Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Kyela , Nuhu Mwafilango
ameelezea jinsi alivyopigwa nondo alipokuwa akiendesha ibada na kudai
kuwa zilikuwa njama za muda mrefu za kundi la Waislamu wanaharakati
wanaoipinga Bakwata na aliyempiga alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu.
Katika Ibada ya Sikukuu ya Idd, saa 2.15 asubuhi
iliingia dosari baada ya kuzuka vurugu kubwa katikati ya ibada hiyo
kutokana na muumini mmoja kuinuka ghafla kwenye msikiti mkuu wa Wilaya
ya Kyela na kumshambulia Sheikh huyo na watu wengine watatu kujeruhiwa.
Akizungumzia tukio hilo Sheikh Mwafilango mwenye
umri wa miaka (76) alisema kuwa vurugu hizo zilitokea katikati ya ibada
alipokuwa akiongoza swala na baada ya kumaliza takbira saba.
“Baada ya kuanza kusujudu kwenye ardhi ndipo
ghafla nikaanza kupigwa na fimbo mgongoni na ndipo nilipotoa kauli ya
kuwaeleza waumini wenzangu kuwa nimevamiwa na nilipopata nafasi ya
kuinuka nikapigwa na kitu kama nondo eneo la goti kwenye mguu wa kushoto
na mkononi,” alisema.
Alisema kuwa hali ilikuwa ni mbaya katika msikiti huo kwani vurugu zilikuwa kubwa.
“Kumbe yule kijana aliyenipiga mimi hakuwa peke
yake bali alikuwa na kundi la watu wengi ambao walikuwa wameshika silaha
mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkasi, kisu na nondo,” alisema.
Aidha sheikh huyo alisema mbali ya tukio hilo pia
Agosti 2, mwaka huu alivamiwa katikati ya ibada ya Ijumaa na mmoja wa
watu waliohusika katika tukio hilo na kumnyang’anya kipaza sauti na
kumtaka aache kuongoza ibada hiyo.
“Aliyenivamia siku ya ibada ya Ijumaa alikuwapo
kwenye tukio hilo la juzi na siku hiyo alichokifanya alitaka mimi
niondoke na akamwita kijana mdogo kuwa ndiye aendelee kuongoza ibada
hiyo kitu ambacho waumini waliokuwapo walizuia na kuniruhusu kuendelea
kuongoza ibada,” alisema.
Alisema baada ya kuvamiwa alitoa taarifa kwa Mkuu
wa Wilaya ya Kyela na baadaye kwa mkuu wa polisi wa wilaya ambapo alitoa
taarifa ya maandishi ya kwamba alivamiwa alipokuwa akiswalisha.
0 comments :
Chapisha Maoni