Jumanne, 5 Novemba 2013


SERIKALI imetangaza kurudisha daraja ziro katika elimu ya sekondari, huku zikiwa zimepita siku tatu, tangu uamuzi wa kufuta daraja hilo utangazwe.

Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kelele nyingi za wadau mbalimbali wa elimu, wakipinga hatua ya kufuta ziro na badala yake lisomeke kama daraja la tano.

Uamuzi wa kurudisha ziro ulitangazwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, huku mtihani wa kidato cha nne ukiwa umeanza jana.
Tamko la Mulugo limepingana wazi wazi na tamko jingine lililotolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifueni Mchome akitangaza uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro.

Kutokana na mkanganyiko huo, Bunge limeitaka Serikali kuwasilisha kauli moja kuhusu mabadiliko ya alama za ufaulu kwa shule za sekondari, ili kuondoa utata huo.

Mulugo alitoa tamko hilo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM), ambaye alitaka kujua kama uamuzi huo wa Serikali ulilenga kuwasaidia wanafunzi wanaofeli.

Akijibu swali hilo, Mulugo alisema taarifa zilizoenea kuwa divisheni ziro imefutwa si za kweli.

“Serikali haijafuta divisheni ziro na wala hakuna divisheni V (daraja la tano), ipo divisheni I, II, III, IV na divisheni ziro kama kawaida,” alisema.

Alisema uamuzi wa kushusha madaraja uliofanywa haukuwa na lengo la kuwaokoa wanafunzi wanaofeli, bali ni kuondoa mrundikano wa alama katika daraja moja.

Alisema Serikali imeweka madaraja mapya kwa kutofautisha alama kumi kumi kutoka daraja moja kwenda jingine na kwamba hata hivyo alama za ufaulu bado ni 40 ambazo ni daraja la C.


Baada ya majibu hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliingilia kati na kuitaka Serikali kuwasilisha bungeni kauli moja inayoeleweka, ili kuondoa utata unaowachanganya wananchi.

“Hii taarifa unayosema Waziri ni tofauti kabisa na tamko la awali lililotolewa. Haiwezekani kuwe na taarifa mbili tofauti katika Serikali moja, nendeni mkakae mje na kauli moja inayoeleweka tusiwachanganye wananchi,” alisema Makinda.

Wakati Mulugo akitoa tamko hilo, zilikuwa zimepita saa tatu tangu kiongozi huyo anukuliwe katika vyombo vya habari akitetea uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro na kuanzisha daraja la tano.

Mulugo alifanya hivyo jana saa 1:40 asubuhi wakati akihojiwa katika kipindi cha kumepambazuka kinachorushwa na kituo cha Redio One, kinachoruka kila siku kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 4 asubuhi.

Katika kipindi hicho ambacho mada ilikuwa ni mfumo wa madaraja mapya, Mulugo aliutetea uamuzi wa Serikali wa kufuta ziro na kudai kuwa hatua ya kupunguza viwango vya ufaulu imefanyika ili kupambanua madaraja hayo.

“Elimu zaidi inahitajika kwenye suala hili la mgawanyo wa madaraja, ukweli ni kwamba kilichofanyika katika kufuta alama ya ziro ni kupambanua madaraja ya ufaulu, ni suala ambalo litasaidia elimu yetu huko mbele ya safari,” alisema Mulugo.

Awali akijibu swali la msingi la Magige, Mulugo alisema Serikali haina mpango wa kuanzisha programu maalumu hasa za ufundi kwa wanafunzi waliofeli katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.

“Kwa mwaka 2013, jumla ya wanafunzi 60,507 wa kujitegemea, wamejisajili kufanya mtihani huo, watahiniwa 3,578 wakiwemo wasichana 2,020 na wavulana 1,558 waliofeli katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamejisajili kurudia mtihani huo,” alisema.

Mulugo alisema Serikali imekuwa ikiongeza na kuboresha vyuo vya ufundi na kuweka mazingira rahisi kwa wanafunzi ili waweze kupata stadi mbalimbali.

“Kati ya mwaka 2010 hadi 2012, Serikali kupitia VETA imesajili jumla ya Vyuo vya Ufundi Stadi 75 sawa na asilimia 75 na asilimia 10.8 ya vyuo 618 vilivyokuwepo.

“Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya vyuo 8 sawa na asilimia 3.2 ya vyuo 248 vilivyokuwepo vilisajiliwa na NACTE,” alisema Mulugo.

Mabadiliko hayo yameibua mjadala mkubwa, ambapo wasomi na wadau mbalimbali waliyaponda mabadiliko hayo na kudai kuwa yanaua elimu nchini.

