Jumatatu, 25 Novemba 2013





PART ONE

JUMANNE iliyopita Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are maarufu kama Mzee Kinesi mbele ya waandishi wa habari alitangaza kamati ya utendaji ya klabu hiyo kukubaliana kumsimamisha mwenyekiti Ismail Aden Rage.

Rage alisimamishwa baada ya kamati hiyo kutoridhishwa na utendaji wake lakini kuu ni kukataa kipengele cha marekebisho ya katiba ya klabu hiyo. Mambo yametajwa kumuhusu Rage lakini mengine ni juu ya uuzwaji wa wachezaji Emmanuel Okwi na Mbwana Samatta na sambamba na mkataba wa Azam TV.

Mapinduzi hayo yasiyo rasmi yalitangazwa wakati Rage akiwa Sudan katika vikao vya kamati za bunge za Afrika zinazoshuhulika na hesabu za serikali hivyo wakati uamuzi huo unatangazwa Rage hakuwepo nchini.



PART TWO

Ijumaa ya Novemba 21, 2013 Rage aliwasili nchini kutoka Sudan akiwa na donge moyoni mwake, na kwa bahati nzuri aliwasili salama uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam huku akilakiwa na kundi la mashabiki wachache wa klabu yake.


Apanda ndege moja na Hanspope


Rage aliwasili nchini na ndege ya Shirika la KQ majira ya saa 1:30 akitokea Nairobi ambako aliunganisha ndege akitokea Sudan na kwa bahati alipanda ndege moja na Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope.

Hanspope alikuwa wa kwanza kutoka uwanjani hapo na kudakwa na waandishi wa habari waliotaka kujua sababu za yeye kuwepo uwanjani pale, na moja kwa moja alijibu kwamba; “Mimi nimetoka Lubumbashi (DR Congo) katika biashara zangu na Rage nimepanda naye ndege moja.”

Aliongeza; “Nimekaa naye jirani kabisa na tumezungumza mengi lakini nimemuhakikishia kwamba nilikuwepo kwenye kikao cha kamati kilichomsimamisha.Msubirini aje hapa mzungumze naye tena msimsubiri hapo maana yeye anatokea VIP.”

Baadaye saa 1:45 Rage alichomoza katika lango la VIP na moja kwa moja alikutana na kundi la mashabiki wa Simba na waandishi wa habari ambao walimuhoji maswali lukuki lakini alisimamia msimamo wa kuozungumza hadi kesho yake (jana jumamosi).

“Nashukuru nimefika salama na napenda kuwaambia kwamba mimi ndiye mwenyekiti wa Simba hakuna mtu mwingine mwenye cheo hicho,” alipoulizwa zaidi kuhusu uamuzi wake juu ya maamuzi hayo ya kamati, Rage alisema; “Unajua rafiki yangu Zitto Kabwe amepata matatizo ya kusimamishwa katika chama chake kwa hiyo sipo katika mood ya kujibu maswali mengi.”

Rage akasema; “Kesho Jumamosi nitazungumza na waandishi saa saba kamili.”


Aondoka na kamsafara zake


Baada ya kauli hiyo, Rage aliondoka uwanjani hapo na gari aina ya Toyota Granvia lenye namba za usajili T 300 CPR. Gari hilo lilifuatiwa na mabasi matatu yenye uwezo wa kuchukua abiria wasiozidi 25 ambalo la kwanza lilikuwa na namba za T 885 BNT, T 208 BFM na lingine lenye namba T 549 BZQ.

Msafara huo wa Rage ulienda hadi makao makuu ya klabu hiyo ambapo ulisimama kwa muda kisha ukaondoka klabuni hapo huku kila mmoja akidhani kesho Rage atatoa neno.


PART THREE


Huku umma ukiwa na shauku ya kufahamu kitakachozungumzwa na Rage, asubuhi ya Jumamosi ya jana, likatoka tangazo kwamba, Rage hasingeweza kuzungumza siku hiyo na badala yake atafanya hivyo leo Jumapili.

Sababu kubwa ya Rage kutozungumza jana ilisemwa ni yeye kupata nafasi ya kwenda TFF kupeleka barua yake ya kuelezea mchakato wake wa kusimamishwa ikiwa ni baada ya Mzee Kinesi kupeleka barua ya kumsimamisha Rage.



