Jumatano, 4 Juni 2014

Mama wa watoto mapacha Eliud na Elikana, Grace Joel akiwa amempakata mtoto Eliud ambaye kwa sasa anasumbulia na tatizo la kutokwa na utumbo.
Picha na Godfrey Kahango: Mwananchi
Mmoja wa watoto pacha waliozaliwa wakiwa wameungana na kutenganishwa kwa upasuaji nchini India, hali yake ni mbaya na utumbo wake mkubwa sasa umetoka nje. Mtoto huyo Eliud Mwakyusa na mwenzake Elikana walizaliwa Februari 20, 2013, Kyela, Mbeya wakiwa wameungana kiunoni na Serikali iliwapeleka India ambako walitenganishwa. Walirejea Februari, mwaka huu na kusherehekea siku yao ya kuzaliwa wakiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili walikofikia baada ya kutoka India katika hafla iliyoandaliwa na gazeti hili. Hata hivyo, siku chache baada ya watoto hao kurejea kijijini kwao Kasumulu maarufu kwa jina la Juakali, Kyela, afya ya Eliud ilianza kubadilika baada ya sehemu kubwa ya utumbo wake mpana kuanza kutokeza nje. Utumbo wa mtoto huyo umetoka nje kupitia tundu lililoachwa na madaktari jirani na kitovu chake kwa ajili ya kutolea haja kubwa. Wakizungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki nyumbani kwao, wazazi wa watoto hao, Grace Joel na Eric Mwakyusa walisema tatizo la Eliud lilianza mwezi mmoja uliopita. Grace alisema hali hiyo imesababisha mwanaye aanze kudhoofika naye akiwa hajui cha kufanya kutokana na hospitali iliyowafanyia upasuaji kuwa mbali. Alisema baada ya kutenganishwa walitengenezewa mirija maalumu ya kutolea haja. “...Waliingiza kwa ndani na kubakiza kidogo nje ya tumbo kwa ajili ya kutolea haja kubwa. Hivyo baada ya kuanza kuugua akawa anatapika na anapotapika utumbo huu ukawa unatoka nje kidogokidogo kama unavyoona,” alisema huku akionyesha utumbo huo. Alisema kuwa hali hiyo ya utumbo kutoka nje iliwahi kumtokea mtoto huyo hata wakiwa bado hospitalini nchini India, lakini haikuleta madhara yoyote. Mama huyo alisema afya ya Eliud imekuwa ikidhoofu kila kukicha na sasa imefikia hatua anashindwa kukaa peke yake tofauti na aliporejea kutoka India. Mwenzake aendelea vizuri Afya ya pacha mwenzake, Elikana ni nzuri na muda mwingi amekuwa akikaa na bibi yake mzaa baba, Subira Kasekele. Akizungumzia afya za wajukuu zake Kasekele alisema: “Watoto walinenepa kweli kipindi fulani na wakawa na afya njema, tatizo lipo tu kwa huyu mwingine (Eliud) kwani lilipoanza kujitokeza tatizo hili na afya yake ikaanza kutetereka.” Alisema huwa anashinda na mtoto huyo na kumrudisha kwa mama yake wakati wa kunyonya. Chakula wanachokula watoto Grace alisema licha ya kupewa masharti ya chakula kwa ajili ya watoto hao, hali ya maisha imewafanya wakiuke masharti kwani sasa wanakula chochote kinachopatikana. Baba wa watoto hao, Eric Mwakyusa anasema watoto wake wanaishi kwa kudura za Mwenyezi Mungu kwani wanakula chakula cha kawaida kutokana kipato chake duni. “Tulishauriwa watoto wale vyakula mchanganyiko ili kuwajengea afya njema, lakini uchumi wangu mbaya sina kitu hivyo wanalazimika kula kile tunachokipata kwa siku hiyo,” alisema. Alisema hivi sasa anaendesha pikipiki ya mtu ambayo anaitumia kwa kusafirisha abiria kwa sharti la kupeleka hesabu ya Sh8,000 kwa siku. “Unaweza kuona wakati mwingine ninapata Sh10,000 wakati mwingine 15,000 na siku nyingine biashara hakuna na hapohapo natakiwa kupeleka kwa bosi Sh8,000 ambayo natakiwa kuigawa nyumbani kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine. “Wakati mwingine siwezi kufanya kazi, nahitajika kumpeleka mtoto hospitali au kumwangalia wakati mama yao anafanya kazi nyingine... Bibi yao ana mtoto mwingine, basi yote tumeyapokea kwa kuwa Mungu ndiye mpaji,” anasema Mwakyusa. Wazazi washukuru Wakizungumza kwa hisia, Grace na Eric waliishukuru Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ambayo kupitia magazeti yake, Mwananchi na The Citizen yaliandikwa hali ya watoto hao na kuwafanya watu mbalimbali kuwasaidia. “Kwa mfano, mwenye pikipiki ninayoendesha alisoma kwenye Gazeti la Mwananchi ndipo aliponiita na kunikabidhi niendeshe walau nipate fedha kidogo,’’ alisema Eric na kuongeza kuwa kuna msamaria mwema ambaye ameahidi kumpatia pikipiki ili fedha zote atakazokuwa akipata zisaidie kuendesha maisha ya familia hususan watoto wake, lakini bado hajatimiza na anaamini akiwa tayari atamwambia. Grace licha ya kuwashukuru watu mbalimbali wanaoendelea kuwajulia hali watoto wao lakini akadokeza kwamba familia yake inahofia kwamba huenda isipate nauli ya kwenda Dar es Salaam na hatimaye India kwa ajili ya matibabu ya pili. Safari hiyo imepangwa kufanyika Julai, mwaka huu.
Credit :MWANANCHI
br>

0 comments :

Chapisha Maoni