Jumatano, 4 Septemba 2013

Wadau wa maendeleo ya elimu nchini wakimsikiliza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa alipokuwa akizindua mpango mkakati wa kuinua sekta ya elimu ujulikanao kama Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Dar es Salaam 

Dar es Salaam. Wakati Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi jana ikizindua Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu, wadau wa elimu na maofisa elimu wa mikoa wameutilia shaka utekelezaji wake kwa mwaka huu kwamba hautafikia kiwango kilichokusua.
Mpango huo uliozinduliwa jana, utekelezaji wake ulianza Aprili mwaka huu na moja ya utekelezaji wake ni kuhakikisha kuwa matokeo ya wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani wa darasa la saba wiki tatu zijazo, kidato cha nne miezi miwili ijayo yanakuwa mazuri, jambo ambalo limepingwa na wadau hao.
Mara baada ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru kuzindua mpango huo, Wakurugenzi wa taasisi mbalimbali za elimu za Serikali pamoja na maofisa elimu wa mikoa yote nchini walikula kiapo cha kuhakikisha kuwa wanasimamia mpango huo kikamilifu.
Wakati wakiapa, wengi walikuwa wakisema kuwa watajitahidi, kujituma ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya haraka yanapatikana na kukwepa kutamka wazi kuwa mpango huo utafanikiwa, jambo ambalo liliwafanya mamia ya watu waliohudhuria uzinduzi huo kuwashangilia.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema ni ndoto kwa wanafunzi kufanya vyema katika mitihani yao ya darasa la saba, kidato cha nne katika muda uliobaki.
Akizindua mpango, Dk Kawambwa alisema kuwa utekelezaji wake ulishaanza tangu mwezi Aprili na kwamba anatarajia matokeo ya haraka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Amandina Lihamba alisema Serikali imekuwa na mipango mingi mizuri mno, lakini tatizo liko kwenye utekelezaji. Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzani (Tamongsco), Mak Mringo alisema kuwa kiapo walicholishwa wakurugenzi wa elimu katika uzinduzi huo hautekelezeki kwa kuwa mpango huo uko kinadharia zaidi.
Kuhusu motisha kwa walimu ambayo ni mkakati wa mpango huo, Mringo alisema kuwa Serikali inazo fedha za kumaliza madai ya walimu, ila hakuna mfumo mzuri wa kuhakiki madeni hayo.
Naye Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijiji, Donald Wilson alisema mkakati huo hautaleta matokeo mazuri kwa mwaka huu.
Naye Kada wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Mutamwega Mugaywa ambaye pia ni mdau wa elimu, japo aliusifu mpango huo alisema umechelewa.
Ofisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Mayasa Ali Hashim alisema kwa mwaka huu haitawezekana kwa mpango huo kutekelezeka kwa maelezo kuwa muda uliobaki kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha nne kufanya mitihani yao ya mwisho, ni mfupi.
                       Na Elias Msuya na Fidelis Butahe

0 comments :

Chapisha Maoni