Jumatano, 9 Oktoba 2013

JESHI LA POLISI kyela limezindua mradi wa Ulinzi Shirikishi katika tarafa ya Unyakyusa na Ntebela Wilayani hapa.
Shughuli nzima ya uzinduzi imefanyika katika ukumbi wa ofisi ya tarafa ya unyakyusa kyecu,ambapo mgeni rasmi OCD Ngassa amewataka watendaji kata kushirikiana na polisi kata ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi hasa katika swala zima la ulinzi wa amani.
Amesema kutakuwa na kikosi cha TAX-FORCE cha tarafa kitakachokuwa na askari wasiopungua ishirini ili kuleta nguvu ya pamoja kwa tarafa zote mbili kwa lengo la kuimarisha amani na usalama wa raia na mali zake kwakuwa usalama katika tarafa ni usalama wa wawilaya nzima.
Kamanda Ngasa ameomba kuwepo kwa ushirikianao kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii kwa maana ya vijana na wazee kupeana taarifa ili kufichua uovu unao weza kufanywa na kundi au mtu flani kutaka kuleta madhara,ameogeza kuwa swala la ulinzi si la polisi na serikali peke yake bali ni lakila raia wa Tanzania.
Aidha amezungumzia pia kuwepo na operesheni kubwa ya pombe haramu ya viroba kwa wilaya ya Kyela na Rungwe ,amewataka watendaji kata na vijiji kufanya operesheni ya waagizaji na wanywaji wa pombe haramu kuhakikisha wanakamtwa na kiisha kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikao hicho afisa tarafa ya unyakyusa Kheri William ametoa shukrani zake uongozi wa jeshi la polisi kyela kuzindua tax force ya tarafa kitu amabacho amesema kitaimaarisha zaidi usalama wa tarafa na wilaya kwa ujumla.

Jumamosi, 5 Oktoba 2013




WILAYA YA  MBEYA MJINI;  WATUHUMIWA  46  KATI YA  WATUHUMIWA 105       WALIOKAMATWA NA JESHI LA  POLISI MKOA  WA MBEYA KUTOKANA KWA  TUHUMA YA  KUFANYA  VURUGU NAUHARIBIFU WAMEFIKISHWA MAHAKAMANI JUZI TAREHE 03.10.2013.

  • MNAMO TAREHE 03.10.2013 WATUHUMIWA 46 KATI YA  WATUHUMIWA 105 WALIOKAMATWA MAENEO YA MWANJELWA,SOWETO,MAMA JOHN NA ILOMBA KWA TUHUMA ZA KUFANYA VURUGU WAMEFIKISHWA MAHAKAMANI LEO KUJIBU MASHTAKA YANAYOWAKABILI YA KUFANYA FUJO/VURUGU NA UHARIBIFU WA MALI- BARABARA.

  • AWALI MNAMO TAREHE 02.10.2013 MAJIRA KATI YA  SAA 09:00HRS  HADI SAA 17:47HRS HUKO KATIKA MAENEO YAMWANJELWA, SOWETO, MAMA JOHN NA ILOMBA KUNDI LA VIJANA WAKOROFI NA WASIO  TAYARI KUTII SHERIAWALISHINIKIZA WAFANYABIASHA KUFUNGA BIASHARA ZAO NA KISHA KUFUNGA BARABARA KUU YA MBEYA/IRINGA  NA BARABARA ZA MITAA KWA KUWEKA MAWE MAKUBWA,  MAGOGO, KUCHOMA MOTO MATAIRI NA KURUSHA OVYO MAWE KWA ASKARI POLISI HALI ILIYOSABABISHA USUMBUFU KWA WATUMIAJI WENGINE WA BARABARA NA WANANCHI WA JIJI LA MBEYA KWA UJUMLA.

  • KUFUATIA VURUGU HIZO JESHI LA POLISI KWA KUSHIRIKIANA NA BAADHI YA WANANCHI LILIKABILIANA NAZO NA KUFANIKIWA KUREJESHA HALI YA AMANI.

  • CHANZO CHA TUKIO HILI ILIKUWA NI WAHALIFU/WAFANYAFUJO KUTUMIA KIVULI CHA MALALAMIKO/MANUNG’UNIKO YA WAFANYABIASHARA KWENYE ENEO LA KODI HUSUSANI CHANGAMOTO KWA WAFANYABIASHARA WADOGO WADOGO KUWA BEI YA MASHINE YA KI-ELEKRONIKI NI GHALI  KIASI CHA TSH 800,000/= HIVYO WAO KUSHINDWA KUNUNUA.

