Ijumaa, 24 Januari 2014

MWANAFUNZI mmoja (Jina limehifadhiwa umri wake ni 16) wa Darasa la Saba katika  Shule ya Msingi Mkombozi iliyopo katika mji mdogo Mbalizi Wilaya ya Mbeya Mkoani hapa ameshindwa kuendelea na masomo tangu shule zifunguliwe akiogopa kuzomewa na wenzie baada ya kuhisiwa kulawitiwa na Mwalimu Mkuu wake.
Hatua ya mwanafunzi huyo kushindwa kufika shuleni kuungana na wenzie kumetokana na madai ya kuzagaa kwa tuhuma za Mkuu wake wa shule kumwingilia kimwili mwanafunzi huyo mwenye jinsia ya kiume wakati wa masomo ya jioni(Twisheni).
denti

Hii ndiyo ofisi ya mwalimu mkuu huyo ambayo ilikuwa inatumika kwa matendo machafu ya mwalimu huyo



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema atalifanyia kazi kutokana na kutokuwa Ofisini kwa wakati huo na kulitolea ufafanuzi unaotakiwa.

Ofisini kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Mbeya

 Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Mbeya, Dionice Boay alipoulizwa kuhusiana na tuhuma za Mwalimu wake alikiri kuzipata na kuongeza kuwa kutokana na Mwalimu huyo kufikishwa katika vyombo vya Sheria wao kama Ofisi hawana cha kufanya zaidi ya kusubiri Ripoti ya Polisi ambapo Mwalimu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.


Akizungumza na waandishi wa habari Mwanafunzi huyo alisema Mwalimu wake huyo ambaye alimtaja kwa jina  la Lusekelo Thom, kuwa anatabia ya kumbakiza yeye peke yake baada ya muda wa masomo ya jioni kuisha na ndipo huenda naye ofisini na kuanza kumvua nguo.

Alisema tatizo hilo limedumu kwa kipindi kirefu tangu Aprili Mwaka jana hadi Disemba 27, mwaka jana baada ya bibi anayemlea kugundua (jina limehifadhiwa kwa ajili ya upelelezi) katika mahojiano kutokana na mwanafunzi huyo kuchelewa kurudi nyumbani kila siku tofauti na wengine.
Kwa mujibu wa majirani wa Mwanafunzi huyo walisema kugundulika kwa maovu anayofanyiwa na mwalimu wake kulitokana na upotevu wa fedha shilingi 20,000 na ndipo bibi huyo alipomuona mjukuu wake akiwa na mkebe mpya na ndipo alipomuuliza kuhusu fedha zake ambapo Mwanafunzi huyo alikataa kabisa.
Walisema baada ya kubanwa zaidi alidai fedha za kununulia mkebe alipewa na Mwalimu wake na amekuwa na kawaida ya kumpa fedha mwanafunzi huyo kila siku ikiwa ni pamoja na kumwambia asilipe ada ya masomo ya jioni kwa madai kuwa atakuwa anamlipia.


Alipobanwa zaidi mwanafunzi huyo alidai kuwa baada ya kupewa fedha na mwalimu huyo huenda naye ofisini na kufunga mlango kisha huvua nguo zake na kumwamuru naye avue na kumlazimisha ashike nyeti za mwalimu wake huku mwalimu naye akimshika shika na huo mchezo ulikuwa ukifanyika kila siku na baada ya hapo mwalimu alikuwa akimrudisha mwanafunzi kwa bibi yake majira ya saa mbili usiku.


Mashuhuda wa tukio hilo na baadhi ya walinzi wa shule hiyo walikiri kuwepo kwa tuhuma za udharirishaji wa Mwalimu huyo kwa Mwanafunzi kwa madai kuwa kila siku Mwalimu huyo kujifungia ofisini na mwanafunzi ikiwa ni pamoja na kuongozana naye kila mara.


Aidha baadhi ya ndugu walisema baada ya kubaini hali hiyo walienda kutoa taarifa katika kituo kidogo cha Polisi cha Mbalizi ambapo Jeshi la Polisi lilimkamata Mwalimu huyo Januari 4, Mwaka huu na kufanya naye mahojiano kisha kumpeleka mwanafunzi huyo Hospitalini kwa ajili ya vipimo.


Hata hivyo Mwalimu huyo alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo alikataa kuhusika huku majibu ya vipimo vya Hospitali vikionesha kutokuingiliwa kimwili kwa mwanafunzi ingawa Maelezo ya mtoto alidai kuchezewa nyeti zake kila siku na kwamba suala la kuingiliwa kimwili alikuwa akilazimishwa lakini hakuweza kufanikiwa.


