Ijumaa, 4 Oktoba 2013








Kwa muda wa siku mbili mfululizo, jumatano na alhamisi wiki hii, jiji la Mbeya lilitawaliwa na dhahma ya moshi na milio ya mabomu ya kutoa machozi sanjari na maji ya kuwasha, kufuatia kukosekana kwa maelewano baina ya mamlaka za kiserikali kwa upande mmoja, na wafanyibiashara kwa upande wa pili. Chanzo kikuu cha sintofahamu hii kilikuwa ni mashine za kuwekea kumbukumbu sahihi za mahesabu ya kibiashara na utoaji risiti kwa bidhaa zinazouzwa (EFDs).

Filamu hii isiyo ya kufurahisha, kilikuwa tangazo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kutangaza kuwa itakapofika novemba 15, kila mfanyibiashara atatakiwa kuhakikisha kuwa amefunga mashine hiyo katika duka au sehemu yake ya biashara. Agizo ambalo liliwalenga wale wote ambao mauzo yao ni zaidi ya shilingi za kitanzania alfu arobaini na tano (45,000/=). Nirejee tena kwa herufi kubwa kuwa agizo hili liliwalenga wafanyibiashara wote ambao MAUZO yao na sio FAIDA yao kwa siku, ni kiasi hicho.

Kutokana na hali hiyo, wafanyibiashara wengi wakaanza kuhoji juu ya hilo chini chini, na siku ya Jumanne, Mkuu wa Mkoa Bw. Abbass Kandoro, baada ya kusikia manung'uniko ya wananchi wake chini chini, akaamua kuwaita viongozi wa wafanyibiashara kuwasikiliza malalamiko hayo. Kikao baina ya pande hizi mbili, kilifanyika katika ukumbi wa Mtenda, maeneo ya Soweto.

Wafanyibiashara hao wakamueleza Mkuu wa Mkoa juu ya mambo kadhaa, kubwa zaidi likiwa ni gharama za mashine hizo, ambazo zinaelezwa kuwa zinauzwa kwa gharama ya kati ya shilingi laki saba hadi nane, ambapo walihoji, iweje mfanyibiashara mwenye mtaji wa milioni mbili kwa mfano alazimishwe kununua mashine ya laki nane?
Wakahoji faida za mashine hizo ikiwa zitawasaidia kuongeza biashara zao au laa, wakitolea mfano kuwa mtu anapolipia chumba, anajua kuwa atakuwa akitunza bidhaa zake kwa kuziuza na kutengeneza faida, sasa je, mashine hizo zitawasaidia kimapato kwa namna gani? Zitawasaidia kuongeza faida kwa namna gani? Wapo ambao waliitaka serikali kama inataka kweli wao wazitumie mashine hizo, basi iwanunulie na wao hawatisita kuzitumia.

Taarifa ambazo nimezipata toka katika kinywa cha Mkuu wa Mkoa mwenyewe ni kuwa, aliyachukua malalamiko yao, kuwaahidi kuwa atayawasilisha mahali husika, na angewaita tena ili kuwajulisha nini kimetoka huko juu, na aliwaomba wafanye biashara zao kama kawaida.

Taarifa za upande wa wafanyibiashara zinaeleza kuwa, baada ya mkutano huo na RC, viongozi wa chama cha wafanyibiashara, waliona ni vyema basi wakawajulisha wenzao juu ya kilichoongelewa huko ambapo walienda wakakodi gari la matangazo, wakalipia katika mamlaka husika na kuzunguka wakitangaza mjini kuhusu uwepo wa mkutano wa wafanyibiashara katika viwanja vya Ruanda Nzovwe, maarufu pia kama CCM Ilomba, lengo likiwa kujadili suala la EFDs na kupeana mrejeshonyuma wa kikao na Mkuu wa Mkoa.

Hadi hapo kila kitu kilikaa shwari hadi pale ilipotimu siku ya jumatano asubuhi, ambapo baadhi ya wafanyibiashara walianza kukusanyika katika eneo ambako mkutano ungefanyika. Lakini wakati wakiendelea kukusanyika, ghafla gari za doria zikaanza kuonekana maeneo ya Mwanjelwa na Kabwe hadi huko Ruanda Nzovwe na kilichofuatia hapo, ndio kile ambacho kimesharipotiwa mara nyingi. Ilikuwa ni mwendo wa mabomu na machozi, maji ya kuwasha, fukuzana za kila kona, virungu kwa waliokamatwa na kila aina ya mvurugano unayoweza kuieleza.

