Jumanne, 3 Septemba 2013


JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeleezea namna mwanajeshi wake, Meja Khatibu Shaaban Mshindo, alivyouawa baada ya kuangukiwa na bomu, wakati akiwa katika jukumu la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
 
Pamoja na hayo, Watanzania wametakiwa kuimarisha mshikamano na kuachana na makundi yenye nia ya kuleta mgawanyiko, hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho Tanzania imepoteza askari wake waliopewa dhamana ya kitaifa ya ulinzi wa amani katika nchi zenye migogoro Afrika.
 
Akitoa salamu za rambirambi wakati askari huyo wa kikosi cha Mizinga namba 83 KJ kilichopo Kibaha akiagwa rasmi kijeshi Dar es Salaam jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamnyange, alisema askari huyo pamoja na askari watano wa Tanzania, waliangukiwa na bomu hilo na kujeruhiwa vibaya.
 
“Waliangukiwa na bomu Agosti 28, mwaka huu huko Goma DRC eneo walilokuwa wakifanyia kazi… Meja Mshindo aliumia vibaya na kukutwa na mauti njiani akipelekwa hospitalini,” alisema Jenerali Mwamunyange.
 
Alisema katika tukio hilo, askari wengine watano wa Tanzania walijeruhiwa vibaya na wanaendelea vizuri na matibabu nchini humo na hali zao zinaendelea vizuri.
 
Akimzungumzia Meja Mshindo, Jenerali Mwamunyange alisema katika uhai wake alikuwa mchapakazi, muaminifu, hodari na mtiifu na kifo chake kimetokea wakati jeshi linamhitaji.
 
“Kifo chake kimeacha pengo ndani ya JWTZ na itachukua muda mrefu kuziba pengo hili.” Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema kifo cha askari huyo ni msiba wa kitaifa na kumtaja Meja Mshindo kuwa shujaa aliyekutwa na mauti wakati akitekeleza kazi aliyotumwa na nchi yake.
 
Alisema kifo hicho pamoja na vifo vya askari wengine saba wa JWTZ vilivyotokea Darfur mwaka huu, ni chachu kwa Tanzania kuendeleza jitihada za kusaidia nchi zenye migogoro na kuhamasisha amani Afrika.
 
“Serikali inapata matumaini namna Watanzania walivyosimama pamoja na kuunga mkono jeshi letu katika kipindi hiki kigumu. Ingekuwa nchi nyingine, haya yaliyotokea yangeleta mgawanyiko mkubwa miongoni mwa raia, lakini kwa hapa kwetu hali imekuwa tofauti,” alisema Membe.
 
Aliwataka wachache wenye mawazo ya kutumia matukio hayo kuwagawa Watanzania, waache mara moja nia yao hiyo, kwa kuwa moja ya kazi ambayo Tanzania inayo, ni pamoja na nia yake ya kuhamasisha na kutangaza amani Afrika na dunia kwa ujumla.
 
“Jamani wajibu wetu ni kuhakikisha haya maeneo yenye migogoro yanakuwa na amani, kule DRC hali ni mbaya, watu wanakufa kila kukicha na akinamama na watoto wanabakwa na kudhalilishwa, sasa sisi kama taifa ni vyema kujitokeza na kusaidia wenzetu,” alisisitiza.
 
Meja mshindo, alizikwa jana nyumbani kwao Fujoni Zanzibar na ameacha mke mmoja, Hawa Mnimbo na watoto watatu ambao ni Shaaban, Abuu na Samir Mshindo

0 comments :

Chapisha Maoni