  • HATA HIVYO KABLA YA VURUGU HIZO TAREHE 01.10.2013 WAFANYABIASHARA ZAIDI YA 300 WALIPATA FURSA YA KUKUTANA NA MKUU WA MKOA MHE ABBAS KANDORO WAKATI  WAFANYABIASHARA HAO WALIPOKUWA NA SEMINA ILIYOANDALIWA NA MAOFISA WA MAMLAKA YA MAPATO MKOA WA MBEYA. KATIKA KIKAO HICHO WALIMUELEZA MKUU WA MKOA MANUNG’UNIKO WALIYOKUWA NAYO IKIWA NI PAMOJA NA BEI YA MASHINE YA ELEKRONIKI INAYOFANYA KAZI YA KUTOA RISITI KWA WATEJA NA KUWEKA KUMBUKUMBU.

  • JUMLA YA WATUHUMIWA 105 WALIKAMATWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA MIONGONI MWAO WANAUME 103NA WANAWAKE 2 KWA MAHOJIANO KUHUSIANA NA TUKIO HILI. AIDHA TARATIBU ZA KISHERIA ZINAFANYWA KWA WATUHUMIWA WENGINE 59 WALIOKAMATWA KATIKA TUKIO HILO  IKIWA NI PAMOJA NA KUPEWA DHAMANA WAKATI UCHUNGUZI DHIDI YAO UKIENDELEA.

  • HAKUNA MADHARA MAKUBWA KWA BINADAMU AU MALI YALIYOTOKEA ISIPOKUWA UHARIBIFU WA KUCHOMA BARABARA.

  • KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA  KAMISHNA MSAIDIZI WA POLISI DIWANI ATHUMANI   ANAENDELEA KUTOA WITO  KWA  WANANCHI NA WAKAZI WA MBEYA KUTOICHEZEA AMANI ILIYOPO KWANI  GHARAMA YA KUIRUDISHA NI KUBWA. AIDHA ANATOA RAI KWA WAFANYABIASHARA KUENDELEA KUTAFUTA UFUMBUZI WA MATATIZO YAO KWA NJIA YA KUKAA MEZA YA MAZUNGUMZO KWA KUJENGA HOJA KWA MISINGI YA KUTII SHERIA ILI KUEPUSHA MATATIZO YANAYOWEZA KUEPUKIKA. PIA ANAENDELEA KUTOA RAI YA KUENDELEA KUWAFICHUA WAHALIFU WAKIWEMO WAFANYA FUJO, VURUGU NA KUKATAA KUWAUNGA MKONO KATIKA MAOVU.

      MBEYA VIJIJINI;     AJALI .MTEMBEA KWA MIGUU AGONGWA NA KUPOTEZA MAISHA

MNAMO TAREHE 02.10.2013 MAJIRA YA SAA 2:00 USIKU HUKO KATIKA KIJIJI CHA HATWELO BARABARA YA MBEYA/TUKUYU WILAYA YA MBEYA VIJIJINI MKOA WA MBEYA. GARI NA DEREVA ASIYEFAHAMIKA LILIACHA NJIA NA KUMGONGA MTEMBEA KWA MIGUU ASIYEFAHAMIKA JINA WALA MAKAZI YAKE JINSI YA KIUMEUMRI KATI YA MIAKA 37-40 NA KUSABABISHA KIFO CHAKE PAPO HAPO. MWILI WA MAREHEMU UMEHIFADHIWA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA. DEREVA ALIKIMBIA NA GARI MARA BAADA YA TUKIO. CHANZO NI MWENDO KASI. KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA  KAMISHNA WA POLISI DIWANI ATHUMANI  ANAENDELEA KUTOA WITO KWA MADEREVA KUWA MAKINI WANAPOENDESHA VYOMBO VYA MOTO KWA KUZINGATIA SHERIA NA ALAMA ZA USALAMA BARABARANI ILI KUEPUSHA AJALI ZINAZOWEZA KUEPUKIKA.  AIDHA ANATOA RAI KWA YEYOTE MWENYE TAARIFA JUU YA  MAHALI ALIPO MTUHUMIWA AZITOE KATIKA MAMLAKA HUSIKA ILI AKAMATWE NA SHERIA ICHUKUE MKONDO WAKE, VINGINEVYO AJISALIMISHE MWENYEWE.