Zaidi kuhusu tukio hili, unaweza kusoma kwa kubonyeza http://www.jukwaahuru.com/vurugu-jijini-mbeya-mkuu-wa-mkoa-aongea-na-jukwaa-huru-na-kuzielezea-a-z/ , na baada ya kujikumbusha yote haya, hebu tutafakari kwa pamoja kuwa je, tatizo hasa lilikuwa ni mashine, Polisi, TRA, wafanyibiashara au nani hasa?

Tukumbuke tu kuwa, tukio la Mbeya mjini, lilikuja ikiwa ni chini ya wiki moja toka mgomo wa wauza ndizi katika wilaya ya Tukuyu kuanza. Mgomo huo nao ulisababishwa na wao kupinga kuingezewa kodi katika mikungu ya ndizi ambapo mkungu mmoja ambao awali ulikuwa unaweza kuununua kwa shilingi 2500 utatakiwa ulipiwe ushuru wa shilingi 1000.

Nionavyo mimi, tatizo haliko kwenye EFDs au kiwango cha kodi ambacho kinapendekezwa kutozwa. Wala hakiko katika utunzaji wa kumbukumbu za kibiashara ili kurahisisha watu wa TRA kufanya makusanyo stahiki ya kodi. Kwa mtazamo wangu, tatizo ni "mbona viongozi na watengaji wakubwa katika mamlaka mbalimbali hususan serikalini, hawana mashine za kutunzia kumbukumbu za ahadi zao kwa wananchi?"
Ndio, ikiwa viongozi wangekuwa na mashine za kutunzia kumbukumbu za ahadi zao kwa wananchi, na kisha kukawepo na mashine (sheria) za kuwawezesha wananchi kutumia kumbukumbu hizo kuwawajibisha viongozi hao, basi hakungekuwa na malalamiko ya EFDs kwa wafanyibiashara leo hii.

Tatizo linakuja kuwa, walalahoi hawa au waganga njaa hawa, wanalazimishwa kuhakikisha wanakuwa na mashine za kutunzia kumbukumbu kwa minajili ya kuziwezesha mamlaka kuzidi kuwakamua kodi, ambazo baadae hawaoni kama zinawanufaisha kwa kiwango cha kutosha.
Muuza ndizi sokoni, analipa ushuru kila siku katika soko, analipa kodi kedekede tangia anapozinunua huko mashambani, kuzisafirisha hadi kuzipanga, lakini mahali anapoziuza, mifereji ni michafu na ili isafishwe ni lazima alipie mchango. Akitaka kwenda kujisaidia, anatakiwa kulipia pia huduma hiyo ya kwenda haja, taka zikizidi sokoni anatakiwa alipie ili zikakusanywe na kwenda kutupwa. Huyu mnapotaka kumuongezea ushuru, mnamtaka nini kama sio ubaya?

Hebu waangalie wale wafanyibiashara pale Mbeya. Analipia kodi ya pango, anapoenda kujisajili kupata namba ya mlipa kodi, anatakiwa apeleke mkataba wa upangaji sehemu yake ya biashara, na anatakiwa alipie kodi kile kiasi anachomlipa mwenye nyumba, na wala sio mwenye nyumba anayelipwa ndio alipie kipato hicho. Analipa ushuru wa eneo analofanya biashara kila siku, analipia kodi bidhaa anapozinunua, analipa kodi anapozisafirisha, analipa kodi anapozipanga tu dukani kwake. Huyu mnapotaka anunue mashine inamsaidia kwa lipi hapo?

Hivi sasa biashara nyingi sana zimekuwa zikienda kombo, ikielezwa kuwa serikali licha ya kupitisha bajeti, haijaingiza hela kwenye mzunguko, na ndio maana kwa mfano serikali hiyo inadaiwa karibu na kila aliyekuwa akiipa huduma. Hawa watu watoe wapi laki nane za kununua EFDs?