Mwalimu huyo aliachiwa na jeshi la Polisi katika kituo kidogo cha Mbalizi alipokuwa ameshikiliwa kwa ajili ya mahojiano baada ya kuwekewa dhamana na Mratibu wa Elimu kata ya Utengule Usongwe, Fredrick Silumbwe, na kwamba upelelezi bado unaendelea ili kubaini kama kweli mwalimu huyo anafanya vitendo hivyo huku kukiwa na taarifa kuwa Mwalimu huyo baada ya tukio hilo alisafiri na kuelekea Kibaha Mkoani Pwani ambako yuko hadi sasa.


Kwa upande wake Mratibu Elimu kata alipoulizwa kuhusiana na tuhuma dhidi ya mwalimu wake alisema hata yeye amekuwa anazisikia mitaani na kuhusu kuweka dhamana alikiri kwa madai kuwa alipigiwa na baadhi ya walimu na ndipo alipofanya hivyo kutokana na dhamana ni haki ya kila mtu.


Naye Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Mbeya, Dionice Boay alipoulizwa kuhusiana na tuhuma za Mwalimu wake alikiri kuzipata na kuongeza kuwa kutokana na Mwalimu huyo kufikishwa katika vyombo vya Sheria wao kama Ofisi hawana cha kufanya zaidi ya kusubiri Ripoti ya Polisi ambapo Mwalimu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.

Alisema kama ofisi hatua ya kwanza ni kumsimamisha kazi na kuteua Mwalimu mwingine kukaimu Ukuu wa Shule ya Msingi Mkombozi wakati ofisi ikisubiri taratibu za Kimahakama kutokana na tatizo hilo kuegemea kwenye makosa ya jinai.
Aliongeza kuwa Ofisi pia inatarajia kufanya ukaguzi katika shule hiyo ili kubaini kama Mwalimu alikuwa na makosa mengine na kujua sababu ya Mwanafunzi kutoenda shule hadi sasa licha ya wenzie kuendelea na masomo.
Hata hivyo Kituo cha Haki za Binadamu kilionesha mshangao kutokana na mtuhumiwa wa tukio hilo kuachiwa kwa dhamana ili hali upelelezi haujakamilika na hakuna hatua zozote ambazo Jeshi la Polisi linaonesha kulifanyia kazi ambapo mtuhumiwa alifikishwa Polisi Januari 4, Mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kituo cha Haki za Binadamu Mkoa wa Mbeya, Said Madudu alisema Jeshi la Polisi limechukulia suala hili kama ni siasa kwa kuchelewa kuchukua hatua kwa wakati huku mtoto akiendelea kukosa haki yake ya msingi ya masomo.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema atalifanyia kazi kutokana na kutokuwa Ofisini kwa wakati huo na kulitolea ufafanuzi unaotakiwa.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa umebaini kuwepo kwa rushwa zinazopelekea upelelezi wa kesi hiyo kuchelewa kutokana na kuwepo kwa taarifa za Mtuhumiwa kutoa fedha shilingi Milioni Tatu ambazo bado haijulikani mgao wake uliwagusa akina nani.