PART FOUR


Mungu si Athuman, TFF ikaona Rage ana hoja na moja kwa moja ikamuagiza aitishe mkutano wa wanachama ndani ya siku 14 ili kumaliza tofauti za kiungozi zilizopo.

TFFilitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa mgogoro katika klabu baada ya kupokea barua mbili; moja kutoka Kamati ya Utendaji ikielezea kumsimamisha uongozi Rage, na nyingine kutoka kwa Mwenyekiti huyo ikielezea kutotambua kusimamishwa huko.

Uamuzi wa TFF ulifanywa kwa kuzingatia Ibara ya 1(6) ya Katiba ya Simba inayosema: “Simba Sports Club ni mwanachama wa TFF, itaheshimu Katiba, kanuni, maagizo na uamuzi wa TFF na FIFA, na kuhakikisha kuwa zinaheshimiwa na wanachama wake.”

TFF ikasema itatuma wawakilishi wake katika mkutano huo, na kumuagiza Mwenyekiti wa Simba kuhakikisha wanachama wote wenye hoja wanapata fursa ya kusikilizwa.


PART FIVE


Leo hii Rage amesema hawezi kuitisha mkutano mkuu wa dharura kama alivyoelekezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuwa shirikisho hilo halina mamlaka ya kufanya hivyo.

Rage alisema TFF haiwezi kumlazimisha kufanya hivyo na ikiendelea kumlazimisha kufanya hivyo atajiuzulu nafasi yake kwani amechoka kuona anaonewa kila siku.


Kina Mzee Kinesi walikaa kikao cha harusi


“Watu walionisimamisha wanasema ni maamuzi ya kamati ya utendaji, hii siyo kweli kile hakikuwa kikao cha kamati ya utendaji bali ni kikao cha kawaida tu kama kikao cha harusi.

“Katiba ya Simba ibara ya 28 (1) kuanzia a, b, c mpaka d inasema wazi kwamba, maana ya kamati ya utendaji ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe saba. Na kamawakitaka kukaa, mwenyekiti ndiye mwenye jukumu la kuitisha kikao au makamu mwenyekiti kwa ridhaa ya mwenyekiti kama akiona kuna ulazima wa kufanya hivyo,” alisema Rage.

Rage alisema katiba ya Simba inamtaka mwenyekiti kuitisha vikao vinne kwa mwaka, yaani kimoja kila baada ya miezi mitatu.”Sasa mimi nimeshaitisha vikao 12 ndani ya mwaka huu,” alihoji Rage. 


Aidindia TFF, aishangaa kuwatambua kina Kinesi


Rage anasema alipeleka barua yake TFF kuelezea uhuni huu uliofanywa na hao watu, lakini anashangaa kwa nini TFF hawakutoa tamko lolote la kulaani kinachoitwa mapinduzi na badala yake wanamlazimisha kuitisha mkutano.

“Katika katiba ya Simba, Ibara ya 22 inaelezea kuhusu mkutano mkuu, haya si maneno yangu lakini nanukuu hapa, inasema mwenye wajibu wa kufanya hivyo ni mwenyekiti kwa kushirikiana na kamati ya utendaji kama anaona inafaa. Sasa hili la maelekezo ya TFF linatoka wapi?,” alihoji Rage.


Adai kuna mbaya wake TFF, wakimzingua anajiuzulu


Rage anasema kuna kiongozi mmoja yupo ndani ya TFF ambaye zamani alikuwepo Simba na akashindwa akaondoka zake lakini sasa ndiye anayemchafua ili tu aweze kurejea Simba lakini yeye anamuachia mungu.

“Kuna kiongozi mmoja aliyekuwa Simba na sasa yupo ndani ya kamati ya utendaji ya TFF, huyu ananiandama na kunichafua kila siku. Niliwapelekea TFF barua ya mambo yote haya na ilipaswa kamati ya maadili ipitie lakini badala yake kamati ya utendaji ndiyo iliyofanya kazi hiyo, hakuna kitu kama hicho. Sasa wakiendelea kulazimisha mkutano mimi nitajiuzulu.”

“Tazama mfano huu, wakati uchaguzi wa TFF ulipoingia katika mgogoro kwa baadhi ya wagombea, Fifa ilielekeza uchaguzi huo ufanyike baadaye lakini si kwa kuipangia TFF kama wanavyoniambia mimi,” alisema Rage na kuongeza.