                                                                        Signed by.
 [ DIWANI ATHUMANI  - ACP ]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Ijumaa, 4 Oktoba 2013



KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida kaburi ambalo alizikwa mtoto Shabani Maulidi (15), ambaye anadaiwa kufariki dunia miaka mitatu iliyopita na kuonekana akiwa hai hivi karibuni, jana lilifukuliwa na viungo vya mwili wake kukutwa ndani.
  
Kazi hiyo iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi pamoja na Mtafiti wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Lucas Ndungulu, ilizua taharuki kwa umati wa watu waliokuwa eneo hilo, baada ya nyumba ya jirani lilipo kaburi hilo, Masanja Marwa, kubomoka ghafla wakati ufukuaji huo ukiendelea, huku mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja naye akianguka na kuzirai.
  
Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.
  
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Ndungulu alisema kuwa wameamua kufukua kaburi hilo ili kupata sehemu ya viungo vya mwili kwa ajili ya vipimo.
  
“Lengo la kufukua kaburi hili ni kutaka tupate kiungo chochote cha mwili wa marehemu ili tufanye utafiti wa kitaalamu ili tujue kama ni kweli huyu anayedaiwa kuwa ni mtoto wao ndiye,” alisema.
  
Alisema kuwa ufukuaji huo umemalizika na kwamba wamepata baadhi ya viungo vya mwili wa marehemu na kuchukua baadhi ya mifupa ya mapaja yote mawili ambayo itapelekwa katika hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
  
Kwa mujibu wa Ndugulu, majibu ya vipimo hivyo yatatolewa baada ya wiki mbili kama hakutakuwa na tatizo lolote la kukatika kwa umeme.
  
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Adamu Sijaona, alisema kuwa pamoja na kuchukua viungo hivyo, pia watachukua damu ya wazazi na mtoto mwenyewe.
  
“Tumechukua pia damu ya mama na baba wa Maulidi mwenyewe ili tukapime vinasaba (DNA) na kama alivyosema mtafiti, majibu yatatoka baada ya wiki mbili,” alisema.
  
Akizungumza baada ya kazi ya ufukuaji kumalizika, baba mzazi wa mtoto huyo, Maulidi Shabani, alisema kuwa endapo majibu yatakuja tofauti au vile wanavyokusudia, wapo tayari kuyapokea na kwamba ikigundulika huyo aliyeonekana ni Maulidi, pia watampokea na kuendelea kumtunza.
  
“Lakini nina imani kuwa huyu aliyeonekana ni mwanangu Maulidi kabisa, kwa sababu anazo alama zote,” alisema mzazi huyo.
  
Mtoto Maulidi aliyefariki dunia miaka mitatu iliyopita na kufanyiwa matanga, alionekana akiwa hai baada ya kukutana na mama yake ana kwa ana mapema wiki hii asubuhi wakati akienda kwenye shughuli zake za biashara.

Ilidaiwa na wazazi wake kuwa Maulidi alitoweka ghafla na kushindwa kurudi nyumbani kwao Januari mosi 2011, wakati alipokuwa amewapeleka mbuzi malishoni na mwili wake kuonekana baada ya siku tatu akiwa amefia kwenye kisima cha maji.
  
Kwa mujibu wa baba yake, Maulidi hakurudi nyumbani siku hiyo, ambapo waliendelea kumtafuta bila mafanikio na ndipo baada ya siku tatu walimkuta akiwa amefia ndani ya kisima cha maji kilicho maeneo ya Kijiji cha Nyankumbu, Kitongoji cha Mwembeni.
  
Tukio hili ni la tatu kutokea mkoani hapa ambapo wilayani Kasamwa, mwanamke aliyefariki dunia miaka mitano iliyopita alionekana hai na kutambuliwa na ndugu yake. 

Tukio la pili lilitokea Wilaya ya Chato, wakati kijana aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita alionekana akiwa hai


KIKUNDI cha Al Shabaab kimetishia kumwaga damu zaidi Kenya kwa kufanya mashambulizi mapya na safari hii wanatamba kupiga patakapouma zaidi. Kundi hilo limesema kwamba litaongeza idadi ya watu katika kikosi cha mashambuzi nchini humo kutokana na Kenya kukaidi kuondoa majeshi yake Somalia.

