Jumatano, 11 Juni 2014


Binti aliyepata mateso kwa kung’atwa na kuchomwa kwa pasi na mwajili wake, Yusta Lucas (Kushoto) akiwa na mama yake, Modesta Simoni katika hospitali ya Mwananyamala juzi Dar es Salaam.
Hatimaye Yusta Lucas (20), binti anayedaiwa kuteswa kwa kung’atwa na mwajiri wake, Amina Maige ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Mwananyamala alikokuwa amelazwa na kukabidhiwa kwa wanaharakati wa Taasisi ya Jipange. Hatua hiyo ilifikiwa baada ya maridhiano kati ya Ustawi wa Jamii, mama mzazi wa Yusta, Modesta Simon, Kamati ya Ulinzi na Usalama Kata ya Makumbusho na Jipange ambao ndiyo iliyofanikisha kumwokoa binti huyo. Akizungumza jana, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makumbusho, Husna Nondo alisema baada ya kutafakari kwa kina juu ya usalama na urahisi wa kupatikana pale atakapohitajika, wamekubaliana binti huyo akae kwa muda kwa mmoja wa wanakikundi kutoka taasisi hiyo. “Tumeafikiana Yusta aendelee kubaki mikononi mwa wanaharakati ili iwe rahisi kupatikana atakapohitajika mahakamani, maana yeye ndiye shahidi wa kwanza. Mama na mjomba wake waliotoka Tabora wataendelea kukaa Upanga walikofikia,” alisema Nondo. Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Mwananyamala, Rose Temu alisema wamemkabidhi Yusta kwa Jipange kwa maandishi na wanaamini yuko katika mikono salama kwa sababu taasisi hiyo ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele kumuokoa. “Wakati akisubiri kesi yake, tumekubaliana awe chini ya Jipange tumeona asiendelee kukaa wodini kwan anaweza kupata ugonjwa mwingine, uamuzi ambao hata mama yake ameuridhia.”
Mwenyekiti wa Jipange, Janet Mawinza alisema wamekubali kumpokea Yusta kwa ajili ya usalama wake lakini akasema hataeleza ni wapi atakuwa anaishi kwa kipindi atakachokuwa akisubiri kesi. “Sisi tumempokea kama kikundi na tunachoomba ni vyombo vinavyohusika na suala hili kuhakikisha vinashughulikia suala lake kwa wakati ili huyu binti aungane na familia yake Tabora,” alisema. Mama wa binti huyo alisema anaamini binti yake yuko katika mikono salama. “Hawa Jipange ndiyo walikuwa naye tangu siku ya kwanza na sioni kama kuna tatizo wao kuendelea kuwa naye.” TUJIKUMBUSHE
Kwa siku tano, Yusta alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala kuuguza majeraha yanayodaiwa kusababishwa na kung’atwa na kuchomwa na pasi na Maige ambaye alikuwa mwajiri wake huko Mwananyamala Kwa Manjunju kwa muda wa miaka mitatu. Mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi katika Kituo cha Oysterbay na wakati wowote atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
Yusta alikumbwa na masaibu hayo kwa muda mrefu hadi hivi karibuni majirani wakiwa na polisi walipovamia nyumba hiyo na kumkamata bosi wake kisha kumpeleka Kituo cha Polisi cha Oysteraby, Dar ambako anashikiliwa na yeye kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibu baada ya kukutwa na majeraha. Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Camillius Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa ametiwa mbaroni.
Yusta alielezea mwenendo wa mwajiri wake ambao sio wa kawaida KUHUSU MAISHA YA TAJIRI WAKE Aidha, Yusta alianika mienendo mitano ya bosi wake huyo na kusema imekuwa ikimshangaza sana.
MWENENDO WA KWANZA “Mimi katika kuishi kwangu pale sijawahi kumwona jirani yeyote amekuja ndani kusalimia wala yeye kwenda kwa jirani kufanya hivyo jambo ambalo si la kawaida.”
MWENENDO WA PILI “Yeye (bosi wake) hana mume. Lakini tangu nimeishi pale kwa miaka mitatu sijawahi kumwona mwanaume ameingia ndani ya nyumba achilia mbali wanawake wenzake, hata mgeni. Kifupi yeye ni yeye kwa pale nyumbani kama ana marafiki labda wanakutana mbali.”
MWENENDO WA TATU
“Muda wake wa kurudi nyumbani siku zote ni usiku mnene, amewahi sana ni saa mbili usiku. Kwa hiyo, muda mwingi mimi ndiyo huwa nyumbani.”
MWENENDO WA NNE
“Anajiweza, sijui kwa nini aliamua kunifanyia hivi. Maana mtu ana gari, anaendesha mwenyewe na anasema ana hela, ndiyo maana namshangaa kuniadhibu kwa kuning’ata kwa meno.”
MWENENDO WA TANO
“Sikumbuki lini nimewahi kumwona akicheka. Muda mwingi anaonekana amekasirika tu kiasi kwamba nimekuwa nikimwogopa siku zote.”
OMBI KWA SERIKALI
Yusta alisema kufuatia matatizo makubwa yaliyompata ameiomba serikali imsaidie aweze kurudi nyumbani kwao Tabora.
SHUKURANI KWA MAJIRANI
Yusta alitoa shukurani kwa majirani waliojitokeza kuokoa maisha yake ambapo alisema kama wasingekuwa wao hajui ingekuwaje.
MANENO YA MUUGUZI
Kwa upande wa hospitali hiyo, muuguzi kiongozi wa zamu siku hiyo, Mahija Swalehe alikemea tabia za waajiri wa wafanyakazi wa ndani kuwatesa na kuiomba serikali kuliangalia suala hilo kwa jicho la tatu ili kukomesha vitendo hivyo

0 comments :

Chapisha Maoni