Amuingiza vitani Wambura, ampa ulaji Malkia wa Nyuki


Rage kabla hajamaliza mkutano wake na waandishi wa habari alitangaza kumteua Michael Wambura kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba na huku akimtaja Rahma Al Kharoos kuwa mjumbe wa baraza la wadhamini la Simba.

“Namtangaza Michael Wambura kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, huyu anachukua nafasi ya malkia wa nyuki (Al Kharoos) aliyeniomba kutolewa katika kamati hiyo kutokana na kubanwa na kazi zake.

“Nimemuomba malkia wa nyuki aingie katika baraza la wadhamini na kuanzia sasa yeye atakuwa mmoja wa wajumbe wa baraza la udhamini na jina lake nitalipeleka likathibitishwe na mkutano mkuu hapo baadaye,” alisema Rage.

Kwa uteuzi huo ina maana Rage sasa atakuwa na mjumbe mmoja anayemuunga mkono ambaye ni Wambura. Wambura huyu anaelezwa kutowakubali Friends of Simba kundi linaloiongoza Simba kwa sasa.


Awaacha waandishi bila kujibu maswali, aondoka nchini


Muda mfupi baada ya mkutano huo na waandishi wa habari, Rage aligeuka mbogo kwa kukataa kujibu maswali ya waandishi wa habari huku akisema anayetaka kuandika habari hiyo naandike na asiyetaka aachane nayo.

“Sitaki maswali hapa, anayetaka kuandika aende kuandika na asiyetaka aache, wengi humu mnatumiwa na hawa watu, sasa ni kipi mtakachoniuliza?, sitaki swali tuondoke,” alisema Rage huku akinyanyuka.


PART SIX


Mtandao huu uliwasiliana na TFF ambapo kaimu katibu mkuu wake ndiye aliyepatikana na aliposomewa maamuzi ya Rage, akasema hakuna tatizo kwa Kamati ya Utendaji ya TFF kutoa uamuzi huo hivyo si kweli kwamba hawakuwa sahihi kutoa maelekezo hayo kwa Rage.

Wambura alisisitiza kwamba, wanasubiri siku 14 ziishe halafu wachukue uamuzi endapo mkutano mkuu hautafanyika ndani ya Simba.

“Sisi tunangoja siku 14 zipite halafu utaona tunafanya kitu gani leo  ndiyo kwanza siku ya pili, yeye kama amesema hivyo wacha tungoje siku 14 ziishe halafu tutakuwa na uamuzi wetu,” alisema Wambura.

 1. Utangulizi Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. 

Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013.
 
 Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. 

Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
  
Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika.  
Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA.  
Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho. 
  
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. 
 Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. 
 
Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama. 
  
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili: 
  • Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
  • Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
  • Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
  • Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.

 ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua. 
  
iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. 
 Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. 
 
Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho. 
  
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. 
 Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko. 
  
v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae.  

Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo: 
  • Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
  • Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.

 vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili: 
  • Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
  • Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala lakimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
  • Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.

 3Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA.  
Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo: 
  1. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
  2. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.

 4. Hitimisho Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. 
 Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'.
 
 Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. 
 
Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
  
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
  
Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
  
 Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka. 
  
Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia.  
Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.
  
Kabwe Zuberi Zitto, Mb Dar es Salaam. 24 Novemba, 2013
Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation, Yesaya Mwakifulefule wakipeana mikono na wasanii kutoka nchini Nigeria maarufu kwa jina la P Square (Peter na Paul Okoye), wakati walipotembelea kituo cha watoto wenye ulemavu wa Utindio wa Ubongo cha Msimbazi Mseto jijini Dar es Salaam, ambapo wasanii hao walitoa msaada kwa watoto hao wenye ulemavu huku ikiwa ni njia moja ya kushiriki kazi ya kijamii.



Alhamisi, 14 Novemba 2013

Marehemu  John Mwankenja, enzi za uhai wake
Mauaji yalifanyika katika gari yake  yenye namba za usajili T127 ACZ AINA YA TOYOTA HILUX  
Kushoto Hakimu Mwakalinga ambaye ni mshtakiwa wa kwanza kuhukumiwa kunyongwa
Baadhi ya wananchi wakiwa nje ya mahakama wakisubiria matokeo ya hukumu


WATUHUMIWA wawili kati ya wanne  wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya.

Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya iliyokuwa ikiendesha vikao vyake katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe chini ya Jaji Samweli Karua, baada ya kuahirishwa kutolewa kwa hukumu hiyo kwa zaidi ya mara tatu na kuzua hali ya sintofahamu kwa ndugu wa washtakiwa na wafuatiliaji wa kesi hiyo.