Msemaji wa AL-shabaab

Tutaishambulia Kenya sehemu itakayowauma zaidi, tutageuza miji yao makaburi na mito ya damu itatiririka Nairobi nzima,” al Shabaab ilisema katika taarifa yake na kuongeza:
Uamuzi wa Serikali ya Kenya kuendelea kuyaacha majeshi yake Somalia ni ishara ya wazi kwamba, hawajataka kujifunza kutokana na yaliyotokea katika shambulizi la Westgate,” ilieleza taarifa hiyo huku ikijigamba kuwa, Kenya itakuwa eneo litakalogubikwa na wingu la damu na vurugu.
Wakati kikundi hicho kikitoa tishio hilo, takriban miili isiyopungua tisa imepatikana katika eneo la ndani ya kifusi kwenye jengo hilo, na sehemu ya eneo liliunguzwa kwa moto wakati wa shambulio hilo la Westgate.
“Baadhi ya miili haiwezi kutambuliwa kabisa na utambuzi wa vinasaba (DNA) utafanywa ili kutambua, mingine imeharibiwa na inatisha,” taarifa kutoka Polisi ilieleza.
Hata hivyo haikuwekwa wazi kama idadi ya miili hiyo tisa imejumlishwa na watu 67 wakiwemo wanajeshi sita waliokufa katika shambulizi hilo. Rais Kenyatta ajibu Hata hivyo Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, juzi alikaririwa akisema majeshi yake yataendelea kubaki Somalia hadi hapo amani na usalama wa nchi nchi hiyo vitakapotengamaa.
Septemba 21 Shambulio la Westgate lililotokea Septemba 21 mwaka huu katika jengo hilo la maduka ya bidhaa mbalimbali za watu wenye maisha ya juu, wanadiplomasia na wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya Kenya.
Mbali ya vifo hivyo vilivyofahamika hadi sasa, watu zaidi ya 170 walijeruhiwa vibaya huku wengine wakipata matatizo ya kisaikolojia. Miongoni mwa waliouawa ni watoto waliokuwa kwenye tamasha la mashindano ya kupika kwenye jengo hilo.
Baadhi ya manusura wa shambulio hilo walieleza namna walivyokutana uso kwa uso na magaidi hao. Kupitia taarifa mbalimbali, magaidi hao walisikika wakidai wanawasaka Wakenya na Wamarekani ingawa waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo ni pamoja na raia kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Ufaransa, Canada, Australia, Marekani, Uingereza, Ghana na kwingineko.
Pamoja na majeshi na polisi wa Kenya kuzingira jengo hilo tangu saa chache baada ya tukio, taarifa zinadai baadhi ya magaidi waliokuwa katika jengo hilo, walitoroka kupitia mtaro wa maji machafu uliokuwa chini ya jengo hilo na huenda watu wengi zaidi wakawa wamepoteza maisha ikiwemo mateka waliodaiwa kushikiliwa na magaidi hao ndani ya jengo hilo.
Shambulio hilo ni la pili kwa ukubwa nchini humo likihusisha kikundi cha al Shabaab chenye ushirika na al Qaeda ambao wanadaiwa kuhusika na shambulizi kubwa lililotokea mwaka 1998 katika Ubalozi wa Marekani nchini humo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 220.

CHANZO: HABARI LEO







Kwa muda wa siku mbili mfululizo, jumatano na alhamisi wiki hii, jiji la Mbeya lilitawaliwa na dhahma ya moshi na milio ya mabomu ya kutoa machozi sanjari na maji ya kuwasha, kufuatia kukosekana kwa maelewano baina ya mamlaka za kiserikali kwa upande mmoja, na wafanyibiashara kwa upande wa pili. Chanzo kikuu cha sintofahamu hii kilikuwa ni mashine za kuwekea kumbukumbu sahihi za mahesabu ya kibiashara na utoaji risiti kwa bidhaa zinazouzwa (EFDs).

