RAIS Jakaya Kikwete anatarajia kuipanga upya safu ya Baraza lake la Mawaziri wakati wowote, huku baadhi ya wabunge na mawaziri wakitakiwa kusitisha mapumziko yao ya mwisho wa mwaka na kurejea jijini Dar es Salaam haraka.
Miongoni mwa wabunge waliositisha mapumziko yao na kurejea nchini ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa nchini Afrika Kusini na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliyekuwa Uswisi.
Wabunge hao walipoteza nafasi zao za uwaziri baada ya ripoti ya Kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, kuwagusa mawaziri hao kwamba walishindwa kuwajibika katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Dk. Nchimbi anapewa nafasi ya kurejea kwenye Baraza la Mawaziri kutokana na kushiriki kwake kuipinga operesheni hiyo, ambayo kwa kiwango kikubwa ilikuwa chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na kwamba alishawahi kumuandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiipinga.
Kwa upande wake Kagasheki, anatajwa kurudi kwenye Baraza la Mawaziri kutokana na kubainika kwamba hakuwa na kosa na kwamba operesheni hiyo ilitekelezwa zaidi kijeshi na haikuwa chini ya wizara yake moja kwa moja.
Aidha Kagasheki anatajwa kuwa mmoja wa waliokuwa mawaziri hodari kutokana na uwezo wake wa kufuatilia mambo, ambapo akiwa ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, alianza harakati za kukomesha biashara haramu ya pembe za ndovu.
Wakati Kagasheki na Dk. Nchimbi wakipewa nafasi ya kurejea kwenye Baraza la Mawaziri, pia zipo taarifa kwamba wapo baadhi ya wabunge wataingia kwa mara ya kwanza kwenye baraza hilo, huku wengine wakirudishwa kwa mara ya pili.
Taarifa za uhakika kutoka kwa watu wa karibu wa baadhi ya wabunge, zimebainisha kwamba jana Rais Kikwete aliwaita Ikulu wabunge wawili vijana, hata hivyo haikujulikana waliitwa kwa sababu gani.
Baadhi ya wabunge wanaotajwa kujumuishwa kwa mara ya kwanza kwenye baraza hilo ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala, Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Kahama, James Lembeli, sambamba na mmoja wa wabunge vijana kutoka mikoa ya Iringa na Njombe.
Wakati wabunge hao wakiitwa Ikulu, zipo taarifa za uhakika kwamba mawaziri wote wametakiwa kusitisha mapumziko yao ya mwisho wa mwaka na kurejea Dar es Salaam.
Hatua hiyo ya kutajwa kwa baadhi ya wabunge kuingia kwenye Baraza la Mawaziri imewatia hofu baadhi ya mawaziri, hasa wale walionyooshewa vidole na chama chao kwamba ni mawaziri mizigo.
Mawaziri waliotajwa na CCM kuwa ni mizigo wamekuwa hawana matumaini ya kurejea kwenye baraza hilo na kwamba wanaamini wao ndio watakuwa wa kwanza kutemwa.
Wakati baadhi ya mawaziri wakiwa na hofu, zipo taarifa kwamba mmoja wa wabunge wanaotoka Mkoa wa Mbeya ameshaanza kufanya sherehe, akiamini kwamba amejumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Aidha imebainika kwamba wapo baadhi ya manaibu waziri wameshaanza kujipigia debe ili kupandishwa na kuwa mawaziri kamili.
Mchakato huo wa kujipigia debe unachagizwa na utaratibu wa Rais Kikwete wa kuwapandisha hadhi manaibu waziri kuwa mawaziri kamili.
Tayari baadhi ya Manaibu Waziri kama Amos Makala, Lazaro Nyalandu na January Makamba, Aggrey Mwanri na Angela Kairuki, wameshaanza kutajwa kuwa wanastahili kuwa mawaziri kamili.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, anatajwa kuwa miongoni mwa Manaibu Waziri wanaoweza kusalia kwenye Baraza la Mawaziri, kutokana na utendaji wake, lakini hawezi kupandishwa hadhi kutokana na makosa madogo aliyowahi kuyafanya, kama vile kushindwa kutofautisha nchi ya Zambia na kisiwa cha Zanzibar, hali iliyoonesha kuishushia hadhi Serikali ya Rais Kikwete, kwa kuwa na kiongozi asiyejua historia na jiografia ya nchi yake.
Utamaduni wa kupandisha manaibu waziri
Dhana ya manaibu waziri hao kupandishwa inatokana na hatua ya Rais Kikwete kuwahi kuwapandisha Dk. Nchimbi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Naibu Waziri wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Aidha Ezekiel Maige kabla ya kupandishwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alikuwa naibu waziri wa wizara hiyo, wakati huo ikiwa chini ya Shamsa Mwangunga.
Balozi Kagasheki kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alikuwa naibu waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mara baada ya Rais Kikwete kuingia madarakani, mwaka 2006 alimpandisha aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji na Mifugo wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Anthony Diallo, kuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.