Awali kabla ya kusoma kwa hukumu hiyo Mwendesha mashtaka wa Serikali., Archiles Mulisa, aliwataja watuhumiwa wote wanne kuwa ni Hakimu Mwakalinga, Daudi Mwasipasa, Obote Mwanyingili na Kelvin Myovela wanaokabiliwa na tuhuma za kumuua kwa maksudi aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe John Mwankenja.



Alisema watuhumiwa hao wenye kesi namba 131/2012 walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.


Mulisa aliyekuwa akisaidiwa na Wakili wa Serikali Lugano Mwakilasa kwa upande wa mashtaka huku  Watuhumiwa wakitetewa na Mawakili wawili ambao ni Victor Mkumbe na Simon Mwakolo.

Mulisa alidai mahakamani hapo kuwa kesi inayowakabili  watuhumiwa hao walilitenda Mei 19,2011 kwa kumuua kwa maksudi John Mwankenja kinyume na kifungu cha 196 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Karua ambaye alianza majira ya saa 14:37 mchana na kukamilisha saa 15:37 alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka na utetezi haubishaniwi kuhusu kifo cha marehemu.

Aliongeza kuwa pande hizo mbili pia hazibishaniwi kuhusu ripoti za kitaalamu na dhamira za mauaji hayo bali kinachobishaniwa ni uhusika wa watuhumiwa hao dhidi ya mauaji hayo.

Alisema katika kutetea hoja zao upande wa mashtaka ulileta mashahidi 11 ambao wote kwa pamoja  wakiongozwa na shahidi namba moja waliwatuhumu washtakiwa kuhusika na tukio hilo.

Shahidi huyo namba moja Weston Jacob(17) mkazi wa Kiwira Mwanafunzi kidato cha Tatu katika shule ya Sekondari Kipoke ambaye pia ni Mjomba wa marehemu ambaye aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio akiwa nyumbani akijisomea majira ya 2: 30 usiku ambapo marehemu alifika nyumbani na kupiga honi ya gari akitaka afunguliwe mlango.


Mbali na ushahidi huo Jaji Karua alisema pamoja na ushauri wa wazee wa baraza la mahakama ambao pia wanawatuhumu washtakiwa hao kuhusika na tukio hilo nae anakubaliana nao lakini siyo kwa watuhumiwa wote.

Kutokana na ushahidi huo alisema Mshtakiwa namba moja na namba mbili ambao ni Hakimu Mwakalinga na Daudi Mwasipasa wanatiwa hatiani kuhusika moja kwa moja na mauaji kutokana na ukiri wao kwa mlinzi wa amani, Mchukua maelezo na  vipimo vya vinasaba.

Alisema Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili yeye anatiwa hatiani kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji hivyo yeye hausiki moja kwa moja na kosa hilo.

Jaji karua alisema kwa upande wa mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela anatiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika nkatika mauaji hayo ingawa hakusika na kitendo hicho moja kwa moja.

Aliongeza kuwa kutokana na kifungu cha sheria cha mwenendo wa makosa ya jinai kifungu namba 300 na 217 washtakiwa namba tatu na namba nne wanatiwa hatiani na mahakama.

Mwendesha mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa, aliiambia mahakama hiyo kwamba itoe adhabu kali kutokana na kitendo alichofanyiwa marehemu na iwe fundisho kwa watu wengine.

Kwa upande wa utetezi ambao siku ya hukumu uliwakilishwa na Wakili Merick Luvinga alisema mahakama iwanee huruma washtakiwa kwa kuwa wote umri wao ni mdogo wanaweza kujifunza na kurudi kuungana na jamii pia ni kosa lao la kwanza hivyo wasipewe adhabu kali.

Kutokana na utetezi huo, Jaji Karua alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuthibitisha kuhusika pasipo shaka kwa washtakiwa namba moja na namba mbili hivyo adhabu yao ni kunyongwa hadi kufa.

Aliongeza kuwa Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili anayehusika kumhifadhi mtuhumiwa wa kwanza ataenda jela miaka saba kwa kosa hilo sambamba na mshtakiwa namba nne  Kelvin Myovela aliyehifadhi silaha iliyotumika kwenye mauaji.

Alisema kutokana kosa hilo mtuhumiwa huyo atatumikia kifungo jela miaka saba ingawa pia tayari alikuwa amehukumiwa kifungo jela cha miaka 20 kwa kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria.