Filamu hii isiyo ya kufurahisha, kilikuwa tangazo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kutangaza kuwa itakapofika novemba 15, kila mfanyibiashara atatakiwa kuhakikisha kuwa amefunga mashine hiyo katika duka au sehemu yake ya biashara. Agizo ambalo liliwalenga wale wote ambao mauzo yao ni zaidi ya shilingi za kitanzania alfu arobaini na tano (45,000/=). Nirejee tena kwa herufi kubwa kuwa agizo hili liliwalenga wafanyibiashara wote ambao MAUZO yao na sio FAIDA yao kwa siku, ni kiasi hicho.

Kutokana na hali hiyo, wafanyibiashara wengi wakaanza kuhoji juu ya hilo chini chini, na siku ya Jumanne, Mkuu wa Mkoa Bw. Abbass Kandoro, baada ya kusikia manung'uniko ya wananchi wake chini chini, akaamua kuwaita viongozi wa wafanyibiashara kuwasikiliza malalamiko hayo. Kikao baina ya pande hizi mbili, kilifanyika katika ukumbi wa Mtenda, maeneo ya Soweto.

Wafanyibiashara hao wakamueleza Mkuu wa Mkoa juu ya mambo kadhaa, kubwa zaidi likiwa ni gharama za mashine hizo, ambazo zinaelezwa kuwa zinauzwa kwa gharama ya kati ya shilingi laki saba hadi nane, ambapo walihoji, iweje mfanyibiashara mwenye mtaji wa milioni mbili kwa mfano alazimishwe kununua mashine ya laki nane?
Wakahoji faida za mashine hizo ikiwa zitawasaidia kuongeza biashara zao au laa, wakitolea mfano kuwa mtu anapolipia chumba, anajua kuwa atakuwa akitunza bidhaa zake kwa kuziuza na kutengeneza faida, sasa je, mashine hizo zitawasaidia kimapato kwa namna gani? Zitawasaidia kuongeza faida kwa namna gani? Wapo ambao waliitaka serikali kama inataka kweli wao wazitumie mashine hizo, basi iwanunulie na wao hawatisita kuzitumia.

Taarifa ambazo nimezipata toka katika kinywa cha Mkuu wa Mkoa mwenyewe ni kuwa, aliyachukua malalamiko yao, kuwaahidi kuwa atayawasilisha mahali husika, na angewaita tena ili kuwajulisha nini kimetoka huko juu, na aliwaomba wafanye biashara zao kama kawaida.

Taarifa za upande wa wafanyibiashara zinaeleza kuwa, baada ya mkutano huo na RC, viongozi wa chama cha wafanyibiashara, waliona ni vyema basi wakawajulisha wenzao juu ya kilichoongelewa huko ambapo walienda wakakodi gari la matangazo, wakalipia katika mamlaka husika na kuzunguka wakitangaza mjini kuhusu uwepo wa mkutano wa wafanyibiashara katika viwanja vya Ruanda Nzovwe, maarufu pia kama CCM Ilomba, lengo likiwa kujadili suala la EFDs na kupeana mrejeshonyuma wa kikao na Mkuu wa Mkoa.

Hadi hapo kila kitu kilikaa shwari hadi pale ilipotimu siku ya jumatano asubuhi, ambapo baadhi ya wafanyibiashara walianza kukusanyika katika eneo ambako mkutano ungefanyika. Lakini wakati wakiendelea kukusanyika, ghafla gari za doria zikaanza kuonekana maeneo ya Mwanjelwa na Kabwe hadi huko Ruanda Nzovwe na kilichofuatia hapo, ndio kile ambacho kimesharipotiwa mara nyingi. Ilikuwa ni mwendo wa mabomu na machozi, maji ya kuwasha, fukuzana za kila kona, virungu kwa waliokamatwa na kila aina ya mvurugano unayoweza kuieleza.

Zaidi kuhusu tukio hili, unaweza kusoma kwa kubonyeza http://www.jukwaahuru.com/vurugu-jijini-mbeya-mkuu-wa-mkoa-aongea-na-jukwaa-huru-na-kuzielezea-a-z/ , na baada ya kujikumbusha yote haya, hebu tutafakari kwa pamoja kuwa je, tatizo hasa lilikuwa ni mashine, Polisi, TRA, wafanyibiashara au nani hasa?

