyowekwa, ilikutwa maiti ya kike, majokofu yote yakafunguliwa lakini hawakuuona.
Siku iliyofuata, yaani siku ya saba, Yahya akakutwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Alitokaje mochwari Temeke hadi Muhimbili wodini? Hakuna anayejua!

Nyongeza ni kwamba kaburi lilishachimbwa, sanda ilishanunuliwa tayari kwa mazishi ya Yahya lakini mambo yalipogeuka, ilibidi wazike mgomba kwa kile kilichoelezwa: “Kimila kaburi huwa halifukiwi tupu.”
Yahya Msemakweli.

MKE WA YAHYA ANASIMULIA
Mke wa Yahya, Mwanjaa Juma, alisema: “Mimi na mume wangu tunaishi Mtoni Madafu, Temeke. Mume wangu ni dereva wa bodaboda.”

Mwanjaa aliendelea kusimulia kuwa Novemba 22, mwaka huu, saa 5:15 usiku, alipigiwa simu na Yahya akamwambia yupo njiani anarudi nyumbani.
“Wakati huo aliniambia yupo Kilwa Mivinjeni. Mpaka saa 6:00 usiku alikuwa hajarudi, nikampigia simu ikawa haipatikani.
“Niliingiwa na wasiwasi sana, kulipopambazuka tu nilikwenda Mtoni Kwa Azizi Ally ambako ndiyo kituo chake cha kupaki bodaboda. Niliwauliza wenzake, wakanijibu kuwa tangu apeleke abiria jana yake saa 4 usiku, hakurudi tena,” alisema na kuongeza:


Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa Yahya.

“Nilirudi nyumbani na kuanza kuwapigia simu baadhi ya ndugu na jamaa lakini sikupata jibu la mahali mume wangu alipo. Baada ya siku mbili nilikwenda Kituo cha Polisi Mtongani, nikakuta pikipiki yake ikiwa imeharibika vibaya kutokana na ajali.
“Nilipowauliza polisi walisema mwenye pikipiki hawamjui na alipelekwa pale usiku wa siku mbili zilizopita na msamaria mwema akiwa hajitambui, ikabidi wamkimbize Hospitali ya Temeke kwa matibabu.

“Tulipofika Hospitali ya Temeke mapokezi jina lake halikuwepo katika kitabu cha orodha ya wagonjwa waliopokelewa, tulikwenda ICU nako hatukumuona.
“Kesho yake asubuhi, tulilazimika kwenda mochwari ya Hospitali ya Temeke, tukakuta mwili wake kwenye jokofu na kujiridhisha ni wenyewe. Wahudumu wakakiri kwamba ule mwili una siku tatu pale.

“Hatukuwa na cha kufanya zaidi ya kupanga taratibu za mazishi. Tuliwataarifu ndugu, tukapanga tarehe ya mazishi iwe Novemba 27, kaburi likachimbwa.
“Siku ya mazishi, watu walikwenda na gari kufuata mwili hospitali lakini hawakuukuta kwenye jokofu alilokuwa amehifadhiwa.
“Walipokwenda kuulizia kwa uongozi wa hospitali, wakasema kwanza waende kituo cha polisi wapate askari wa usalama barabarani, wakapime ajali ndipo watapewa mwili.

“Ikabidi waende Kituo cha Polisi Mtongani, wakaambiwa waende Kituo Kikuu cha Mkoa wa Polisi, Temeke, Chang’ombe, pale alipatikana askari wa usalama barabarani, wakaongozana hadi eneo la ajali na kupima na kuchora ajali ilivyokuwa.
“Baada ya mchoro, polisi walitoa kibali cha mazishi. Ndugu walikwenda na kibali kwa uongozi wa hospitali wakaomba wapewe mwili lakini danadana zikaendelea, maana haukuonekana mochwari.

“Wakiwa na sanda mkononi, waliuliza maiti ilipokwenda lakini hawakujibiwa, hakuna aliyekuwa na maelezo ya kueleweka.
“Ulifanyika msako pale mochwari lakini hakuna kilichopatikana.