Wakati huohuo

MAHAKAMA kuu kanda ya Mbeya imemhukumu kwenda jela miaka 35 mtuhumiwa wa mauaji dhidi ya watoto huku mwingine akiachiwa huru baada ya kukutwa bila hatia.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji wa Mahakama kuu kanda ya Mbeya Samweli Karua mbele ya mwendesha mashtaka wa serikali Archiles Mulisa katika vikao vilivyofanyika katika Mahakama ya wilaya ya Rungwe.

Awali mwendesha mashtaka wa serikali Archiles Mulisa aliiambia mahakama kuwa washtakiwa Baraka Mwandibwa na Zuberi Lwila walifikishwa mahakamani hapo wa kosa la kumlawiti na kumuua mtoto Esta James(5) Novemba 21, 2010.

Alisema kosa hilo ni kinyume cha sheria kifungu cha 196 (16) kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambalo walilifanya katika kijiji cha Bulyaga Wilayani Rungwe baada ya kumteka mtoto huyo.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Karua alisema Mshtakiwa namba moja anatiwa hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ambao ulitoka kwa shahidi namba moja ambaye ni mtoto aliyejulikana kwa jina la Marietha.

Alisema mtoto huyo ambaye alisema siku ya tukio alikuwa akicheza na marehemu ambapo mtuhumiwa alifika na kumpa pipi aina ya Ivory marehemu kisha kuondoka naye ambapo shahidi huyo aliwerza kumtambua mtuhumiwa katika gwaride la utambuzi.

Mbali na hilo alisema ushahidi mwingine ni ushaidi wa Vinasaba ambao unawahusisha moja kwa moja watuhumiwa wote wawili ikiwa ni pamoja na ushaidi wa kimazingira unaomhusisha mtuhumiwa wa kwanza.

Alisema kutokana na ushahidi huo Mtuhumiwa wa kwanza anahusika moja kwa moja na mahakama inamtia hatiani ingwa kwa mujibu wa ushahidi hakuua kwa makusudi kutokana na kutokuwa na vifaa vya mauaji kama visu panga na silaha zingine.

Alisema katika mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa unadamu na mbegu za kiume sehemu zake za siri na hakuwa amejeruhiwa nsehemu yoyote, hivyo mahakama iliona mtuhumiwa hakuua kwa kukusudia bali ilikuwa ni bahati mbaya.

Hata hivyo upande wa Mshtaka uliomba mahakama itoe adhabu kubwa na kali dhidi ya washtakiwa kutokana na mazingira aliyofanyiwa mtoto huyo ili iwe fundisho kwa wanaume wengine wenye tabia za kuwalaghai watoto wadogo.

Akitoa hukumu hiyo Jaji karua alisema anakubaliana na ushauri wa upande wa mashtaka kwamba tukio hilo ni kubwa na mstakiwa wa kwanza Baraka Mwandibwa ataenda jela kwa miaka 35 huku mshtakiwa wa pili Zuberi Lwila akiachiwa huru baada ya kutokuwa na ushahidi wa kuhusika katika tukio hilo.





