Jumapili, 2 Februari 2014


Wachezaji wa Young Africans wakiwa mazoezini nchini Uturuki
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Young Africans kesho siku ya jumapili itashuka dimbani kuivaa timu ya Mbeya City FC kutoka jijini Mbeya katika muendelezo wa michezo ya mzunguko wa pili, mechi itakaofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Young Africans ambayo kwa sasa inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa VPL ikiwa na pointi 32, pointi moja nyuma ya vinara wanaongoza timu ya Azam FC huku Mbeya City wakiwa nafasi ya tatu na pointi 31.
Kikosi cha Young Africans kimeendelea na mazoezi yake leo asubuhi mjini Bagamoyo kujiandaa na mchezo huo wa kesho ambao ni muhimu kwa vijana wa Jangwani kupata pointi 3 na kuweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kurejea kileleni.
Kocha mkuu Hans Van der Pluijm amesema wameendelea kufanyia marekebisho kwa makosa yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya timu ya Coastal Union na kusema anaamini vijana wake watafanya vizuri katika mchezo wa kesho.
Kuna mapungufu yalijitokeza katika mchezo uliopita mjini Tanga dhidi ya Coastal, tulipata nafasi kadhaa za kufunga tukashindwa kuzitumia pia umakini haukuwa mzuri sana, tumeendelea kufanyia marekebisho mapungufu hayo ili tuweze kufanya vizuri.
Katika mchezo wa awali uliofanyika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya mwezi Septemba mwaka jana, timu hizi zilitoka sare ya mabao 1-1 huku bao la Young Africans likifungwa na Didier Kavumbagu.

0 comments :

Chapisha Maoni