“Ikabidi ndugu warudi Kituo cha Polisi Mtongani, wakapewa askari hadi Hospitali ya Temeke. Yule askari alipouliza ndiyo wahudumu pale hospitali wakasema kuna mgonjwa mahututi alihamishiwa Muhimbili pale Moi (Kitengo cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu).
“Kweli walikwenda Moi, walimkuta mume wangu akiwa ICU anaendelea na matibabu.”

NINI KILIFANYIKA
Mwanjaa alisema, baada ya kumkuta Yahya yupo ICU, hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kurudi nyumbani na kuwataarifu kila kitu ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya mazishi.
“Hakuna aliyeamini haraka, wengine walikwenda mpaka Moi kuhakikisha, waliobaki waliamua kuzika mgomba kwa sababu kimila kaburi halifukiwi bila kitu.

“Japo tulitumia fedha nyingi kwa ajili ya maandalizi ya mazishi, tuliandaa chakula kingi lakini kimedoda, ila yote kwa yote namshukuru Mungu mume wangu bado mzima.
“Namuomba Mungu amponye mume wangu haraka, arudi nyumbani tuendelee na maisha yetu. Hivi sasa kila mara nipo Moi kwa ajili kuhakikisha anapata huduma kwa ukaribu na anapona haraka,” alisema Mwanjaa.

DADA MTU AZIMIA MARA SABA
Zafarani Msemakweli ambaye ni dada wa Yahya, alizimia mara sita mara ya kwanza alipopewa taarifa ya msiba.
Habari ambazo zimethibitishwa na Zafarani mwenyewe, zinasema kuwa baada ya kupewa taarifa kaka yake yupo hai ICU Moi, alizimia tena, hivyo kufikisha mara saba.

Zafarani alisema: “Nilipopokea taarifa kwamba kaka yangu amekufa niliishiwa nguvu, unajua yule ni tegemeo la familia yetu. Ndugu zangu wanasema nilizimia mara sita.
“Nilipoambiwa ni mzima kwa mshtuko nilizimia tena. Ni maajabu, mtu amehifadhiwa mochwari na madaktari wamethibitisha amekufa baadaye tunaambiwa yupo hai, inashangaza sana.”

UWAZI LAMSHUHUDIA YAHYA ICU
Mwandishi wetu alikwenda Moi kumwangalia Yahya na kujiridhisha kweli yupo hai anaendelea na matibabu.
Jitihada zinaendelea za kumtafuta mganga mkuu wa Hospitali ya Temeke, aseme nini kilitokea kwenye hospitali yake mpaka Yahya akawekwa mochwari na kuwekwa ndani ya jokofu kwa siku tano kisha kupelekwa Moi akiwa mgonjwa mahututi.

Awali mwandishi wetu alikwenda hospitalini hapo na kuomba kuzungumza na mganga mkuu lakini alikosa fursa na kila akipiga simu yake haipatikani.
 Chanzo;       UWAZI