Novemba 12, 2013
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) imefungia viwanja saba vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya mechi za mpira wa miguu.
Uamuzi huo umefikiwa na TPL Board katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika juzi (Novemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa kwanza.
Viwanja vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika kwanza ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji), na Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo (dressing rooms) havina 
hadhi).
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea- pitch ni mbovu), 
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha (pitch ni mbovu), 
Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili ya shule ya awali), 
Uwanja wa Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) 
na
 Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (pitch ni mbovu).
Klabu ambazo timu zake zinatumia viwanja hivyo zimeshaarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo ambapo ama vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo ili wafanye marekebisho au kutafuta viwanja vingine vya kuchezea mechi zao.
Kwa upande wa ripoti za mechi za VPL;
     Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 na kupewa onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza mechi ya utangulizi walipocheza na Yanga. Pia wanatakiwa kulipa gharama za uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja kioo cha basi la Yanga baada ya gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya Ligi.
Pia Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kushambulia basi la wachezaji wa Tanzania Prisons baada ya mechi dhidi yao, na kulipa gharama za uharibifu baada ya kuthibitisha na Bodi ya Ligi.
     Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake ilipocheza na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi Hassan Zani alishambuliwa kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na kichwa, tukio lililosababisha mchezo kusimama kwa dakika tatu.
Beki wa Coastal Union, Hamad Khamis wa Coastal Union amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam. Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu zinazofuata za timu yake.
      Mchezaji Cosmas Lewis wa Ruvu Shooting alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kupiga kelele wakati mgeni rasmi akisalimia timu na kukataa kupeana mkono na kamishna kwenye mechi dhidi ya Rhino Rangers, hivyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000.
      Mtunza vifaa (Kit Man) wa JKT Ruvu, Selemani Oga aliondolewa kwenye benchi la ufundi wakati wa mechi yao dhidi ya Mbeya City kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa refa, hivyo suala lake litapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Kocha Msaidizi wa Oljoro JKT, Fikiri Elias amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kumshambulia kwa matusi refa wakati wa mechi yao dhidi ya Ashanti United. Naye mtunza vifaa wa timu hiyo Elas Justin amepelekwa Kamati ya Maadili kwa kumshambulia refa kwa matusi ya nguoni.
Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar.
Katika FDL, mchezaji Ally Mtoni wa Villa Squad amepigwa faini y ash. 200,000 na kufungiwa mechi tano. Kosa lake ni kujisaidia haja ndogo golini wakti wa mechi dhidi ya Ndanda FC iliyochezwa mjini Mtwara.
Kamishna Paul Opiyo wa mechi ya FDL kati ya Villa Squad na Transit Camp kwa kutokuwa makini. Katika ripoti yake ameeleza kuwa Transit Camp ilichelewa kufika uwanjani, lakini hakusema ilichelewa kwa muda gani.
Kocha wa Polisi Dar es Salaam, Ngelo Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo Mrimi Masi wamepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi tatu kila mmoja kwa kuongoza kundi la washabiki kumvamia refa wa mechi yao dhidi ya Villa Squad iliyochezwa Dar es Salaam.
Pia Bodi ya Ligi imeagiza Polisi waandikiwe barua ya onyo kwa vile wakati waamuzi wanapigwa walikuwepo lakini hawakutoa msaada kwa wakati.
Kocha wa Friends Rangers, Kheri Mzozo amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kosa la kumtukana refa na kutishia kuhamamisha washabiki waingie uwanjani kufanya fujo kwenye mechi dhidi ya Villa Squad.
Naye Kocha msaidizi wa timu ya Transit Camp, Haji Amiri amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi wa akida wakati wa mechi dhidi ya Friends Rangers.Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa kanuni. 
     Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ili kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili (Novemba 17 mwaka huu).
FUTURE YOUNG TAIFA STARS vs TAIFA STARS UWANJANI KARUME
Timu ya Taifa ya Future Young Taifa Stars imeibamiza bao 1 Taifa Stars katika mechi iliyochezwa leo (Novemba 13 mwaka huu). Mechi hiyo ya kirafiki imefanyika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi hiyo ilikuwa maalumu kwa Benchi la Ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na Kim Poulsen kuangalia wachezaji kumi kutoka Future Taifa Stars watakaoongezwa katika Taifa Stars tayari kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Novemba 19 mwaka huu jijini Arusha.
Watazamaji 300 tu wataruhusiwa kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini jana (Novemba 12 mwaka huu). Miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kuripoti ni kipa Ivo Mapunda wa Gor Mahia ya Kenya
                    
               Boniface Wambura Mgoyo
                Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF)

Jumatano, 13 Novemba 2013

Marehemu Dk. Sengondo Mvungi alipokuwa ICU katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.


Habari za kusikitisha zilizotufikia jioni hii zinasema kuwa Dk. Sengondo Mvungi amefariki dunia katika Hospitali ya Milpark Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa. Dk. Mvungi alipelekwa wiki iliyopita Nov. 7 mwaka huu kwa ajili ya kupewa matibabu zaidi akitokea Hospitali ya Muhimbili kitengo cha MOI ambako muda wote alikuwa hajitambui baada ya kushambuliwa na majambazi na kuumizwa vibaya sehemu ya kichwani akiwa nyumbani kwake Kibamba. Wakati Dk. Mvungi anafariki, jana Jeshi la Polisi, kupitia  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, lilitangaza kuwakamata watuhumiwa 9 wakiwa na mapanga yaliyotumika katika uvamizi huo.
Mpaka mauti yanamfika, Dk. Mvungi alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini na Mhadhiri Mwandamzi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Bagamayo (UB).
Marehemu aliwahi kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi.

---SOURCE: GPL