William Ngeleja, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, alipandishwa hadhi na kuwa waziri kamili wa wizara hiyo, kabla ya kutemwa kwenye mabadiliko ya mawaziri yaliyofanyika Mei, mwaka 2013.
Aidha Waziri wa sasa wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, awali alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.
Dk. Cyril Chami, ambaye ameanza kupigiwa chapuo la kurejea kwenye baraza jipya, kabla ya kupandishwa hadi kuwa Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara na kutemwa mwaka 2012, alianzia kwenye unaibu waziri kwenye wizara hiyo.
Mawaziri wengine ambao walianzia kwenye nafasi ya unaibu waziri ni Celina Kombani, ambaye kabla ya kuwa waziri kamili wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), alikuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo, kabla ya kupewa nafasi hiyo alianzia kwenye nafasi ya Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Historia hiyo ya Rais kuwapa hadhi manaibu waziri kuwa mawaziri inatoa nafasi kwa manaibu wengi kuamini kuwa huenda wakapandishwa, hata hivyo hali ni tofauti kwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, ambaye amekosa bahati ya kupandishwa kuwa waziri kamili, ingawa ni mmoja wa manaibu waziri wa muda mrefu waliozunguka kwenye wizara mbalimbali.
Dk. Migiro na uwaziri
Kwa upande wake, Dk. Asha-Rose Migiro anapewa nafasi kubwa ya kuwemo kwenye Baraza la Mawaziri, kutokana na historia ya Rais Kikwete ya kutoa nafasi ya uwaziri kwa watu anaowateua kuwa wabunge, ambapo kwenye idadi ya wateule wake nane, tayari watano amewapa nafasi ya uwaziri.
Wabunge hao ni Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa akiongoza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Makame Mbarawa, anayeshikilia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Wateule wengine wa Rais kwenye ubunge ambao wameteuliwa kuwa mawaziri ni Profesa Sospeter Muhongo, anayeshikilia Wizara ya Nishati na Madini, Saada Mkuya na Janet Mbene, ambao ni manaibu waziri wa Wizara ya Fedha.
Wakati Dk. Migiro na wabunge wengine wakipewa nafasi ya kuwemo kwenye Baraza la Mawaziri, joto linabaki kwenye nani atakwenda wizara gani.
Wizara zinazoonekana kuwa ni mtihani kwa Rais Kikwete kumpa mtu sahihi ni Wizara ya Fedha, ambayo inashikiliwa na Dk. William Mgimwa, ambaye kwa sasa ni mgonjwa.
Hata hivyo, Dk. Abdallah Kigoda, anayeshikilia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa sasa, anatajwa kuweza kuimudu wizara hiyo, huku Zakia Meghji akitajwa kuwa na nafasi kubwa ya kurudi kwenye Baraza la Mawaziri, ili kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dk. Migoro anapewa nafasi ya kurejea kwenye wizara yake ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Bernad Membe, anayeshikilia wizara hiyo, akipewa nafasi ya kurudishwa Wizara ya Mambo ya Ndani, aliyoihudumia kwa kipindi kifupi akiwa naibu waziri wa wizara hiyo.
Uteuzi wa nafasi ya uwaziri kimikoa
Kama Rais Kikwete ataendeleza utaratibu wake wa kuchagua mawaziri kulingana na mikoa yao na kuamua kutomrejesha Nchimbi kwenye Baraza la Mawaziri, anaweza kuteua mmoja kati ya wabunge hawa, Mbunge wa Viti Maalumu, Mhandisi Stella Manyanya, Jenister Mhagama (Peramiho), Vita Kawawa (Namtumbo) au Mhandisi Ramo Makani (Tunduru Kaskazini) ili kujaza nafasi ya Nchimbi.
Endapo Kagasheki hatarejea, ni wazi turufu ya kuwemo kwenye Baraza la Mawaziri inaweza kumuangukia Jason Rweikiza (Bukoba Vijijini), Charles Mwijage (Muleba Kaskazini), Deogratius Ntukamazina (Ngara) au Asumpta Mshama (Nkenge).
Nafasi ya Dk. David Mathayo, huenda ikawa kaa la moto kwa Rais Kikwete kufanya maamuzi ya kumpata mtu sahihi, kwani idadi ya wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro ni ndogo na kwamba wengi wao wameshashikilia wizara, ukimuondoa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, ambaye wachambuzi wa masuala ya siasa hawampi nafasi sana ya kuingia kwenye Baraza la Mawaziri.
Kauli ya Ikulu
MTANZANIA Jumatano lilimtafuta Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga, ili kujua ukweli wa habari hizo, lakini alisema hajui chochote.
“Mimi niko Tanga, sijui kinachoendelea,” alisema Kibanga kwa kifupi, alipozungumza kwa simu na Mtanzania.
0 comments :
Chapisha Maoni