Ijumaa, 29 Mei 2015

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Bwana Abas Kandoro akiongea kwenye mkutano wa RCC
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kyela Bwana Gabriel Kipija na wajumbe wengine wakifuatilia kwa makini mkutano wa RCC jijini Mbeya
KAMATI ya ushauri ya Mkoa wa Mbeya (RCC) imepitia na kupitisha mapendekezo ya Halmashauri za Mkoa huo ya kugawa majimbo na mengine kubadili majimbo ya uchaguzi. Jimbo la Kyela limekosa kigezo cha kugawanywa hivyo litaendelea kubaki jimbo moja kama ilivyokuwa awali likiungana na majimbo ya Ileje, Lupa,Songwe,Mbeya Mjini na Mbarali. Awali Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Kyela walipitisha kwa kauli moja mapendekezo ya Jimbo la Kyela kugawanywa na kuwa majimbo mawili yaani Kyela Mjini na Kyela Vijijini Jimbo la Kyela limeshindwa kukidhi sifa mbili ambazo ni Jiografia na Idadi ya watu Akifafanua katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa uliopo Sokomatola jijini Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bwana Abbas Kandoro alisema kikao hicho kimekubaliana na baadhi ya mapendekezo na mengine kuyakataa. Kandoro alisema mapendekezo hayo yamezingatia vigezo vilivyotolewa ambavyo ni idadi ya watu katika jimbo na hali ya Kijografia ambayo inamuwia vigumu Mbunge mmoja kuwafikia wananchi wake kwakati ikiwa ni pamoja na mawasiliano. Aliyataja majimbo waliyokubaliana kuyagawa kuwa ni pamoja na Jimbo la Mbozi Magharibi linalogawanywa kupata majimbo ya Momba na Tunduma, Mbozi Mashariki inakuwa na majimbo ya Vwawa na Mbozi. Kandoro alisema jimbo lingine lililopitishwa kugawanywa ni Jimbo la Mbeya vijijini linalokuwa na Jimbo la Santilya na Mbeya vijijini na kufafanua kuwa Jimbo hilo linakosa kigezo cha idadi ya watu lakini kutokana na hali ya Jografia na mawasiliano ni vigumu kuongozwa na Mbunge mmoja. Aliongeza kuwa Majimbo mengine yamebadilishwa majina kutokanana mapendekezo ya Halmashauri ambayo ni Jimbo la Rungwe Mashariki kuwa Jimbo la Busokelo na Jimbo la Rungwe Magharibi kuwa jimbo la Rungwe. Alisema Majimbo mengine yaliyopendekezwa na halmashari ni pamoja na Halmshauri ya Jiji la Mbeya lakini wazo lao limekataliwa kutokana na kukosa vigezo ambavyo ni kuwa na idadi ndogo ya watu, kuwa na mawasiliano mazuri na ukubwa wa eneo linalofikia kilomita za mraba 214. Aliongeza kuwa vigezo vingine vinavyoifanya Halmashauri ya jiji kushindwa kugawanywa ni kutokana na kutokuwa na changamoto nyingi zinazowakabili wananchi, muingiliano wa mamlaka kwa majimbo mawili kuwa chini ya Halmashauri moja.

0 comments :

Chapisha Maoni