Tukumbuke tu kuwa, tukio la Mbeya mjini, lilikuja ikiwa ni chini ya wiki moja toka mgomo wa wauza ndizi katika wilaya ya Tukuyu kuanza. Mgomo huo nao ulisababishwa na wao kupinga kuingezewa kodi katika mikungu ya ndizi ambapo mkungu mmoja ambao awali ulikuwa unaweza kuununua kwa shilingi 2500 utatakiwa ulipiwe ushuru wa shilingi 1000.

Nionavyo mimi, tatizo haliko kwenye EFDs au kiwango cha kodi ambacho kinapendekezwa kutozwa. Wala hakiko katika utunzaji wa kumbukumbu za kibiashara ili kurahisisha watu wa TRA kufanya makusanyo stahiki ya kodi. Kwa mtazamo wangu, tatizo ni "mbona viongozi na watengaji wakubwa katika mamlaka mbalimbali hususan serikalini, hawana mashine za kutunzia kumbukumbu za ahadi zao kwa wananchi?"
Ndio, ikiwa viongozi wangekuwa na mashine za kutunzia kumbukumbu za ahadi zao kwa wananchi, na kisha kukawepo na mashine (sheria) za kuwawezesha wananchi kutumia kumbukumbu hizo kuwawajibisha viongozi hao, basi hakungekuwa na malalamiko ya EFDs kwa wafanyibiashara leo hii.

Tatizo linakuja kuwa, walalahoi hawa au waganga njaa hawa, wanalazimishwa kuhakikisha wanakuwa na mashine za kutunzia kumbukumbu kwa minajili ya kuziwezesha mamlaka kuzidi kuwakamua kodi, ambazo baadae hawaoni kama zinawanufaisha kwa kiwango cha kutosha.
Muuza ndizi sokoni, analipa ushuru kila siku katika soko, analipa kodi kedekede tangia anapozinunua huko mashambani, kuzisafirisha hadi kuzipanga, lakini mahali anapoziuza, mifereji ni michafu na ili isafishwe ni lazima alipie mchango. Akitaka kwenda kujisaidia, anatakiwa kulipia pia huduma hiyo ya kwenda haja, taka zikizidi sokoni anatakiwa alipie ili zikakusanywe na kwenda kutupwa. Huyu mnapotaka kumuongezea ushuru, mnamtaka nini kama sio ubaya?

Hebu waangalie wale wafanyibiashara pale Mbeya. Analipia kodi ya pango, anapoenda kujisajili kupata namba ya mlipa kodi, anatakiwa apeleke mkataba wa upangaji sehemu yake ya biashara, na anatakiwa alipie kodi kile kiasi anachomlipa mwenye nyumba, na wala sio mwenye nyumba anayelipwa ndio alipie kipato hicho. Analipa ushuru wa eneo analofanya biashara kila siku, analipia kodi bidhaa anapozinunua, analipa kodi anapozisafirisha, analipa kodi anapozipanga tu dukani kwake. Huyu mnapotaka anunue mashine inamsaidia kwa lipi hapo?

Hivi sasa biashara nyingi sana zimekuwa zikienda kombo, ikielezwa kuwa serikali licha ya kupitisha bajeti, haijaingiza hela kwenye mzunguko, na ndio maana kwa mfano serikali hiyo inadaiwa karibu na kila aliyekuwa akiipa huduma. Hawa watu watoe wapi laki nane za kununua EFDs?

Lakini mtu huyu huyu akiumwa anajilipia matibabu, mtaa anaokaa barabara ni mbovu kupita maelezo, hakuna mitaro ya maji ya kueleweka, hakuna mifumo mizuri ya utoaji wa maji machafu. Akiumwa akienda hospitali, analazimika kwenda kununua dawa, akiumwa mwanae ndio hivyo hivyo, akiumwa baba, mama au ndugu yake yeyote hali ni hivyo hivyo. Hizi kodi za awali anazolipa zinakwenda wapi? Akinunua mashine, itamsaidia vipi kukuza biashara yake zaidi ya kuweka kumbukumbu za kuwawezesha TRA kuzidi kumkamua kodi zaidi?

