Alhamisi, 26 Septemba 2013




MKAGUZI na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini madudu katika matumizi na mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Kutokana na upungufu huo, CAG amewataka madiwani kuchukua hatua ili waliosababisha ufujaji huo wa fedha wachukuliwe hatua za kisheria.

Upungufu huo upo katika baadhi ya miradi ya maendeleo chini ya mfuko wa LGCDG yenye thamani ya sh 326,208,530 ambayo haikukamilika na fedha hazionekani.

Mradi mwingine ni ule ulio chini ya mfuko wa MMAM, wenye thamani ya sh 218, 349, 260 ambao nao haukukamilika na fedha hazionekani.

CAG aliitaja miradi mingine kuwa ni madawa yenye thamani ya sh 9,867,005 yaliyoharibika, lakini hayakufutwa na kuondolewa kwenye vitabu, mradi wa thamani ya sh 208,140,250 wa mfuko wa ASDP uliokamilika, lakini hautumiki kana kwamba fedha zilizotumika ziliokotwa, pamoja na mradi wa barabara yenye thamani ya sh 181,146,200 ambao haujakamilika na fedha zilizotengwa hazionekani.

Pamoja na upungufu huo wa msingi, mkaguzi katika taarifa yake alibaini hoja zilizojadiliwa na kufungwa katika mwaka 2011/2012 ni 37 kati ya 79 wakati 42 hazijafungwa. Zitakaguliwa na kujadiliwa tena mwaka 2012/2013.

Aidha, katika kikao cha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango cha kupitia hoja za CAG kilichofanyika katika ukumbi wa Community Center Julai 22, 2013 na Baraza la Madiwani lililofanyika Septemba 4, 2013, baada ya kubainika kuwepo na upungufu kadhaa wakuu wa idara na madiwani walipewa ushauri kuufanyia kazi.

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alitoa ushauri kwa watendaji na wataalamu ambao aliwataka wazingatie kanuni, taratibu, miongozo na sheria za fedha na manunuzi ya umma, na pia aliwataka wataalamu hao kutoa ushirikiano kwa wakaguzi wa ndani na nje pindi wanapokuja kukagua ili kuleta ufanisi katika kutekeleza shughuli zao.

Aliendelea kuwataka wataalamu kusimamia matumizi ya sheria ndogo ndogo za kuzuia magonjwa ya mifugo ambayo inawataka wafugaji kutumia kikamilifu majosho kwa kuogesha mifugo yao, na kuwa aliwataka wataalamu kuandaa sera na mpango kwa ajili ya kuzuia majanga na hasara kwa wahanga (Risk and Fraund Assessment Policy) ikiwamo mpango wa kuhakikisha dawa, vifaa tiba, vitendanishi na vifaa chakavu vilivyokwisha muda wa matumizi vinateketezwa.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka madiwani na watendaji kushirikiana katika kufanya shughuli za wananchi kupitia halmashauri ya wilaya kwa kuwa tayari imepata hati ya shaka kutokana na utendaji mbaya na kwamba wasipokuwa makini kuna uwezekano wa kupata hati chafu.

Wananchi kwa upande wao waliokuwepo katika kikao hicho kilichokaliwa siku za hivi karibuni walishangazwa na taarifa hizo za ubadhirifu uliofanywa katika halmashauri hiyo na kupata wasiwasi juu ya uwezo duni wa madiwani wao ambao mbali na kupewa ushauri na mkuu wa mkoa wameshindwa kuchukua hatua kwa watendaji waliokwamisha shughuli za maendeleo.
Imeandaliwa na Ibrahim Yassin (Kyela)

0 comments :

Chapisha Maoni