Kwa mujibu wa wadau hao, uamuzi wa kufuta ziro sekondari ulikuwa umefanywa kisiasa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kisiasa na si kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

Walisema uamuzi wa awali ulilenga kutimiza lengo la Mpango wa Maendeleo Makubwa Sasa (BRN), ambao ni kuongeza ufaulu kwa mtihani wa kidato cha nne mwaka huu kutoka asilimia 33 mwaka jana na kufikia asilimia 60

Jumatatu, 4 Novemba 2013


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa washitakiwa sita, baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia. Imetoa adhabu hiyo katika kikao chake kinachoendelea mkoani Shinyanga.

Adhabu hiyo ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Simon Lukelelwa katika kesi nne tofauti. Kesi hizo ni za mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake vikongwe, kutokana na imani potofu za kishirikina.

Mauaji hayo yalifanyika kati ya mwaka 2005 na 2007 katika Wilaya za Bukombe, Shinyanga na Kahama, ambako wanawake wanne waliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili.

Waliopewa adhabu hiyo ni Venance Nuba na Tegemeo Paulo, ambao walitiwa hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Sophia Gundu Januari 25,2006 katika Kijiji cha Kazibizyo Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita.

Wengine wawili waliokumbwa na adhabu ya kifo cha kunyongwa ni Joseph Lushika na Maziku Mpiga Chai baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa kukusudia Monica Bulemela Mei 5, 2005 katika Kijiji cha Lutembela Wilaya ya Bukombe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Simon Lukelelwa.




Mshitakiwa mwingine aliyekumbwa na adhabu ya kunyongwa ni Mhande Manyanya baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa kukusudia Wande Bulugu Julai Mosi, 2007 katika Kijiji cha Ihapa Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa.
 

Mshitakiwa wa sita aliyekumbwa na adhabu ya kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia ni Tembo Hussein, aliyetiwa hatiani kumuua kwa kukusudia Anjelina Hungwi katika kijiji cha Itega Wilaya ya Kahama

Jumapili, 3 Novemba 2013


kamanda wa polisi mkoani Mbeya Diwani Athumani akiongea na waandishi wa Habari kuhusu vurugu Tunduma 

Diwani wa kata ya Tunduma Ndugu Frank Mwaijoka (Chadema) pamoja na mchungaji wa kanisa la KKT katika eneo hilo la Tunduma wilayani momba Mkoani mbeya wametakiwa kujisalimisha kituo cha Polisi Tunduma mara baada ya kuhusika na uchochezi wa kidini hali ambayo imepelekea kutokea kwa vurugu  katika eneo hilo.

Vurugu hizo zimeanza majira ya saa 3:asubuhi katika eneo hilo la tunduma mara baada ya kundi la watu wanaodai kuwa wao ni wafuasi wa dini ya kikristo wakidai waruhusiwe kuchinja mifugo na kuuza katika mabucha yao hali iliyo pelekea kuibuka kwa vurugu hizo.

Akizungumza kuhusiana na tukio hilko Kamanda wa Polisi Mkoani humo Ndugu Diwani Athumani amesema kuwa kufuatia kuwepo kwa tukio hilo jumla ya watu zaidi ya 40 tayari wamekwisha kamatwa .

Amesema mpaka sasa taarifa walizo zipata kufuatia vurugu hizo zinaeleza kuwa miongoni mwa watu walichochea vurugu hizo ni diwani wa kata hiyo ya Tunduma Ndugu John mwaijoka pamoja na Mchungaji wa kanisa la kkt ndugu Neema Mwaipusa ambao kwa pamoja wametakiwa kujisalimisha kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.
Amesema suala hilo limegubikwa  na siasa kwani tayari viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa mkoa huo Ndugu Abbas Kandoro amekwisha litolea ufafanuzi Apri 02 mwaka huu wakiwepo pia viongozi wa dini .
Amesema kwa asilimia kubwa mgogoro huo juu ya nani achinje umeingiliwa na mambo ya kisiasa kwani hata baadhi ya wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakilalamika juu ya kutokea kwa vurugu hizo.

Amesema shughuli za kibiashara katika eneo hilo zimeshindwa kufanyika katika eneo hilo hivyo kufanya wananchi kupata adha hasa kwa nchi jirani ya Zambia ambao kwa asilimia kubwa wanategema kupata mahitaji kutoka mpakani mwa Tanzania.

Hata hivyo Diwani amesema kuwa katika vurugu hizo askari mmoja  pamoja na mwananchi wamejeruhiwa kwa kupigwa mawe ambapo tayari wamekwisha fikishwa kituo cha polisi.

Kufuati hali hiyo Kamanda huyo wa Polisi amesema kwa sasa hali imelejea katika hali yake ya kawaida hivyo amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa watulivu wakati jeshi hiulo la Polisi likiendela na msako wa kuwatafuta wahalifu wengine.