Nionavyo mimi, tatizo kubwa ni kutokuwepo kwa uwiano wa kodi ambazo tayari zinakusanywa hivi sasa, na upatikanaji wa huduma katika maisha halisi. Mafanikio mengi yamekuwa kwenye hotuba ya waziri wa fedha anapowasilisha bajeti na sio katika eehemu ambazo walipa kodi wenyewe wanaishi, na hili ndio tatizo kubwa.
Ikumbukwe kuwa, mfanyibiashara ni ndugu wa mwananchi wa kawaida na mfanyakazi. Na kwamba kama huyu mwananchi wa kawaida angekuwa anaziona kodi zake na za mfanyibiashara zimemletea matunda, hakika angesimama mstari wa mbele kumshurutisha ndugu yake huyo kununua mashine kwa maslahi zaidi ya wananchi. Mfanyakazi naye pia angefanya hivyo hivyo, na mwisho wa siku, wafanyibiashara wangezinunua na kuzifanyia kazi.
Inapotokea kuwa mfanyibiashara anapogoma anaungwa mkono na kundi kubwa la walio kando ya biashara zenyewe, inamaanisha kuwa hata hawa wasio wafanyibiashara wanaona kabisa kuwa ndugu zao wanaonewa. Na bahati mbaya sana ni kuwa, mifano ya namna hii ipo haijasahaulika. Simulizi la zile mashine za kudhibiti mwendo, ziliishia wapi kama sio ajali kuzidi kuua ndugu zetu hadi leo hii? Magari yalifungiwa hadi kila moja likawa na kidhibiti mwendo, lakini leo tuko wapi?
nionavyo mimi, Watanzania tayari wanalipakodi nyingi mno, na kuwaambia eti wawe na mashine za kutunzia kumbukumbu za biashara zao, ambayo kimsingi inamaanisha mashine ya kumbukumbu za wanavyokamuliwa kodi na kubakia watupu, ni kuwataka ubaya zaidi. Kwanza viongozi watuonyeshe mashine za kutunzia kumbukumbu za ahadi zao, kisha mashine zinazowawezesha wananchi kuchukua hatua kama hawaridhishwi na utekelezaji wa ahadi walizoahidiwa awali, ndipo wafanyibiashara nao washurutishwe kumiliki mashine za EFDs.

Kama hatuwezi kuuona kwanza uwiano wa kiuhalisia wakodo ambazo tayari zinakusanywa na maendeleo ambayo tuliahidiwa, basi tutarajie kuwa hili la EFDs litakuwa moja ya mambo yatayoleta migogoro zaodo katika zama hizi ambapo wakubwa wanalazimisha kuwa zinunuliwe na wafanyibiashara.

Kama viongozi hawaoni umuhimu wa wao kuwa na mashine za kutunza kumbukumbu za ahadi zao, na kama hawaoni umuhimu wa kuktengenezea mwananchi mashine (sheria) ya kuweza kuchukua hatua dhidi ya kiongozi ambaye anamletea mambo ya kipuuzi na majibu ya ajabu ajabu pindi anapomhpomhoji, basi sioni umuhimu wa waganga njaa hawa kulazimishwa kumiliki mashine za kutunza kumbukumbu za hesabu za biashara zao. Haziwaongezei chochote katika ufanisi wa biashara zao wala ubora wa huduma za msingi.
--
Ramadhani Msangi
Founder & CEO - Jukwaa Huru Media
P. O. Box 693, Mbeya - Tanzania

Alhamisi, 3 Oktoba 2013



Vurugu kubwa zimetokea hapa jijini Mbeya ambapo wafanyabiashara katika soko la Mwanjelwa wameigomea mamlaka ya mapato Tanzania(TRA) mkoani hapa wakidai inawashinikiza wananchi hao kununua vifaa vya Electronic Fiscal Devices(EFD) maalum kwa kuhakikisha mamlaka hiyo inarahisisha ukusanyaji wa kodi kirahisi na kwa umakini zaidi.
Wafanyabiashara hao wameilalamikia mamlaka hiyo kuwa inawashinikiza kutumia kifaa hicho wakati uwezo wa mitaji yao ni mdogo sana.Waliedelea kulalamika kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikiwashinikiza kuwa kila mfanyabiashara mwenye mtaji usiopungua shilin gi za kitanzania elfu arobaini na tano(Tshs 45000) analazimika kutumia kifaa hicho katika kutoa risiti kwa uuzaji wa bidhaa zake ambapo kifaa hicho kinapatikana kwa shilingi zisizopungua laki nane .
Hata hivyo Kyela Nyumbani inaendelea na jitihada za kuwatafuta wanaohusika kujibu malalamikao hayo ya wananchi yaliyopelekea kutokea kwa vurugu hizo kubwa jijini hapa na kuathiri uchumi wa nchi kwa ujumla.  
 
