Jumatatu, 26 Agosti 2013

WAVUVI katika kambi zilizopo kijijini Senga kata ya Kamsamba wilayani Momba wamejeruhiwa kwa kupigwa fimbo kabla ya vibanda vyao kuchomwa moto na wakazi wa kijiji cha Ilambo, Kata ya Kapeta wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athumani, tukio hilo lilitokea juzi saa 6:00 mchana katika kambi za wavuvi hao huku chanzo kikitajwa kuwa mgogoro wa kugombea mipaka ya vijiji.
Kamanda Athumani aliwataja wavuvi sita waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Msabaha Juma (40), Maximo Mwakanyemba (24), Michael Sanga (30), Chonde Kalisto (56), Zawadi Sichula (39) na Gibson Kachingwe (26) maarufu kama Msagala wote wakazi wa kijiji cha Senga ambao wamepata matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Alisema kutokana na tukio hilo wakazi saba wa kijiji cha Ilambo wanashikiliwa kwa tuhuma za kujeruhi na kuharibu mali huku wengine wakiendelea kusakwa.
Aliwataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo kuwa ni Samwel Daudi (42), Gervas Lukas (52), Nyerere Mwita (52), Richard Wilson (43),Gebrus Ramadhani (28), Lulinde Dase (43), Funguza Masanja (43) na taratibu zinafanyika ili wafikishwe mahakamani.

0 comments :

Chapisha Maoni