Lakini mtu huyu huyu akiumwa anajilipia matibabu, mtaa anaokaa barabara ni mbovu kupita maelezo, hakuna mitaro ya maji ya kueleweka, hakuna mifumo mizuri ya utoaji wa maji machafu. Akiumwa akienda hospitali, analazimika kwenda kununua dawa, akiumwa mwanae ndio hivyo hivyo, akiumwa baba, mama au ndugu yake yeyote hali ni hivyo hivyo. Hizi kodi za awali anazolipa zinakwenda wapi? Akinunua mashine, itamsaidia vipi kukuza biashara yake zaidi ya kuweka kumbukumbu za kuwawezesha TRA kuzidi kumkamua kodi zaidi?

Nionavyo mimi, tatizo kubwa ni kutokuwepo kwa uwiano wa kodi ambazo tayari zinakusanywa hivi sasa, na upatikanaji wa huduma katika maisha halisi. Mafanikio mengi yamekuwa kwenye hotuba ya waziri wa fedha anapowasilisha bajeti na sio katika eehemu ambazo walipa kodi wenyewe wanaishi, na hili ndio tatizo kubwa.
Ikumbukwe kuwa, mfanyibiashara ni ndugu wa mwananchi wa kawaida na mfanyakazi. Na kwamba kama huyu mwananchi wa kawaida angekuwa anaziona kodi zake na za mfanyibiashara zimemletea matunda, hakika angesimama mstari wa mbele kumshurutisha ndugu yake huyo kununua mashine kwa maslahi zaidi ya wananchi. Mfanyakazi naye pia angefanya hivyo hivyo, na mwisho wa siku, wafanyibiashara wangezinunua na kuzifanyia kazi.
Inapotokea kuwa mfanyibiashara anapogoma anaungwa mkono na kundi kubwa la walio kando ya biashara zenyewe, inamaanisha kuwa hata hawa wasio wafanyibiashara wanaona kabisa kuwa ndugu zao wanaonewa. Na bahati mbaya sana ni kuwa, mifano ya namna hii ipo haijasahaulika. Simulizi la zile mashine za kudhibiti mwendo, ziliishia wapi kama sio ajali kuzidi kuua ndugu zetu hadi leo hii? Magari yalifungiwa hadi kila moja likawa na kidhibiti mwendo, lakini leo tuko wapi?
nionavyo mimi, Watanzania tayari wanalipakodi nyingi mno, na kuwaambia eti wawe na mashine za kutunzia kumbukumbu za biashara zao, ambayo kimsingi inamaanisha mashine ya kumbukumbu za wanavyokamuliwa kodi na kubakia watupu, ni kuwataka ubaya zaidi. Kwanza viongozi watuonyeshe mashine za kutunzia kumbukumbu za ahadi zao, kisha mashine zinazowawezesha wananchi kuchukua hatua kama hawaridhishwi na utekelezaji wa ahadi walizoahidiwa awali, ndipo wafanyibiashara nao washurutishwe kumiliki mashine za EFDs.

Kama hatuwezi kuuona kwanza uwiano wa kiuhalisia wakodo ambazo tayari zinakusanywa na maendeleo ambayo tuliahidiwa, basi tutarajie kuwa hili la EFDs litakuwa moja ya mambo yatayoleta migogoro zaodo katika zama hizi ambapo wakubwa wanalazimisha kuwa zinunuliwe na wafanyibiashara.

Kama viongozi hawaoni umuhimu wa wao kuwa na mashine za kutunza kumbukumbu za ahadi zao, na kama hawaoni umuhimu wa kuktengenezea mwananchi mashine (sheria) ya kuweza kuchukua hatua dhidi ya kiongozi ambaye anamletea mambo ya kipuuzi na majibu ya ajabu ajabu pindi anapomhpomhoji, basi sioni umuhimu wa waganga njaa hawa kulazimishwa kumiliki mashine za kutunza kumbukumbu za hesabu za biashara zao. Haziwaongezei chochote katika ufanisi wa biashara zao wala ubora wa huduma za msingi.
--
Ramadhani Msangi
Founder & CEO - Jukwaa Huru Media
P. O. Box 693, Mbeya - Tanzania

0 comments :

Chapisha Maoni