HALMASHAURI ya Busokelo katika Wilaya ya Rungwe na Shirika la nyumba (NHC) wameingia kwenye makubaliano ya msingi ya kujenga nyumba 14 kwa ajili ya watumishi wake.
Uamuzi wa kujenga nyumba hizo unalenga kuboresha utendaji na ufanisi wa halmashauri hiyo mpya iliyoanzishwa 2012, huku ikiwa inakabiliwa na tatizo kubwa la miundombinu, ikiwemo nyumba za watumishi.
Akizungumza na waandhishi wa habari Jijini Mbeya, ikiwa ni muda mfupi baada ya kumalizika kikao cha pamoja na watendaji wa shirika la nyumba, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Meckson Mwakipunda, alisema mpango huo wa ujenzi wa makazi ya watendaji ni sehemu ya miradi ya kipaombele katika halmashauri hiyo.
Mwenyekiti Mwakipunda alisema “Kipaumbele cha mkakati huu ni kwa halmashauri mpya 16 nchini, ambazo katika maeneo yao hakuna nyumba za kutosha , miongoni mwa halmashauri hizo katika mkoa wa Mbeya tumeanza na Halmashauri ya Busokelo”
“Kama mnavyojua Busokelo ni halmashuri mpya ambayo ilianza rasmi Oktoba 10 mwaka 2012, na upya huo inachangamoto nyingi hasa makazi ya watumishi na kwenye bajeti yetu ya kwanza ambayo ndio tunaendelea nayo tuliingiza hilo la kujenga nyumba lengo likiwa ni kuwajali wafanyakazi kwa kuwapa mazi bora ” .
Alisema halmashauri hiyo ilitenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya mradi wa kuboresha makazi, ambao umegawanyika katika awamu mbili, awamu ya kwanza ikiwa ni kujenga nyumba 14 za watumishi, huku awamu ya pili ikihusisha nyumba 36 kati ya 50 zitakazuhusisha miradi hiyo, ambapo baadhi ya nyumba hizo zitauzwa na kupangishwa kwa wananchi wa kawaida.
Alisema serikali kwa kutambua changamoto ilikubali kuthibitisha bajeti hizo na tayari fedha hizo zimeshaingizwa katika halmashauri hiyo na kilichobaki ni kukamisha hatua za kisheria kati yake na mkandarasi ambaye ni shirika la nyumba ambalo litahusika katika ujenzi huo.
Akizungumzia muda wa kuanza kwa mradi huo, Mwakipunda alisema kinachosubiliwa hivi sasa ni halmashauri hiyo kupata Baraka za Wizara ya Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi) ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuidhinisha vibali vya miradi ya aina hiyo.
|
0 comments :
Chapisha Maoni