 Baadhi ya watu wakiwa wanakimbia Baada ya Mabomu ya machozi kuanza kurushwa kuepusha vurugu
 Mawe yakiwa yamepangwa kuzuia magari yasiende kokote

 Maduka yote yakiwa yamefungwa eneo la mwanjelwa kupinga ununuzi wa mashine hizo za TRA
 Vijana hawa wakiwa wananawa uso baada ya Bomu la machozi kuwapitia 
 Jiwe kubwa likiwa limewekwa katika Barabara magari yasipite

Wafanya Biashara wakiwa wanajiandaa kusikiliza mkutano 

Mpaka sasa hivi tunapo toa ripoti hizi za moja kwa moja kutoka Jijini Mbeya  kutokana na vurugu kubwa iliyozuka kwa wafanya biashara kugomea mashine za TRA, Sasa wafanya biashara hao wamerejea makwao ingawa kulikuwa na vugu vugu la Vijana vibaka kuleta vurugu lakini  Jeshi la polisi limeweza kuwadhibiti wote na hali sasa imekuwa tulivu... Ingawa kulikuwa na Minong'ono kutoka kwa watu mbalimbali wakiomba hali hii kesho iwe shwari na kusiwe na vurugu tena..

Jumanne, 1 Oktoba 2013





 Juu na chini, Dr. Mary Mwanjelwa akipandisha bendera katika tawi hilo la Mwanjelwa ambako mashabiki wa timu ya Mbeya City, walimwalika kuwa mgeni rasmi.

 Viongozi wa Jiji la Mbeya wakishangilia ilipokuwa ikipanda bendera....
 Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza, akizungumza katika hafla hiyo fupi ya uzinduzi wa tawi la wakereketwa wa timu ya Mbeya City.
 Kulia ni Mwenyekiti wa mashabiki wa Mbeya City FC, Willy Mastala, akifurahia baada ya kukabidhiwa fedha taslmi Tsh. 500,000 na Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa.



 Mbeya City hoyeeeeee..hoyeeeeee...hoyeeeee
 Mashabiki wa tawi la Mbeya City wakiwa pamoja katika hafla hiyo...
 Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga, akielea protocal za kiuongozi, jambo ambalo vijana walionekana kutomwelewa huku wakipiga kelele za kutofurahia, baadae wakamshangilia baada ya kusema kuwa Jiji litawasafirisha mashabiki kuelekea Arusha tmu hiyo itakapoenda kucheza huko...
 Mbunge Dr. Mary Mwanjelwa akiwa ndani ya uzi wa MBEYA CITY






MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Mbeya, Dr. Mary Mwanjelwa, amewachangia Sh. 500,000 mashabiki wa timu ya Mbeya City, walioamua kujiunga na kufungua tawi lao katikati ya Jiji la Mbeya.
Pesa hizo alizikabidhi juzi kwa mashabiki hao ambao walimwalika kuwa mgeni rasmi wa kufungua tawi la mashabiki wa timu hiyo kutoka eneo la Mwanjelwa na Kabwe.
Dr. Mwanjelwa alisema kuwa, timu ya Mbeya City imewauganisha na kutaka tawi hilo, liwe chachu ya umoja na mshikamano kwasababu huwezi kuzungumza Mbeya bila kutaja Mwanjelwa.
Mwenyekiti wa mashabiki hao, Willy Mastala, alisema tayari tawi lao lina akiba ya Sh. 450,000 na mashabiki hao wamejipanga kusafiri na kushangilia timu hiyo popote itakapoenda na gharama zote waliomba ziwe juu ya Jiji la Mbeya.
Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga, alisema kuwa Jiji lake litasafirisha mashabiki wote na bajeti ya timu hiyo tayari ipo na kwamba amefurahi kusikia kuwa Mbunge Mwanjelwa atakuwa mlezi wa tawi hilo.
Mkurugenzi wa Jiji hilo Mussa Zungiza, alisema kuwa anajisikia furaha kuona mashabiki wanaendelea kuunga mkono jitihada za Jiji lake kuimarisha timu ya Mbeya City.