Jumatatu, 2 Desemba 2013

KWA UFUPI
  • Malawi na Tanzania zimewasilisha ushahidi na majibu ya maswali kuhusu umiliki wa maeneo kwenye Ziwa Nyasa, kwa jopo la wasuluhishi linaloongozwa na Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano
 Malawi na Tanzania zimewasilisha ushahidi na majibu ya maswali kuhusu umiliki wa maeneo kwenye Ziwa Nyasa, kwa jopo la wasuluhishi linaloongozwa na Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano.
Wasuluhishi hao walizitaka Malawi na Tanzania kutoa majibu ya maswali manne muhimu, wakati wakiwasilisha ushahidi wao kuhusu umiliki wa ziwa hilo wenye mgogoro.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na Tanzania kutoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni, kutafuta mafuta katika eneo la ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la Malawi la  Nyasa Times, msemaji wa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Malawi, Quent Kalichero alithibitisha Jumatano wiki hii kwamba nchi hiyo imewasilisha majibu ya maswali hayo na ushahidi uliohitajika.
“Waziri wetu amewasilisha taarifa maalumu ya maandishi kwa wasuluhishi na kwa sasa yuko nchini Msumbiji, kwa ajili ya suala hilo,” alisema Kalichero juzi.
Makabidhiano hayo yalifanyika mjini Maputo, Msumbiji ikiwa ni siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mazungumzo na wasuluhishi, marais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano na wa Botswana, Festus Mogae jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mkutano huo wa Jumatatu mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe aliwaeleza wanahabari kwamba mazungumzo baina ya Rais Kikwete na wasuluhishi hao yalihusu zaidi ushahidi wa Tanzania katika suala la umiliki wa Ziwa Nyasa.
Pia alithibitisha kwamba Tanzania ilikuwa tayari  kuwasilisha ushahidi wake kwa sekretarieti ya ofisi ya waliokuwa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) inayoongozwa na Chissano, Jumatano iliyopita.
Baada ya mkutano huo wa Jumatatu, Membe alieleza kwamba nchi zote husika, yaani Tanzania na Malawi zinatakiwa kuheshimu maagizo na kuwasilisha ushahidi huo kwa wakati, na kuwaachia wasuluhishi kazi ya kupitia na kutekeleza wajibu wao wakiwa wamepewa muda unaofikia mwaka mmoja kupata suluhu.
Wasuluhishi hao wa Sadc, Chissano na Mogae waliwasili jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mgogoro huo, kama walivyofanya kwa Malawi Julai mwaka huu.
Julai mwaka huu, Rais Joyce Banda wa Malawi alinukuliwa akisema kuwa nchi yake haina nia ya kulegeza kamba katika mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na Tanzania.
 Alitoa msimamo huo baada ya kukutana na Chissano wa Msumbiji na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambao ni wajumbe maalumu wa Jumuiya ya Sadc katika mgogoro huo
Alisema kwamba madai ya Tanzania kuwa inamiliki sehemu ya Ziwa Nyasa, siyo ya kweli na kwamba mpaka uko ufukweni mwa ziwa hilo upande wa Tanzania.
Rais Banda alidai kuwa nchi yake inafuatilia kwa karibu upatanishi wa SADC na kwamba isiporidhishwa na uamuzi ya jumuiya hiyo italiwasilisha suala hilo Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).
Kabla ya hatua hiyo ya Malawi,  Aprili mwaka huu Serikali ya Tanzania iliitaka nchi hiyo kuacha kutapatapa na kuonya kuwa kamwe isithubutu kugusa eneo hilo la mpaka.
Akitoa kauli ya Serikali ya Tanzania Membe alisema: “Nadhani watasikia na kuelewa, Serikali ya Malawi iache kutapatapa, nchi zote ilikoenda kulalamika kuhusu mgogoro huu, Tanzania tumekuwa tukielezwa na hata hao wanaotueleza wanaishangaa sana Malawi.” Kauli hiyo ya Serikali ilifuatia Rais Banda kusema kuwa mgogoro huo sasa utapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kwa madai kwamba juhudi za usuluhishi wa kidiplomasia zimeshindikana.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Malawi ni kinyume na makubaliano baina ya nchi hizo mbili yaliyofanyika Novemba 7 mwaka jana, jijini Dar es Salaam ambapo zilikubaliana kwamba jopo hilo ndiyo sehemu ya mwisho ya makubaliano.
Katika maelezo yake, Rais Banda alisema nchi yake imejitoa katika mazungumzo ya usuluhishi kwa madai ya kuhujumiwa na katibu wa jopo hilo ambaye ni Mtanzania, John Tesha kwa maelezo kuwa anavujisha taarifa muhimu za Malawi kwa Tanzania kabla ya Tanzania haijawasilisha taarifa zake kwa jopo hilo. Alisema kuwa tangu kuibuka kwa mgogoro huo, Malawi imekwenda kulalamika katika nchi za Uingereza, Marekani, Umoja wa Afrika (AU) na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).
Hata hivyo, baadaye Julai mwaka huu, Serikali ya Malawi ilitangaza kuwa itaendelea na mazungumzo na Tanzania kuhusu mpaka huku ikieleza kuwa viongozi wa Tanzania hawaelewi mipaka ndiyo maana wanapigania kuwa wao ni sehemu ya ziwa.
Waziri wa Habari wa Malawi, Moses Kunkuyu aliliambia Shirika la Utangazaji la Malawi (MBC) kuwa viongozi wote wa Tanzania wanadhani wanamiliki Ziwa Malawi (Nyasa) lakini watakuja kubaini baadaye kuwa hawana hata tone la umiliki.
.