Jumatano, 16 Septemba 2015


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, leo imempa siku 14 Mwanasheria Mkuu wa Serikali kueleza kama anamaelezo yoyote au pingamizi juu ya kesi iliyofunguliwa na jopo la mawakili 7 wanaopinga baadhi ya vipengele vya Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015 iliyoanza kutumika Septemba 1, 2015 wakati haijafanyiwa marekebisho yaliyowasilishwa na wadau mbalimbali katika mamlaka husika.
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wakati upande wa utetezi uliongozwa na wakili Benedict Ishabakaki. Kesi hiyo ya kikatiba ilikuwa imepangwa kupangiwa majaji leo Septemba 15, 2015.
Kesi hiyo itasikilizwa na majaji watatu chini ya Mwenyekiti wake Prof. Jaji John Ruhangisa, Jaji Lugano Mwandamo na Jaji Winfrida Korosso.
Mahakama imempa AG siku 14 awe amewasilisha kwa maandishi maelezo kama anapingamizi lolote juu ya kesi hiyo ya kikatiba au awe amejibu malalamishi ya mlalamishi ambaye ni wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole.
Mara baada ya AG kuwasilisha maelezo yake, walalamishi watapewa siku saba au kabla ya Oktoba 7, 2015 wawe wanejibu mambo ambayo yatakuwa wameainishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Keshi hiyo inasimamiwa na jopo la mawakili saba (7) wa kujitegemea na kesi hiyo itatajwa Oktoba 22, 2015.
Akizungumza mara baada ya kutajwa kwa keshi hiyo wakili Kambole, amekarriwa akisema kitendo cha serikali kupuuza maoni ya wadau wa habari na haki za binadamu juu ya baadhi ya vipengele vya sheria hiyo ni mwendelezo wa ukandamizaji wa kuzuia kuwapa uhuru wananchi kujieleza pamoja na sekta ya habari nchini.
Mawakili hao wanaiomba Mahakama kutengua baadhi ya vifungu vya sheria hiyo ikiwemo kifungu cha 4,5, na 45 (4) cha sheria ya makosa ya mitandao amabcho kinazuia haki ya kutafuta, kupata na kutoa taarifa na hivyo kukinzana na ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania
Kifungu cha 6,7,8,10,11,14,19,21 na 22 vya Sheria hiyo ambavyo vinaelezwa kuwa na maneno yasiyo na tafsiri na hivyo kuhofiwa kuwa vinaweza kupekeleka taafsiri mbaya kwa watekeleza sheria na hivyo kupelekea uvunjifu wa haki za binadamu na kukiuka ibara ya 17 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vipengele vingine kifungu cha 31,33,34,35 na 37 vya sheria hiyo vinatoa maamlaka kwa Polisi kufanya upekuzi na kuchukua kompyuta bila idhini ya mahakama hivyo kukinzana na ibara ya 16 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Na kifungu 38 cha sheria hiyo kinachonyima haki ya mtu kusikilizwa na mahakama hivyo kupingana na ibara ya 13(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Baadhi ya mawakili katika kesi hiyo ni pamoja na Harold Sungusia, Flugence Massawe, Jeremiah Mtobesya, Benedict Alex, Boka Melkisedeckm Neema Ndemno na Jebra Kambole.

0 comments :

Chapisha Maoni