CREDIT: MBEYA YETU

Alhamisi, 23 Januari 2014

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amewaomba wabunge, wasomi na Watanzania wawasaidie Bunge la Katiba ili liweze kupitisha hoja ya Watanzania kuwa na uraia wa nchi mbili ili uchumi wa nchi uweze kukua.
Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam jana kwenye ufunguzi wa semina ya majadiliano ya Watanzania wanaoishi nchi za nje (Diaspora) na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
“Kuna wasomi wengi wenye utalaamu wapo nchi za nje wanafanya kazi ila wanashindwa kusaidia nchi zao kwa kuwa hawana uraia wa nchi zao,” alisema Membe.
Alisema kumruhusu Mtanzania kuwa na uraia wa nchi mbili siyo kuhatarisha usalama wa nchi. “Anayeweza kuhatarisha usalama wa nchi ni sisi viongozi. Sisi hatutetei hii hoja ya kuwa na uraia wa nchi mbili ila lazima ufike wakati tuamue kufanya hivi sio uhaini” alisema.
Alisema nchi nyingine ambazo raia wao wana uraia wa nchi mbili wamekuwa wakichangia uchumi wa nchi hizo kwa asilimia kubwa tofauti na nchi yetu.
membe
Alitoa mfano wa nchi ya Ghana kuwa raia wake wenye uraia wa nchi mbili wamekuwa wakichangia uchumi wa nchi hiyo kila mwaka.
“Ghana wanachangia bilioni 2.1, Nigeria milioni 3.1, Kenya bilioni 1.6 ambazo ni dola za Marekani” alisema.
Alisema kwa Tanzania fedha zinazochangiwa na raia wake waliopo nje hazifiki hata 100,000 za Marekani, hali inayozorotesha uchumi wa nchi.
Upande wake, Msaidizi wa Waziri Mkuu Kitengo cha Uchumi na Uwekezaji, Suzani Mzee alisema Tanzania inaelekea kwenye uraia wa nchi mbili ambao utasaidia kuchangia maendeleo ya nchi.
“Mtanzania anayeishi nchi za nje anatoa misaada kwa kificho kwa kuwa hana uraia wa nchi yake ana uraia wa nchi anayoishi ifike wakati serikali ituunge mkono ili tuweze kuisaidia nchi yetu pasipo kificho,”alisema
CHANZO: NIPASHE
SIKU zote tumezoea kuona baadhi ya wanasiasa na viongozi wakiwa mstari wa mbele kupinga ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na hata kupinga ajira kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Hali hiyo imekuwa ni tofauti kwa Kigogo mmoja wa Chama Tawala CCM wilayani Mbarali mkoani Mbeya ambaye mbali na kumtumikisha mtoto aliyechini ya miaka 18 bali pia amemfanyia unyama na ukatili uliopitiliza kwa kummwagia maji ya moto kwa kile kinachodaiwa kuwa mtoto huyo anakula sana.
Kigogo huyo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Kitongoji cha Mahango kijiji cha Mageya kata ya Rujewa wilayani Mbarali aliyefahamika kwa jina la Ziada Bakari Mwihesi anadaiwa kummwagia maji ya moto mtoto Agustino Sanga(12) ambaye alikuwa akimtumikisha kwa kufanya kazi za  kuchunga mifugo yake kuanzia alfajiri hadi usiku bila kumpatia chakula cha uhakika.
Mtoto Agustino ambaye ni yatima anayelelewa na bibi yake baada ya kufiwa na wazazi wake huko wilayani Makete mkoani Njombe alianza kuishi na Mwenyekiti huyo wa chama mwaka 2011 akitokea wilayani Makete mkoani Njombe ambapo Bibi yake kutokana na kutokuwa na uwezo alimkabidhi mama huyo ili aishi naye huku akimsaidia kazi za kuchunga mifugo yake.
 jamani
Akizungumza mkasa huo mbele ya mwandishi wa habari hizi aliyefika kijijini hapo  kufuatilia taarifa za unyanyasaji dhidi yake, mtoto huyo alisema kuwa aliletwa nyumbani kwa mama huyo mwaka 2011 na Bibi yake akitokea Wilayani Makete Mkoani Njombe ili aweze kufanya kazi ya kuchunga ng’ombe kwa mwenyekiti huyo.
Alisema kuwa tukio la kuunguzwa moto lilimtokea mwezi Juni 2013 shambani kwa Mwenyekiti huyo eneo la Jangulutu majira ya usiku ambapo Mwenyekiti huyo alianza kumsimanga kwa madai kuwa amekuwa akila chakula kupita kiasi na  kusababisha watoto wake kutoshiba.
Mtoto Agustino aliendelea kusema kuwa, mama huyo aliendelea kumsimanga na ghafla alichukua maji yaliyoinjikwa jikoni yakiwa yamechemka kwa ajili ya kupika ubwabwa  usiku huo na kummwagia kifuani na baadaye kumfungia ndani huku akilia kwa uchungu.
“Nilipata uchungu mkubwa, nililia sana sikuwa na msaada wowote usiku ule mama Yule alinifungia ndani, sikupata matibabu yoyote,’’aliongea kwa uchungu mtoto Agustino.
Agustino aliendelea kufafanua mkasa huo kwa kusema kuwa  akiwa amefungiwa ndani mama huyo alikuwa akisaga  mifupa ya ng’ombe na kumpaka katika jeraha la kidonda alichounguzwa na kwamba kila alipokuwa akimpaka ndipo kidonda kilipozidi kutoa usaha.
Alisema akiwa ndani Bibi yake alianza kumtafuta ndipo siku hiyo alipofika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kumuuliza alipo ambapo alimweleza kuwa mjukuu wake aliungua moto alipokuwa akicheza karibu na moto.
