BAADA ya manung'uniko  makubwa ya wadau wa soka wa Tanzania hatimaye Shirikisho la soka kupitia kwa Rais wake Jamali Malinzi wiki hii alimteua kocha Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ akichukua nafasi ya Mholanzi Mart Nooij aliyetimuliwa kazi kufuatia matokeo mabaya ya timu hiyo.
Mkwasa amepewa nafasi hiyo na kusaidiwa na Hemed Morocco ambaye ni kocha wa timu yataifa ya Zanzibar mwenye sifa kubwa ya kufundisha timu na kutoa upinzani hasa kwa mataifa makubwa.
Kwa mujibu wa TFF, makocha hawa watakuwa wakilipwa mishahara yao kama vile walivyokuwa wakilipwa makocha kutoka nje ya Tanzania kama Mart Nooij na wengineo walio tangulia.
Wadau wengi wa soka wamefuraishwa na uteuzi huo wakiami Mkwasa ndiye mtu sahihi atakayeweza kurudisha matumaini ya Watanzania angalau kutinga kwenye fainaliza mataifa ya Afrika zitakazo fanyika Gabon mwaka 2017 licha ya kufungwa na Misri 3-0.
Watanzania wanaimani na Mkwasa kutokana na kuamini uzalendo atakao kuwa nao kwa taifa lake la Tanzania lakini pia ni kocha ambaye nalijua vizuri soka pamoja na mazingira wanayoishi wachezaji wa Tanzania.
Nandiyo maana muda mchache baada ya kutambulishwa aliwataka Watanzania kuweka silaha chini na kurudisha umoja wa kuisapoti timu yao ya taifa ili iweze kuwa rahisi kwake kufanya kile ambacho wananchi wanakitaka.
Mara baada ya kutangazwa Mkwasa mbali na kutaja watu wake wa benchi la ufundi pamoja na kikosi cha wachezaji 26 lakini alisisitiza wadau na mashabiki kuungana na kuachana na ushabiki wa Simba na Yanga ili kubadili matokeo ya timu hiyo pamoja na kurudisha amani kwa timu hiyo.
Mkwasa alisema pamoja na kuwa na leseni A, aliyo kabidhiwa na CAF na kutambulika na Shirikisho la soka duniani FIFA, lakini siyo malaika wa kuweza kubadili matokeo ya timu hiyo haraja na kikubwa anahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau na mashabiki ili kufanikisha hilo.
KWA WASIO MJUA CHARLES BONIFACE MKWASA
Kwa wasiomjua Mkwasa ni mmoja wa makocha wa watatu wa Tanzania kumiliki Leseni A mwanzoni mwa miaka ya nyuma kabla ya Rais wa sasa wa Shirikisho la soka Tanzania Jamali Malinzi kuingia madarakani na kuongeza idadi hiyo na kufikia 24 hivi sasa.
Mkwasa aliyewahi kufanya vizuri wakati akiwa mchezaji akiwa na klabu ya Yanga ambayo kwa sasa anaifundisha kama kocha msaidizi na timu ya taifa amepitia nafasi mbalimbali ikiwemo kufanya kazi ndani ya shiriki hilo siku za nyuma.
Mkwasa alikuwa ni mmoja ya wachezaji waliokuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars kilicho shiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 huko Lagos Nigeria akiwa kama mchezaji chipukizi wakati huo akiwa mchezaji wa Yanga.
Baada ya hapo Mkwasa aliendelea kujishuhulisha na mashala ya soka na kupitia kozi mbalimbali ambazo zimemsaidia kuwa na uwezo mkubwa katika kufundisha soka na wakati mwingine kuitwa kutoa mafunzo.
HIZI NDIO TIMU ALIZOWAHI KUZIFUNDISHA
Mkwasa amekuwa na bahati kubwa ya kuifanyia kazi taaluma yake aliyoisomea kwa kufudisha timu mbalimbali mbalimbali ndani na nje ya Tanzania na kizuri zaidi timu hizo zimekuwa zikifanya vizuri kwa kuonyesha soka la kuvutia.
