Wadau wa maendeleo ya elimu nchini wakimsikiliza Waziri wa Elimu na 
Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa alipokuwa akizindua mpango 
mkakati wa kuinua sekta ya elimu ujulikanao kama Matokeo Makubwa Sasa 
(BRN), Dar es Salaam 
            
Mpango huo uliozinduliwa jana, utekelezaji wake 
ulianza Aprili mwaka huu na moja ya utekelezaji wake ni kuhakikisha kuwa
 matokeo ya wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani wa darasa la saba 
wiki tatu zijazo, kidato cha nne miezi miwili ijayo yanakuwa mazuri, 
jambo ambalo limepingwa na wadau hao.
Mara baada ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya 
Ufundi, Dk Shukuru kuzindua mpango huo, Wakurugenzi wa taasisi 
mbalimbali za elimu za Serikali pamoja na maofisa elimu wa mikoa yote 
nchini walikula kiapo cha kuhakikisha kuwa wanasimamia mpango huo 
kikamilifu.
Wakati wakiapa, wengi walikuwa wakisema kuwa 
watajitahidi, kujituma ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya haraka 
yanapatikana na kukwepa kutamka wazi kuwa mpango huo utafanikiwa, jambo 
ambalo liliwafanya mamia ya watu waliohudhuria uzinduzi huo 
kuwashangilia.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti 
walisema ni ndoto kwa wanafunzi kufanya vyema katika mitihani yao ya 
darasa la saba, kidato cha nne katika muda uliobaki.
Akizindua mpango, Dk Kawambwa alisema kuwa 
utekelezaji wake ulishaanza tangu mwezi Aprili na kwamba anatarajia 
matokeo ya haraka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa 
Amandina Lihamba alisema Serikali imekuwa na mipango mingi mizuri mno, 
lakini tatizo liko kwenye utekelezaji. Naye Mwenyekiti wa Chama cha 
Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzani (Tamongsco), Mak Mringo alisema kuwa 
kiapo walicholishwa wakurugenzi wa elimu katika uzinduzi huo 
hautekelezeki kwa kuwa mpango huo uko kinadharia zaidi.
Kuhusu motisha kwa walimu ambayo ni mkakati wa 
mpango huo, Mringo alisema kuwa Serikali inazo fedha za kumaliza madai 
ya walimu, ila hakuna mfumo mzuri wa kuhakiki madeni hayo.
Naye Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya 
Morogoro vijiji, Donald Wilson alisema mkakati huo hautaleta matokeo 
mazuri kwa mwaka huu.
Naye Kada wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), 
Mutamwega Mugaywa ambaye pia ni mdau wa elimu, japo aliusifu mpango huo 
alisema umechelewa.
Ofisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Mayasa Ali Hashim 
alisema kwa mwaka huu haitawezekana kwa mpango huo kutekelezeka kwa 
maelezo kuwa muda uliobaki kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha 
nne kufanya mitihani yao ya mwisho, ni mfupi.
Na Elias Msuya na Fidelis Butahe
Na Elias Msuya na Fidelis Butahe
Jumatano, Septemba 04, 2013
Unknown
  
0 comments :
Chapisha Maoni