Agustino aliendelea kubainisha kuwa tangu alipofika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo mwaka 2011 hajawahi kupumzika na kwamba amekuwa akitumikishwa kama Punda kuanzia alfajiri hadi usiku huku akipewa chakula kidogo.
Kwa upande wake Babu wa Mtoto huyo Method Ndelwa(55) Mkazi wa Kitongoji cha Mahango alisema mtoto huyo baada ya kufika nyumbani hapo alikuja mume wa Mwenyekiti aitwaye Seleleka Twasanga na kumuomba mtoto huyo awe anamchungia ng’ombe na mbuzi shambani kwake.
Alisema tangu mjukuu wake  alipoungua mwaka 2013 mwezi wa 6  hakuna msaada wowote ambao unatolewa na familia ya Mwenyekiti na kwamba ameendelea kuugulia na majereha yake bila kupatiwa matibabu ya uhakika.
“Mimi na Bibi wa wa mtoto huyu hatuna hali zetu ni duni  kipato chetu ni kidogo kama mnavyoona kidonda cha mtoto kinatoa usaha na hapo mwanzo kilikuwa kinatoa funza, mama mmoja Rukia Shomari alitusaidia kumnunulia dawa,’’alisema Babu wa mtoto huyo.
Alisema kuwa hakuwa anajua utaratibu wowote wa kutoa taarifa hizo kwenye vyombo vya sheria ikiwemo Polisi na kwamba tangu alipounguzwa moto walikuwa wakimuangalia tu mtoto huyo huku wakishindwa kujua  hatima yake.
“Tunaomba mtusaidie kulifikisha hili ili jamii ijue kama mna uwezo wa kumsaidia mtoto huyu tunaomba msaada wenu kumuokoa mtoto huyu’’,alisema Mzee Ndelwa.
kigogo2
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahango ambaye ndiye anayedaiwa kufanya unyama huo,Ziada Mwihesi alikana kumchoma moto mtoto huyo na kudai kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na mume wake aliyemtambulisha kwa jina la Seleleka kuwa mtoto Agustino ameungua moto  ndipo alipoondoka na kwenda shambani na kumkuta mtoto huyo akiwa ameungua kifuani.
Hata hivyo  Mwenyekiti huyo anadai kuwa  chanzo cha mtoto huyo kuungua ni kutokana na kuota moto asubuhi  wakati akipasha kiporo cha wali katika jiko la kuni na kusema kuwa mtoto huyo alishaungua moto akiwa  kwa bibi yake na kudai kuwa hapo amekuja kuungua kwa mara ya pili.
Pamoja na kufanya unyama huo Mwenyekiti huyo alionekana kutohitaji kutoa ushirikiano kwa mwandishi wa habari hizi kwa kutoa majibu ya mkato wakati alipokuwa akiendelea kuulizwa maswali  juu ya kuchomwa moto kwa mtoto huyo ambapo pia alikanusha kummwagia maji ya moto mtoto huyo kwa madai ya kumaliza chakula.
Naye  Mume wa Mama huyo Seleleka Twasanga alikiri kuungua kwa mtoto huyo na kudai kuwa yeye alipata taarifa baada ya kupigiwa simu na jirani yake ambaye wapo jirani shambani  kwamba Mtoto Agustino ameungua moto ndipo alipoondoka na kwenda shambani ili kujua chanzo cha tukio hilo.
Bw.Twasanga alisema wakati anamchukua mtoto huyo kwa Bibi yake walifanya kama kubadilishana na Bibi huyo ambaye alihitaji kila mwaka alimiwe shamba la heka mbili kwa ng’ombe wakati mtoto Agustino akifanya kazi ya kulima na kuchunga Ng’ombe na mbuzi shambani kwa Twasanga.
Akielezea zaidi mume wa mama huyo alisema aliendelea kumlimia shamba bibi wa mtoto Agustino na kukiri kutomlipa chochote zaidi ya bibi huyo kulimiwa shamba.
Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake TAMWA kimekuwa katika harakati za kupinga ukatili wa kijinsia ikiwemo unyanyasaji wa wanawake na Watoto.
Mkurugenzi wa TAMWA Valerie Msokwa kupitia jarida lake linalotolewa na taasisi hiyo alisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria ya Kimataifa ya haki ya mtoto ya mwaka 2009 iliyowekwa katika tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Mtoto linalotoa mwongozo wa kulinda na kutambua haki za mtoto nchini.
Alisema watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo wanapaswa kulindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyiwa watoto katika maeneo mengi ya mijini na vijijini.
Naye Diwani wa Kata y Rujewa Bi.Gurzar Sabil alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo la kinyama la mwenyekiti huyo alisema kuwa  hana taarifa hiyo lakini aliahidi kuwasiliana na Ofisa Ustawi wa jamii wilaya ya Mbarali ili waweze kwenda nyumbani kwa mtoto waweze kumsaidia ikiwa ni pamoja na kumkamata mtuhumiwa.
kigogo3
Mara baada ya Mwandishi wa habari hizii kuondoka wilayani humo Ofisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Mbarali Winifrida Mahali akiambatana na Mratibu wa Dawati la Jinsia wilayani humo Christa Komba walifika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kumchukua hadi kituo cha Polisi.
Bi Mahali alisema kuwa walimfuata mtuhumiwa pamoja na mumewe na kuwapeleka kituo cha polisi ambako walilala hadi asubuhi  na kufikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mbarali ambako wamesomewa mashtaka ya kujeruhi na wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana hadi Januari 29.