Msimu wa mwaka 2011 alichukuliwa na timu ya Jeshi inayoshiriki ligi ya Vodacom Tanzania bara Ruvu Shooting ambayo aliiongoza kwa misimu miwili kabla ya kuchukuliwa na Yanga akiziba nafasi ya mchezaji mwenzake wa zamani wakiwa na Yanga Fredy Miziro.
Akiwa na kikosi cha Yanga kama msaidizi wa Hans van der Pluijm, katika kipindi cha miezi sita Mkwasa aliweza kuisaidia timu hiyo kumaliza Ligi ya Vodacom nafasi ya pili na baadaye yeye pamoja na boss wake kupata timu ya kufundisha nchini Saudi Arabia ujulikanano kama Al Shoalah.
Kwa bahati mbaya kibarua hicho kilidumu kwa miezi mitano kabla ya mkataba wao kuvunjwa na viongozi wa timu hiyo ya Al Shoalah FC,kutokana na kutotaka kutimiza maagizo ya benchi la ufundi ili kuipa ubingwa timu hiyo.
Miaka ya nyuma Mkwasa pia aliwahi kuwa na nafasi timu ya Reli ya Morogoro na baadaye kuhamia Dar es Salaam alipo jikita zaidi na maswala ya soka.
ALIISHAWAHI KUJIUZULU KUIFUNDISHA TAIFA STARS MWAKA 2011
Mkwasa kiungo maridadi wa miaka ya 1980 Decembar 2011 aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania bara Kilimanjaro Stars kwa ajili ya michuano ya Tusker Challenge Cup, akisaidiwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Hicho kilikuwa kipindi kibaya kwa Mkwasa kwani alipata upinzani mkali kuanzia katika kuchagua timu hiyo na hata mambo kumuwia magumu na kushindwa kutetea ubingwa huo uliokuwa unashikiliwa na Kilimanjaro Stars kwa kujikuta wakitolewa kwa aibu katika hatua ya nusu fainali kwa kufungwa mabao 3-1 na Uganda nyumbani.
Hiyo ilitokana na matokeo mabovu katika mechi za awali ambazo muda wote timu hiyo ilikuwa ikizomewa na mashabiki kutokana na kutoridhia uteuzi wa timu hiyo na baada ya kufungwa na Sudani kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu Mkwasa alitangaza kujiuzulu kuifundisha timu hiyo.
Licha ya kuachia ngazi Kilimajaro Stars TFF iliendelea kuwa na imani naye na kumpa kazi mbalimbali za timu za taifa na safari hii ilimkabidhi kikosi cha timu ya taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ lakini licha ya mazuri aliyofanya akiwa na kikosi hicho ikiwepo kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika zilizo fanyika Afrika Kusini mwaka 2012, kocha huyo alilazimika kujiuzulu kuifundisha timu hiyo kufuatia matokeo mabovu kwa kutolewa na Ethiopia kwenye kuwania kufuzu fainali kama hizo kwa kichapo cha mabao 3-1.
Mkwasa alijiweka pembeni na kuendelea na kazi yake ya kuifundisha klabu ya Ruvu Shooting iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu kabla ya kuchukuliwa na Yanga na hata alipo timuliwa kazi Saudi Arabia Shirikisho la Soka TFF, lilimchukua na kumpa kazi ya ushauri wa ufundi lakini alidumu kwa kipindi kifupi kabla Yanga kumrudisha tena kundini sambamba na Pluijm.
Kuitwa kwake ni imani ya kila Mtanzania mpenda soka kwamba timu hiyo itabadili matokeo yake na kupata matokeo mazuri hata kama itashindwa kufuzu katika fainali ambazo zipo mbele yake ila cha msingi apewe muda kutokana na weledi aliokuwa nao.