Jumapili, 8 Septemba 2013

KITENDO cha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukataa kumpa nafasi Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kuwaamuru askari kumtoa kwa nguvu, lakini pia kiongozi huyo kugoma kutii amri ya kiti, na hivyo kuzua vurugu bungeni kimeibua hisia na maoni tofauti kutoka kwa wachambuzi mbalimbali.


Baadhi ya wachambuzi wa sayansi ya kisiasa pamoja na wafuatiliaji wa mambo, wamezungumzia tukio hilo kuwa linajengwa na sura mbili ya ukaidi na udhaifu wa kiti cha Spika.

Ni kwa namna hiyo wamemtaja Ndugai moja kwa moja kuwa pengine anaponzwa na ujasiri alionao lakini pia kushindwa kwake kutumia busara wakati wa kufanya maamuzi ya kiti.

Wakati Ndugai akishutumiwa kwa namna hiyo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe naye amenyooshewa kidole lakini kwa sura tofauti na ile ya Ndugai.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache, baada ya vurugu kubwa pengine kuliko zote zilizowahi kutokea bungeni, ambazo chanzo chake ni pale Mbowe aliposimama na Ndugai kushindwa kumpa nafasi ya kuzungumza alichotaka kusema badala yake akamuamuru kukaa chini kabla hajawaita askari kumtoa.


Ikiwa ni mwendelezo wa vurugu zilizowahi kutokea bungeni siku za nyuma, wachambuzi hao wameanza kupata shaka na hata kuanza kuhoji ni kwanini matatizo mengi yanapotokea bungeni chanzo chake huwa ni kiti ambacho wakati huo huwa kimekaliwa na Ndugai.

Wanaoliona hilo wanamzungumzia Ndugai kwamba huenda anaponzwa na ujasiri wake wa kiti kuliko kutumia busara.

Wanahoji alikoupata ujasiri Ndugai wakati ambapo Tanzania inafuata mfumo wa Kibunge wa Jumuiya ya Madola unaotoa fursa sawa kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Waziri Mkuu.

Wakati haya yakitokea sasa, wachambuzi hao wameanza kuupima utendaji wa Ndugai kwa namna ya kuangalia idadi ya matukio ambayo yamekuwa yakivuruga mwenendo wa Bunge wakati yeye akiwa amekalia kiti.

Katika hilo, itakumbukwa kuwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), aliwahi kufukuzwa bungeni na Ndugai baada ya kutamka kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu.

Mbali na hilo, Mei 30 mwaka huu, Ndugai alilazimika kuahirisha Bunge mara mbili na kusitisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya wabunge wa CUF, kumchachamalia Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema), ambaye alisema msimamo wa kiliberali wanaoufuata CUF unashabikia ushoga na usagaji.

Ni kwa mwenendo huo wa utendaji wa Ndugai, Mwanasheria maarufu nchini, Majura Magafu, ameeleza kushangazwa na mwenendo wa Naibu Spika huyo huku akihoji kuwapo kwa mlolongo wa mizozo inayoibuka ndani ya Bunge wakati anapoongoza vikao.

“Huwa najiuliza maswali mengi, ni kwanini kila wakati Ndugai akiwa kwenye kiti kunatokea mzozo? Hapa ni dhahiri kuwa kuna udhaifu mkubwa na hata kwa kiti kizima cha spika, wameshindwa kuendesha Bunge na hata wabunge wenyewe hawajiheshimu,”alisema.

Alieleza kuwa siku zote hakuna aliye juu ya sheria, hivyo kitendo cha Mbowe kukaidi amri ya Naibu spika nayo ni kukiuka sheria.

“Wabunge watambue kuwa Bunge ni sehemu inayoheshimika na inastahili ipewe heshima. Pia watambue kuwa Bunge haliongozwi kama klabu ya pombe bali kuna kanuni na sheria.

Mbunge na Spika wanapokiuka kanuni wanakuwa hawawatendei haki Watanzania na hawajatumwa bungeni kwenda kutukanana na kupigana bali kutatua matatizo ya wananchi,” alisema Magafu.

Kwa upande wake, Mwanasheria, Peter Kibatala, alisema Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, hadhi yake ni sawa na Waziri Mkuu, hivyo hata kama amekosea hatakiwi kuamriwa kama wabunge wengine, bali kiti cha spika kinatakiwa kitumie staha.

Kuna namna ya ‘kum-handle’ Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni tofauti na wabunge wengine. Ndugai alitakiwa kutumia busara ya kipekee si kama alivyofanya na ndiyo maana yakatokea yote yale,”alisema Kibatala.


Mwanasheria nguli nchini, Masumbuko Lamwai, alisema ni dhahiri kwamba Ndugai si kiongozi kwa kuwa kila fujo inapotokea bungeni yeye anakuwa kwenye kiti.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ni tofauti na wabunge wengine mfano angesimama Waziri Mkuu wangemwambia akae chini?,”alihoji Lamwai.

Alipoulizwa na gazeti hili endapo ni sahihi kwa kitendo cha Mbowe kukaidi amri ya Naibu Spika, alisema suala lililokuwa linazungumzwa lilikuwa kubwa hivyo alitakiwa kusikilizwa.

Ndugai aachie ile nafasi haimfai na waliomchagua hawakuchagua kiongozi. Ile issue ilikuwa hot hivyo alitakiwa kutumia busara na uongozi wakati mwingine ni busara si sheria,”alisema Lamwai.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ali, alisema kilichotokea bungeni ni kawaida na inaweza kutokea hata nje ya Bunge kwa kuwa watu hawataki kufikia muafaka wa namna ya kupata Katiba.

Tunatakiwa tuangalie chanzo na si kilichotokea bungeni na tunaweza kushuhudia vurugu kama zile hata nje ya Bunge. Waliofanya vile ni wale wenye wasiwasi kuhusu mchakato wa Katiba kutokana na mwenendo wake,”alisema Bashiru Ali.

Naye Mwanasheria Mabere Marando alisema Kiongozi wa Kambi ya Upinzani anaposimama bungeni hata kama kuna mbunge anazungumza anatakiwa asikilizwe kama alivyo kwa Waziri Mkuu.

Source: Mtanzania.

0 comments :

Chapisha Maoni