Jumamosi, 9 Novemba 2013


      Kutoka kushoto kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya akiongea na waandishi wa Habari,kulia kete inayosadikika kumuua kijana huyo baada ya kupasukia tumboni  .


MAITI ya kijana aliyejulikana kama Kassim Said Mboya (36), mkazi wa Jijini Dar es Salaam, imekutwa na kete 65 za zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.



Taarifa zilizolifikia Tanzania daima tangu jana jioni, zilieleza kuwa maiti ya kijana huyo, ilikutwa katika basi la kampuni ya Taqwa eneo la Kasulumu lililokuwa likitokea Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania na kuelekea nchini Malawi.



KYELA NYUMBANI blog ilifuatilia na kujua ukweli wake kisha kuwasiliana na kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani leo asubuhi, ambaye pia alikiri kuwepo kwa maiti hiyo na kumwambia mwandishi wakutane eneo la chumba cha maiti cha hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya kuona mwili wa marehemu huyo.



Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, alisema kuwa kijana huyo kabla hajafariki, alikamatwa Novemba 7, mwaka huu akiwa ndani ya basi hilo lenye namba za usajili T 319 BLZ akiwa na tiketi yenye jina la Kassim Mueck Michael.



‘’Awali basi hilo kabla ya kufika mpakani Kasumulu na abiria kushuka na kuanza kufanya taratibu za kuvuka mpaka na kuingia nchini Malawi, marehemu alibaki kwenye gari huku afya yake ikizidi kudhoofika’’ alisema Kamanda Dwani Athumani.



Alisema baada ya kuona hivyo, wahusika wa basi hilo walitoa taarifa kituo cha polisi ambapo kijana huyo alichukuliwa na kupelekwa katika hospitali ya wilaya ya Kyela na kabla hajapata matibabu alifariki dunia.



Alieleza kuwa, kwa kuwa kijana huyo kabla hajaaga dunia alikuwa na dalili zilizogundulika kuwa alikuwa na dawa za kulevya, iliamuliwa mwili huo kusafirishwa mpaka hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambako ulipasuliwa na kukutwa na pipi 65 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya na moja ikiwa imepasuka.



‘’Natoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya na nchi nzima kwa ujumla kufika hospitali ya rufaa ya Mbeya kwa ajili ya utambuzi wa mwili wa marehemu na kwamba ijulikane kuwa usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya ni hatari kwa afya ya mtumiaji’’ alisema Kamanda Diwani.



Alipoulizwa kuwa kutokana na mkanganyiko uliowahi kujitokeza katika upotevu na kuwa dawa zilizowahi kukamatwa awali hazikuwa dawa, alisema kuwa kikosi kazi chake kimejipanga vema na jitihada za kupeleka kwa mkemia mkuu zinafanywa chini ya kikosi kidogo cha ulinzi na usalama cha mpaka wa Kasumulu.



Hii ni maiti ya tatu kukamatwa na dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya mkoani Mbeya, ambapo shehena ya kwanza ya dawa hizo ilikamatwa mwaka mjini Tunduma mkoani hapa mwaka 2006 ikiwa kwenye tumbo la marehemu Kombo Siriri.



Shehena ya pili ya dawa hizo ilikamatwa Desemba 5, 2011 katika hotel ya High Class mjini Tunduma, ikiwa katika tumbo la maiti ya Mshanga Mwasala.



Licha ya ukamataji wa dawa hizo na baadhi ya watuhumiwa wakiwa haia, hakuna mtuhumiwa aliyewahi kupatikana na hatia tangu mfululizo wa ukamata dawa hizo zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya mkoani Mbeya.





 Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari nje ya ofisi yake huku akiwa na baadhi ya askari wa jeshi hilo mkoani hapa.

 Pasi ya kusafiria kijana huyo alizokutwa nazo...



 Kete zilizokutwa tumboni mwa kijana huyo baada ya kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya.



 Kulia ni kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, akiwa amevalia mavazi maalum, kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Mbeya kwa ajili ya kuona maiti hiyo.



 Maiti ya kijana Kassim Said Mboya ukiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Mbeya baada ya kufanyiwa upasuaji na kutolewa dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya.





*Wananachi watakiwa kufika Rufaa Mbeya kuitambua maiti ya kijana huyo

*Ni maiti ya tatu kukamatwa ikiwa na kete za namna hiyo

0 comments :

Chapisha Maoni